
Washington. Rais wa Marekani, Donald Trump amefuta miradi kadhaa ya misaada ya kimataifa, ikiwemo mikataba inayounga mkono programu za kuzuia maambukizi ya virusi vya Ukimwi (VVU), polio na malaria katika baadhi ya jamii za nchi maskini duniani.
Tovuti ya The New York Times ya nchini Marekani imeripoti leo Jumamosi Machi Mosi, 2025 kuwa Taifa hilo limesitisha rasmi mikataba hiyo kupitia barua pepe na za moja kwa moja zilizotumwa katika taasisi zinazoratibu programu hizo.
Takriban mikataba 5,800 iliyo chini ya Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Marekani (USAID) imefutwa.
The New York Times limeripoti uamuzi huo unahusisha miradi muhimu kama vile misaada kwa wakimbizi, kliniki za kifua kikuu (TB) na mipango ya chanjo ya polio.
Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani inayosimamiwa na Marco Rubio, imekuwa ikifadhili programu nyingi za afya, elimu, utamaduni na sayansi duniani.
Mapema wiki hii, wizara hiyo ilituma barua pepe kusitisha ufadhili kwa kambi za wakimbizi, kliniki za TB, miradi ya chanjo ya polio na mashirika mengine maelfu yanayotegemea ufadhili wa Marekani katika shughuli za kuokoa maisha.
Imeeleza programu hizo zinasitishwa kwa masilahi ya Serikali ya Marekani.
Licha ya kuwa miradi mingi ilikuwa imeondolewa katika masharti ya kusitishwa kwa ufadhili kwa sababu ya umuhimu wake wa kibinadamu, sasa mingine imesitishwa ghafla.
Miradi iliyositishwa
Kwa mujibu wa barua hiyo, miradi iliyofutwa ni ya Dola za Marekani milioni 131 (Sh339 bilioni) za msaada wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (Unicef) kwa ajili ya chanjo ya polio, ikijumuisha upangaji, vifaa na usambazaji wa chanjo.
Pia imesitisha Mkataba wa ‘Chemonics’ wenye thamani ya Dola milioni 90 (zaidi ya Sh190 bilioni) zilizokuwa zinatumika kukabiliana na malaria na kunufaisha watu milioni 53 duniani.
Pia kuna mradi wa FHI 360 unaotekelezwa nchini Yemen, ukisaidia watoto wenye utapiamlo katikati ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vinavyoendelea.
Uamuzi huo haujauacha salama Mpango wa Shirika la Afya duniani (WHO) wa Global Drug Facility, ukitoa msaada kwa wagonjwa milioni tatu wa TB, wakiwemo watoto 300,000 waliokuwa wananufaika na matibabu kupitia mpango huo.
Mpango mwingine ni wa Elizabeth Glaser Foundation unaosaidia mapambano ya VVU na kufikia watu 350,000 Kusini mwa Afrika, pia mpango wa kufuatilia na kuchunguza maambukizi ya Ebola nchini Uganda.
Trump pia amesitisha utoaji wa Dola milioni 34 (zaidi ya Sh70 bilioni) zilizokuwa zinatumika kusambaza vifaa vya matibabu nchini Kenya, vikijumuisha masuala ya VVU, malaria na magonjwa mengine.
Amesitisha ufadhili wa makazi 87 nchini Afrika Kusini yaliyokuwa yanasaidia wanawake takriban 33,000 waliokumbwa na unyanyasaji wa majumbani.
Uamuzi huo pia umeathiri huduma za afya kwa watoto milioni 3.9 na wanawake milioni 5.7 nchini Nepal.
Programu ya ‘Helen Keller International’ inayojihusisha na matibabu ya magonjwa yasiyopewa kipaumbele Afrika Magharibi inayowafikia watu zaidi ya milioni 35 nayo imeathiriwa.
Uamuzi wa Trump umesitisha matibabu ya utapiamlo kwa watoto milioni 5.6 na wanawake milioni 1.7 nchini Nigeria.
Akizungumzia uamuzi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Utafiti wa Idadi ya Watu na Afya barani Afrika, Dk Catherine Kyobutungi, amesema utasababisha vifo lukuki akieleza idadi kamili huenda isijulikane, kwani hata programu za kufuatilia vifo nazo zimekatiwa fedha.
Uamuzi wa Serikali ya Trump ni mwendelezo wa usitishwaji wa misaada na ufadhili wa programu zilizokuwa zinasimamiwa na Serikali ya Shirikisho nchini humo.
Miongoni mwa hatua nyingine ni wafanyakazi wa USAID kutakiwa kuchukua likizo ya lazima isiyo na malipo.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.