
Juzi Ijumaa, timu ya taifa ya wanawake ya Tanzania ‘Twiga Stars’ ilifahamu kundi na wapinzani wake katika fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake (Wafcon) 2024 zitakazifanyika mwakani kuanzia Julai 5 hadi Julai 26 huko Morocco.
Katika droo ya upangaji wa makundi hayo ambayo ilifanyika Casablanca, Morocco, Twiga Stars ilipangwa kundi C na timu za Afrika Kusini, Ghana na Mali.
Hii ni mara ya pili kwa Twiga Stars kushiriki fainali za mataifa ya Afrika kwa wanawake ambapo ya kwanza ilishiriki katika fainali za 2010 zilizofanyika Afrika Kusini ambapo ilimaliza ikiwa imeshika mkia kwenye kundi lake ikitoka sare mechi moja na kupoteza mbili.
Kutoshiriki kwa muda mrefu fainali hizo za Afrika kwa wanawake hapana shaka kunafanya Twiga Stars kuwa na kibarua kigumu katika fainali hizo ambazo timu mbili zinazotinga hatua ya fainali zinafanikiwa kupata tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia la Wanawake.
Pia timu mbili zinazoishia hatua ya nusu fainali, zinacheza mechi za mchujo dhidi ya timu kutoka bara la Asia kusaka nafasi mbili za kucheza Kombe la Dunia la Wanawake ambalo fainali zake hufanyika kila baada ya miaka miwili.
Timu tatu zilizopo kwenye kundi C la Twiga Stars katika Wafcon sio nyepesina histori ya nyuma kwa kila moja inaonyesha kuna kazi kubwa ambayo Tanzania tunapaswa kuifanya ili kuhakikisha timu yetu inaleta ushindani na kufanya vizuri katika mashindano hayo badala ya kuwa msindikizaji kama ilivyotokea 2010.
Timu ya taifa ya wanawake ya Afrika Kusini ‘Banyana Banyana’ ndio mabingwa watetezi wa Wafcon na kabla ya fainali zilizopita, walishika nafasi ya pili katika fainali za 2018.
Banyana Banyana imeshiriki mara mbili fainali za Kombe la Dunia kwa wanawake na mara ya mwisho ilikuwa ni 2023 ilipoishia hatua ya 16 bora.
Timu ya taifa ya wanawake ya Ghana ‘Black Queens’ imeshiriki mara tatu fainali za kombe la dunia kwa wanawake ambapo zote iliishia hatua ya makundi. Iimeshiriki mara 12 tofauti katika fainali za Wafcon ambapo mafanikio yao makubwa ni kumaliza katika nafasi ya pili mwaka 1998, 2002 na 2006 huku ikiishia katika nafasi ya tatu mara tatu ambazo ni 2000, 2004 na 2016.
Mali haijawahi kushiriki fainali za Kombe la Dunia lakini imecheza Wafcon mara saba zilizopita na mafanikio yao makubwa yalikuwa ni kumaliza katika nafasi ya nne katika fainali za 2018.
Wasifu huo wa wapinzani wetu unapaswa kutushtua na kutufanya tuanze maandalizi ya mapema ili hadi pale mashindano yatakapoanza tuwe na uwezo wa kupimana nao ubavu na ikiwezekana tuwashinde.
Zama za kuingia kwenye mashindano kwa utetezi wa kusema sisi bado ni wachanga na hatuna uzoefu zimeshapita kwa vile hadi tunafika hapo maana yake Twiga Stars ni miongoni mwa timu bora 12 kwa mwaka huu katika soka la wanawake na ndio maana ikaweza kufika hapo.
Timu inahitaji kupata mechi nyingi za kimataifa za kirafiki dhidi ya timu bora na imara zaidi yetu ili ziweze kuonyesha ni maeneo gani tuna upungufu na kulipa fursa benchi la ufundi kushughulikia kabla fainali za Wafcon hazijaanza.
Tunao wachezaji wengi hivi sasa wanawake wanaocheza soka la kulipwa nje ya Tanzania ambao wanao huo uzoefu na wamepevuka kiakili tayari kwa kuweza kucheza mechi zenye ushindani mkubwa lakini tukumbuke kwamba kikosi pia kinaundwa na wachezaji baadhi wanaocheza ligi ya hapa nyumbani.
Tukipata mechi nyingi kubwa za kirafiki tutawasaidia hawa wachezaji wa ndani kuzoea joto la ushindani dhidi ya timu zenye majina na wachezaji wakubwa lakini pia zitasaidia kutengeneza muunganiko mzuri wa kitimu na wale wanaocheza nje ya nchi.
Ukiondoa mechi za kirafiki, pia timu hiyo inahitaji kupata kambi ya nje ya nchi kabla ya kuanza kwa fainali hizo za mataifa ya Afrika kwa wanawake.
Katika kambi hiyo kwanza kutakuwa na miundombinu bora na ya kisasa zaidi ya kufanyia mazoezi ambayo itawawezesha wachezaji kupata maandalizi bora zaidi kifizikia tofauti na hapa nyumbani.
Lakini pia kambi ya nchi itawezesha wachezaji kuwa na utulivu wa kiakili ambao utawafanya maandalizi yao yawe ya daraja la juu na yatakayowapa utayari wa kushindana na vigogo kwenye fainali hizo.
Wachezaji nao wanapaswa kujitunza katika kipindi hiki ambacho wanasubiria kufanyika kwa mashindano hayo ili wasipoteze viwango vyao ama kupata majeraha ambayo yataathiri ushiriki wao kwenye Wafcon.
Mashindano hayo ndio yenye thamani kubwa zaidi katika soka la wanawake barani Afrika hivyo tunapaswa kuyatumia vizuri kwa kuhakikisha tunaonyesha kiwango bora kuanzia mechi ya kwanza hadi ya mwisho ambayo tutacheza katika kipindi chote tutakachokuwa Morocco.
Wachezaji watapata fursa ya kujitangaza na kupata malisho bora zaidi ambayo yataboresha maisha yao, ndugu na jamaa zao siku za usoni.
Pia ni fursa ya kuitangaza nchi kwani yanafuatiliwa na kundi kubwa la watu ndani na nje ya bara la Afrika.
Mafanikio hayo ili tuyapate tunahitaji maandalizi bora na ya kisasa na sio ya kuungaunga.