Tyson aibuka na mpya kipigo cha Jake Paul

Texas, Marekani. Bondia Mike Tyson juzi alifanikiwa kumaliza pambano la raundi nane na kupoteza kwa kura za majaji dhidi ya Jake Paul.

Mashabiki walikuwa na hofu kubwa Tyson angeweza kupoteza pambano hilo raundi ya kwanza lakini mambo yalikuwa tofauti kabisa baada ya kuonyesha upinzani mkali hadi dakika za mwisho.

Staa huyo wa ngumi wa zamani amesema pamoja na kura hizo za majaji, lakini kwake pambano hilo ni ushindi mkubwa zaidi tofauti na watu wengi wanavyosema.

Tyson, mwenye miaka 58 ambaye ni bingwa wa zamani wa uzito wa juu alipigwa kwenye pambano hilo ikiwa ni mara yake ya kwanza anapanda ulingoni baada ya kupita miaka 19 ya misukosuko mingi.

Katika pambano hilo ambalo lilifanyika kwenye Uwanja maarufu wa AT&T Texas, Marekani, majaji walimpa Paul ushindi wa pointi 80-72, 79-73 na 79-73.

Akizungumza baada ya pambano hilo Tyson alisema kuwa: “Kila mmoja anajua hali inavyokuwa bondia anapopoteza pambano, lakini kwangu hili nimeshinda.

“Nimefurahi sana usiku huu na sijuti hata kidogo suala la kupanda ulingoni.

“Nilikuwa nakaribia kufariki mwezi Juni kutokana na afya kutetereka. Nilipambana hospitali na nashukuru nimeweza kuyashinda mambo yote na kupata tena nafasi ya kupanda ulingoni.

“Kuwaona watoto wangu wakiwa jukwaani wananiangalia namaliza pambano la raundi nane ni jambo zuri sana na nafikiri siyo kitu cha kuelezea zaidi bali ninachotakiwa ni kufurahi,” alisema Tyson.

Hata hivyo, baadhi ya mashabiki wamekuwa wakilitazama pambano hilo kama la kupangwa zaidi kwa kuwa zaidi ya mara tatu ilionekana Jake akishindwa kumpiga Tyson ngumi yenye nguvu, lakini mwishoni pia mwa pambano hilo kila mmoja alikuwa akisubiri kengele bila kujali kuwa ni nani ameshinda.

Tyson alionekana kushindwa kusimama vizuri dakika za mwisho, huku akiishiwa pumzi lakini mpinzani wake naye alikaa mbali na bondia huyo mkongwe huku akimpongeza hata kabla pambano halijaisha.

Hata baada ya pambano hilo, pamoja na kwamba Jake ambaye amezidiwa na Tyson kwa miaka 31, alishinda lakini alimsifu zaidi bondia huyo mkongwe  na kusema kuwa ni mtu mwema na bondia ambaye alikuwa akitamani sana kukutana naye ulingoni.

“Kwangu hili ni jambo zuri, kukutana na bondia mkubwa zaidi ulingoni ni kitu ambacho kila mmoja kinaweza kumvutia, kwangu ni heshima kubwa na nitaendelea kumpa heshima yake kwa kipindi kirefu kijacho,” alisema Paul.

Kauli ya Paul, mwenye miaka 27 inaonyesha kuwa hakuwa tayari kumuona mkongwe huyo anaanguka chini kwa kuwa ni tukio ambalo lingewaumiza mashabiki wengi ukumbini.

Hata hivyo, Paul alipoulizwa kama alishuhudia kuwa Tyson alishachoka, alisema aligundua hilo mapema sana, lakini bondia huyo mkongwe alikuwa mjanja.

“Nilitakiwa kuwapa mashabiki kitu kizuri, lakini sikuwa tayari kuwaumiza watu ambao hawakutaka wamuonea mkongwe wao  ameumia.

“Kwenye ukumbi nilikuwa nikirusha ngumi mashabiki wanatulia, akipiga yeye ukumbi mzima unapiga kelele ya kushangilia,” alisema.

Pambano hilo lilitazamwa na mashabiki 73,000 ikielezwa kuwa asilimia 80 ya mashabiki hao walikwenda kumuangalia Tyson zaidi kuliko Jake.

Vyanzo mbalimbali vinaripoti kuwa Tyson alipata kitita cha pauni 20 milioni huku Paul akilipwa pauni 40 milioni kwa ajili ya pambano hilo.