Twiga Stars na kundi la kifo Wafcon

Dar es Salaam. Timu ya taifa ya Tanzania ya wanawake ‘Twiga Stars’ imepangwa katika kundi lenye wapinzani watatu wagumu katika fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake (Wafcon) 2024 zitakazofanyika Morocco kuanzia Julai 5 hadi Julai 26, 2025.

Katika droo ya upangaji wa makundi ya mashindano hayo iliyofanyika jana Novemba 22 huko Casablanca, Morocco, Twiga Stars ilipangwa katika kundi C na timu za Afrika Kusini, Ghana na Mali.

Timu tatu ambazo zimepangwa na Twiga Stars katika kundi C la Wafcon 2024, zipo katika 10 kwenye chati ya viwango vya ubora wa soka kwa wanawake barani Afrika kwa mujibu wa viwango vya ubora wa soka vilivyotangazwa na shirikisho la mpira wa miguu duniani (Fifa) mwezi Agosti

Katika chati ya viwango vya ubora wa soka la wanawake Afrika, Afrika Kusini ipo nafasi ya pili, Ghana ikiwa nafasi ya tano na Mali inashika nafasi ya tisa.

Wakati wapinzani wake wote wakiwepo kwenye 10 bora, Twiga Stars yenyewe ipo nafasi ya 27 katika chati ya viwango vya ubora kwa soka la wanawake Afrika.

Timu ya taifa ya wanawake ya Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ ndio mabingwa watetezi wa Wafcon na kabla ya fainali zilizopita, walishika nafasi ya pili katika fainali za 2018.

Banyana Banyana imeshiriki mara mbili fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake na mara ya mwisho ilikuwa ni 2023 ilipoishia hatua ya 16 bora.

Timu ya taifa ya wanawake ya Ghana ‘Black Queens’ imeshiriki mara tatu fainali za kombe la dunia kwa wanawake ambapo zote iliishia hatua ya makundi.

Black Queens imeshiriki mara 12 tofauti katika fainali za Wafcon ambapo mafanikio yao makubwa ni kumaliza katika nafasi ya pili mwaka 1998, 2002 na 2006 huku ikiishia katika nafasi ya tatu mara tatu ambazo ni 2000, 2004 na 2016.

Mali ‘Majike ya Tai’ haijawahi kushiriki fainali za Kombe la Dunia lakini imecheza Wafcon mara saba zilizopita na mafanikio yao makubwa yalikuwa ni kumaliza katika nafasi ya nne katika fainali za 2018.

Ikumbukwe hii ni mara ya pili kwa Twiga Stars kushiriki Wafcon ambapo ya kwanza ilikuwa ni 2010 ilipoishia hatua ya makundi, ilipomaliza ikiwa na pointi moja iliyoipata katika mechi tatu.