Ubomoaji holela Kariakoo unavyoathiri kiafya wananchi

Dar es Salaam. Wakati ubomoaji usiofuata sheria ukikoleza hatari za kiusalama katika eneo la Kariakoo, Dar es Salaam, afya za wananchi wanaofanya shughuli zao au kwenda maeneo hayo nazo ziko shakani.

Kutokana na mazingira ya eneo la Kariakoo lenye maghorofa kila mtaa, wakati wa ubomoaji wa majengo yaliyopo katikati, inakuwa ngumu linaloathiri afya za wananchi.

Ujenzi ukiendelea katika Mtaa wa Raha huku wafanyabiashara wakiendelea na shughuli zao.

Eneo hilo si tu kwa ajili ya biashara bali pia kuna makazi ya watu, hivyo wanaoathirika na vumbi linalotoka katika majengo yanayobomolewa ni wengi na wa wakati wote.

Kwa mujibu wa uchunguzi wa Mwananchi, ubomoaji huo unaendeshwa kinyume na kifungu cha 55 cha Sheria ya Usalama na Afya Kazini ya mwaka 2003, kinachotamka ni haki ya wafanyakazi na umma kupata mazingira salama na kila mwajiri au mmiliki wa eneo la kazi anapaswa kuhakikisha usalama na afya ya wafanyakazi wake na watu wote walioko karibu na eneo hilo.

Nyumba iliokuwa Mtaa wa Sikukuu ikiwa inabomolewa chini wafanyabiashara wakiendelea na shughuli zao.

Si hicho tu, ubomoaji huo hauzingatii kifungu cha 47 cha Sheria ya Mipango Miji ya mwaka 2007, ambacho kinasema utekelezaji wa shughuli za kubomoa majengo lazima uzingatie mipango miji na usalama wa raia.

Wakati sheria zikieleza hayo, uchunguzi huo wa Mwananchi uliofanyika kati ya Juni – Oktoba 2024 umebaini shughuli za ubomoaji zimekuwa zikifanyika pasipo kuchukuliwa kwa tahadhari ambao umekuwa unasababisha madhara mbalimbali.

Katikati ya uchunguzi huo, Jumamosi ya Novemba 16, 2024 jengo la ghorofa nne katika Mtaa wa Congo na Mchikichi liliporomoka na kusababisha vifo vya watu 16, majeruhi 86 na uharibifu wa mali za mamilioni ya fedha.

Kutokana na ajali hiyo ambayo uokoaji bado unaendelea, Serikali imeunda timu nyingine ya uchunguzi wa majengo yote ya Kariakoo yenye wajumbe 19.

Ghorofa ya Shirika la Nyumba liliokuwepo mtaa wa Tandamti likiwa linabomolewa bila wahusika kuwa na vifaa maalumu.

Mbali na madhara hiyo, zinapo athari za kiafya ambazo zimekuwa hazipewi kipaumbele, zinazotokana na vumbi pale ubomoaji unapofanyika.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya wakazi na wafanyabiashara wa maeneo jirani wanasema wanashindwa kuishi kwa amani kutokana na athari za moja kwa moja za kimazingira, ikiwemo magonjwa ya mfumo wa kupumua.

Miongoni mwa waathirika wa vumbi hilo ni wafanyabiashara wanaozunguka jengo la zamani la DDC na wengine katika Mtaa wa Sikukuu na Aggrey; Congo na Tandamti wafanyabiashara 16 na wengine wenye maduka ya jirani.

Ahmed Othman, mfanyabiashara wa nguo anasema wamejikuta wakifuta vumbi mara kwa mara bidhaa zao na wao kutumia maziwa kutokana na vumbi linalotimka wakati wa ubomoaji.

“Vumbi limekuwa tatizo kubwa. Tangu ubomoaji uanze, nimeanza kupata matatizo ya kupumua. Siku ya kwanza nilipata kikohozi kikali, na baada ya wiki moja, nililazimika kwenda hospitali kwa ajili ya vipimo. Wakati wa kazi zetu, hatuwezi hata kufungua maduka yetu vizuri kwa sababu ya vumbi.”

Wakazi kwenye mitaa hiyo pia wanakutana na changamoto za kiafya. Abhijaya Latif, mama wa watoto wawili anayekaa Mtaa wa Tandamti/Sikukuu, anasema hali hiyo kwao ni changamoto na kuwa licha ya kufunga madirisha, vumbi linaingia ndani.

“Watoto wangu sasa wanaugua kila mara kutokana na vumbi, na hali hii imeathiri afya zao. Hii inatufanya tuendelee kutumia gharama kubwa kwa matibabu, kitu ambacho hatukukitarajia kabisa.

Pia, kelele zinazosikika wakati wa ubomoaji zinasababisha msongo wa mawazo,” amesema.

Wanasema pamoja na umuhimu wa mabadiliko ya kimaendeleo, kuna haja ya kuzingatia afya ya umma wakati wa kutekeleza miradi kama hii ya ubomoaji, ili kuzuia athari mbaya zinazoweza kudumu kwa muda mrefu.

Watoto na wazee

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, watoto na wazee ndio walio katika hatari zaidi kutokana na hali hiyo.

Daktari wa Hospitali moja iliyopo Iringa, Dk Amani Seif anasema kinga za miili ya watoto na wazee hazina uwezo wa kukabiliana na uchafuzi wa hali ya juu wa hewa.

“Watoto ni rahisi kupata maambukizi ya njia ya hewa kutokana na kinga zao kuwa dhaifu. Wazee nao wanapambana na magonjwa mengine, na hili vumbi linaweza kuwa mzigo zaidi kwao,” anasema.

Alibainisha vumbi linalotokana na ubomoaji wa majengo lina chembe ndogo ambazo zinaweza kusababisha matatizo makubwa ya kiafya.

“Chembechembe hizi huingia moja kwa moja kwenye mapafu, na mara nyingi huleta magonjwa ya muda mfupi kama vile kikohozi na homa za mara kwa mara. Kwa wale wenye magonjwa sugu kama pumu au mzio, hali inakuwa mbaya zaidi,” anasema Dk Seif.

Anasema madhara ya muda mrefu yanaweza kujumuisha saratani ya mapafu au magonjwa sugu ya mfumo wa kupumua kama vile COPD (Chronic Obstructive Pulmonary Disease).

Daktari mwingine, Grace Ndebaliba, mtaalamu wa afya ya mazingira, anazungumzia uwezekano wa kuwepo hatari inayosababishwa na kemikali kama asbesto kwenye maghorofa yanayobomolewa.

“Tunashuku baadhi ya majengo haya yaliyobomolewa yanawezaka kuwa na asbesto. Asbesto ni nyenzo inayotumika katika baadhi ya mabati ya zamani na insulation. Chembechembe zake, zinapovutwa, hujishikiza kwenye mapafu na zinaweza kusababisha ugonjwa mbaya wa asbestosis pamoja na saratani ya mapafu,” anasema Dk Grace.

Shirika la Afya Duniani (WHO) limeonya mara kadhaa kuhusu athari za kimazingira kutokana na ubomoaji wa majengo makubwa, likisisitiza umuhimu wa kuchukua hatua za tahadhari kama kunyunyizia maji ili kupunguza vumbi na kuweka mipaka kwa wale wasiohusika. 

Makandarasi wawajibishwe

Kwa mujibu wa Profesa Geraldine Kikwasi, utafiti wa Chuo Kikuu Ardhi ulibaini sheria na kanuni zilizowekwa kuhusu ubomiaji huwa zinakiukwa.

Anasema kuna kanuni za Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) zipo wazi zikielezea mwenye jengo, mchoraji na mjenzi wanachotakiwa kufanya.

“Kwenye ubomoaji ni lazima kuwe na vizuizi ikiwemo kuzungusha mabati na wanatakiwa kumwaga maji ili kupunguza vumbi huku wakihakikisha mtu akipita aweze kujua na kuweka tahadhari,” anasema Profesa Kikwasi.

Licha ya umuhimu wa kumwaga maji kulinda afya za watu, uchunguzi wa Mwananchi umebaini hakuna jengo kati ya yanayobomolewa yaliyozingatia tahadhari hiyo.

Katika kujibu swali hilo, mmpja wa makandarasi aliyezungumza na Mwananchi alisema jambo hilo halitekelezeki kwa sababu ya gharama na ili wasikose zabuni kuna vitu wanavipunguza.

“Kwa sababu ghorofa huwezi kuvunja siku moja na kila siku kabla ya kubomoa lazima kumwaga maji ili vumbi lisiende mbali, lakini hiyo ni vigumu kwa sababu gharama za kuita gari kwa ajili ya shughuli hii hapa inatakiwa awamu zisizopungua mbili,” anasema mkandarasi huyo aliyeomba hifadhi ya jina lake.

Kama una maoni kuhusu habari hii, tuandikie ujumbe kupitia WhatsApp: 0765864917.