
Ligi Kuu Bara ni chachu ya vipaji na ndoto za wanasoka wanaotamani kufikia mafanikio ya kimataifa. Hata hivyo, changamoto ya miundombinu hususan hali ya viwanja vya mazoezi imekuwa inatishia maendeleo ya mpira wa miguu na afya za wachezaji.
Viwanja visivyokidhi viwango vimekuwa sehemu ya majeraha ya mara kwa mara, yanayoathiri uwezo wa wachezaji kushiriki kikamilifu kwenye michezo, huku baadhi yao wakilazimika kuacha mpira kutokana na majeraha, maumivu sugu au ulemavu wa kudumu.
Mfano ni kiungo wa zamani wa Yanga, Salum Telela aliyekuwa pia mchezaji wa timu ya Taifa Tanzania ‘Taifa Stars’ alilazimika kuachana na soka baada ya kukumbana na majeraha yaliyotokana na kufanya mazoezi kwenye uwanja mbovu.
Kiungo wa zamani wa Yanga na Mbeya City, Omega Seme alipatwa na matatizo kama hayo alipoumia akiwa mazoezini baada ya kuruka juu kuwania mpira kisha kutua kwenye eneo lililokuwa na shimo dogo na kupata majeraha yaliyomstaafisha mapema.
Vilevile mshambuliaji Yacouba Songne wa Tabora United aliwahi kupata majeraha kama hayo wakati akiwa Yanga alipokuwa anafanya mazoezi.
Ukubwa wa tatizo
Utafiti uliofanywa na mwandishi wa makala haya umebaini kuwa kati ya timu 16 zinazoshiriki Ligi Kuu Bara ni tatu pekee zinazofanya mazoezi kwenye viwanja vyenye nyasi sahihi, mifumo bora ya maji na matengenezo ya mara kwa mara.
Timu nyingine 13 hasa za nje ya Dar es Salaam zinategemea viwanja ambavyo havikidhi viwango vinavyotakiwa.
Changamoto za viwanja hivyo ni pamoja na nyasi bandia au ardhi ngumu, mashimo na sehemu zisizo salama, ukosefu wa vifaa vya msingi vya kusaidia mazoezi kama mipira, vifaa vya mazoezi ya mwili na uzio wa usalama.
Hali hiyo inawaweka wachezaji katika mazingira hatarishi na kuathiri maendeleo ya mpira wa miguu nchini na imekuwa na madhara kwa wachezaji katika nyanja mbalimbali.
Kifiziolojia, wachezaji wanakumbana na majeraha ya mara kwa mara kama vile mivunjiko, michubuko mikubwa na maumivu ya mgongo yanayotokana na mazoezi kwenye ardhi ngumu au maeneo yenye mashimo.
Kisaikolojia, wachezaji hupoteza morali ya kucheza kutokana na hofu ya kuumia, jambo ambalo pia linaathiri utendaji wao viwanjani wakati wa mechi za mashindano – changamoto ambazo zimekuwa mzigo kiuchumi kwa klabu ambazo hulazimika kugharamia matibabu ya wachezaji walioumia au kutafuta wachezaji mbadala pale majeruhi wanaposhindwa kupona kwa wakati.
Pamoja na kuwepo kwa kanuni za ligi zinazotaka viwanja vya mazoezi kufikia viwango, ukaguzi wa mara kwa mara huwa haufanyiki na hivyo timu nyingi zinaendelea kutumia viwanja visivyo na viwango.
Kiini cha majeraha
Daktari mkongwe wa tiba maungo (fiziotharapia), Gilbarte Kigadye anaeleza uhusiano uliopo wa kuumia wanamichezo na viwanja vyenye ubora mdogo, akisema: “Ukiangalia kwa haraka haraka huwezi kuona mwingiliano wa mambo hayo mawili, lakini ngoja nikupe mtazamo kwa kipengele kimoja baada ya kingine.”
Anasema, “Kiwanja cha mpira kikitengenezwa kina marefu na mapana pia, kwa kipa kule kwenda chini hivi ni mstari wa goli (goal line), kuna hii ambayo ni kushoto na kulia ‘touch line’
Dk Kigadye anasema vyote vikiwa sawa, pamoja na uwanja usio na majani marefu, yaani ukawa kwa viwango ambavyo vinahitajika kuwepo na vipimo maalumu, usio na mashimo, mchanga mwingi na maeneo yote yana majani ya kutosha, viwango vya wachezaji kuumia hupungua.
“Haina maana kwamba kila kitu kikiwepo hawa watu hawataumia ila afadhali tunapunguza nusu yake, kwa sababu kinachoanzisha kuumia kwa mchezaji ni mapungufu au changamoto ya ndani ya kiwanja, kikiwa na mchanga mwingi mchezaji anatumia nguvu kubwa kuliko kikiwa na majani.
“Kwa sababu kwenye majani viatu vinashika ‘njumu’ na anapata mwendo, kwenye mchanga akisukuma kwenda mbele anazama kwanza, halafu ndio asoge kwa hiyo meno yale yanatafuta pakukamata kwanza ndio anazama, ile pekee yake tayari kama mwili ulipotua kwenye ‘base’ ulipiga hesabu kuwa hii ni sehemu sahihi ya kushukia chini, hivyo nafasi ya mchezaji kuumia ni kubwa kama itajirudia rudia.”
Dk Kigadye anasema majani yanapokuwa mengi hukwamisha njumu, mchezaji anapotaka kugeuka kushoto au kulia, amegeuka njumu haikusogea tayari hapo unapata tatizo la ‘nise speng’ kulia au kushoto, ameumiza moja ya kiungo ndani ya goti tayari.
Anasema uwanja mzuri, lakini una mashimomashimo kama ataanguka na ana uzito mkubwa na pale anapotua anafikia juu ya gubu, goti la juu linatembea. Kama lililotua mwanzo ni mguu wa chini kwa sababu huu wa juu unatembea.
“Ndio maana tunapata haya majeraha mengi ya ‘ligament’ japokuwa wengine wanayapata kwa kugongana, lakini ‘crush landing’ mbaya kabisa ni hiyo… unatua na goti na mguu wa juu unateleza na wa chini unapata hayo majeraha ni kwa sababu ulikosea hatua ukaanguka.
“Tunaenda kuangalia kiwanja ‘touch line’ kuna nini kimewekwa, vipo vinavyowekwa mabomba ya kumwagilia (maji) yapo baada ya mistari hiyo mchezaji anatoka huko kasi anagongana na mwezake anaangukia nje ya uwanja anapata majeraha,” anafafanua.
Anasema hiyo ndiyo sababu refa akiona mchezaji amemsukuma mwenzake hata kama ni bega kwa bega halafu mmoja akaangukia nje ya kiwanja huwa ni faulo.
‘’Uwanja unaweza kuwa mzuri, lakini hauruhusu maji kutoka hasa kipindi cha mvua, hapo mchezaji anateleza kwa muda mrefu na hata kama hatateleza au hatapata majeraha ya nyama za paja ili kucheza tu dakika 45 bila kuteleza misuli pia inaanzisha maumivu kwa sababu imekaza.
Anasema maumivu hayo akicheza siku ya pili na ya tatu ni kama majeraha tayari na hivyo watu wengi hawafahamu kama anapocheza kwenye eneo la kuteleza anasababisha majeraha.
“Kiwanja kama ‘draining system’ itakuwa sio nzuri majeraha yatakuja, au hata kiwanja kikiwa na matope kiwango cha majani sio kizuri mvua inaponyesha tu kidogo inatengeneza tope, huyu akateleza na mwingine pia, Mungu saidia mkutane mikono sio miguu, ikitokea mmegongana kichwa hiyo ni ‘pure contusion injury’
“Kuna majeraha kabisa, kiwanja tumeshakiona kina hali hii mvua imenyesha kubwa sana mwamuzi anapima tu urefu wa maji, hapana wanatakiwa waangalie pia na je? Kuna kuteleza, kama uwezekano huo upo basi mchezo usichezwe,” anasema.
Dk Kigadye anataja kubadilika kwa mwelekeo ghafla bila mwili kuwa tayari mchezaji anaweza kupata majeraha kwenye goti.
Anasema kwa ujumla viwanja vina vitu vingi ambavyo vinasababisha wachezaji kuumia, hivyo unakuta kuna muunganiko mdogo unahitajika kutoka kwa mchezaji mwenyewe anavyojitunza katika mchezo ili uwanja uwe sababu kubwa ya yeye kuumia.
Anatolea mfano kujinyoosha kabla na baada ya mazoezi akisema suala hilo timu nyingi halizipi umakini na hata wanavyolifanya sio kwa ukubwa unaotakiwa.
“Mnapomaliza lazima muanze kucheza, kuna ile kupiga makofi ili muende kwenye hatua nyingine ya kujinyoosha.. ukiwaangalia kuna ambao wamemaliza na wengine bado,” anasema.
Anasema mchezaji anayechelewa akiendelea hivyo ndani ya msimu mzima, upungufu wa misuli yake unakuwa mkubwa, ikatokea akakuta utelezi kwenye uwanja na misuli yake sio imara, uwezekano wa kuchanika kwake ni mkubwa sana.
“Umetokea muunganiko wa mchezaji na ubovu wa kiwanja kwa pamoja vinazaa majeraha, huwa zinatokea katika hali tofauti kutokana na mtu na eneo wako katika hali gani wote wawili, kwani kila jeraha linaonyesha upungufu mahala,” anasema Dk Kigadye.
Nini kifanyike
Kwa mujibu wa Dk Kigadye tatizo liko sehemu mbili. Moja anataja ni taarifa ya kutosha kwa wanamichezo kuhusu majeraha, kujua wameumia kitu gani, wanaweza kutibiwa kwa namna gani, hasa hawa wachezaji wachanga.
Anataja kitu cha pili kuwa wanaocheza mpira wengi walitokea maisha ya chini, kwamba waufanye mchezo kuwa sehemu ya kipato, hivyo ukiwatafuta walioumia uwezo wao wa kujitibu unakuwa mdogo.
Anasema wengi wanakwama na ndoto inaishia hapo, kwa hiyo wanakuwa wengi kwa sababu hawakuandaliwa kwa kujua ili usipate tatizo hili, lazima wafanye hayo ambayo pia yanahitaji pesa.
“Wachezaji wanaoumia michezoni na hawana uwezo, ndoto imeishia hapo. Kuna watoto wa kiume na wakike wote hawa kwa sasa wanamuamko wa kucheza mpira, nadhani kuna taasisi nyingi za misaada zinakuja kwa sasa, kwanini zisisaidie na huku ili wapate matibabu kwa gharama rahisi wasipoteze uwezo wao,” anashauri Dk Kigadye.
Bosi Bodi ya Ligi
Akizungumzia mkakati wa maboresho ya viwanja, Mwenyekiti wa Bodi ya Ligi Tanzania, Steven Mnguto anasema wakati wakiendelea kushirikiana na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), ili kuhakikisha kwamba viwanja vya mechi vinakuwa na ubora, mpango huo utakuwa endelevu zaidi kwa msimu ujao.
Mnguto anasema kuanzia msimu ujao watahakikisha kila klabu inakuwa na uwanja bora wa mazoezi unachokidhi vigezo ili kuendeleza sera ya maboresho ya miundombinu.
“Tumekuwa na msimamo mkali tukishirikiana na wenzetu TFF kuhakikisha kila klabu inakuwa na uwanja bora wa kucheza mechi, hii inatokana na matakwa ya leseni ya klabu,” anasema Mnguto.
“Msimu ujao tutakwenda mbali zaidi, tutazitaka klabu kuwa na viwanja bora vya mazoezi kama vile vya kuchezea mechi, lengo letu hapa ni kuhakikisha wachezaji wanaandaliwa vizuri kuanzia kwenye eneo lao la mazoezi ili kuondoa changamoto kama hizi.”
Usikose kufuatilia mfululizo wa simulizi za wachezaji waliopata majeraha kwenye viwanja visivyokidhi viwango, na kuathiri uwezo wao kushiriki kikamilifu kwenye michezo, huku baadhi yao wakilazimika kuacha mpira kutokana na maumivu sugu au ulemavu wa kudumu.
Itaendelea kesho
Makala hii imeandikwa kwa msaada wa Taasisi ya Gates Foundation