
Unguja. Kwa mara ya kwanza Zanzibar imeandaa tuzo za umahiri katika mawasiliano ambazo zitashirikisha waandishi wa habari kutoka ndani na nje ya nchi.
Tuzo hizo ambazo zimeandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina Zanzibar, Taasisi ya Uhusiano ya Umma Tanzania (IPRT) na Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, zinatarajiwa kutolewa Julai 5 mwaka huu kisiwani humu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Ijumaa Aprili 18, 2025, Msajili wa Hazina Zanzibar, Waheed Mohammad Ibrahim Sanya amesema malengo makuu ya tuzo hizo ni kuhamasisha vyombo vya habari ndani na nje ya nchi kutoa taarifa za kina kuhusu maendeleo ya Zanzibar.
Amebainisha kuwa tuzo hizo pia zitalenga kutoa mafunzo kwa wandishi wa habari katika taasisi na mashirika ya umma katika maeneo maalum ili kuongeza mchango wao katika maendeleo ya jamii.
Kutoa mafunzo kwa watendaji wa serikali na bodi za wakurugenzi kwa taasisi na mashirika ya umma katika nyanja za utawala bora na mawasiliano ya kimkakati ili kuboresha utendaji serikalini.
“Tuzo hizi zitasaidia kuonesha fursa za kiuchumi ambazo zitavutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi na utengamano kwa jamii katika kuimarisha umoja kwa jamii ya Zanzibar na kuhifadhi utamaduni wa kizanzibar ambao ni urithi wa thamani kwa nchi,” amesema.
Hivyo, amesema ushirikiano huo pamoja unalenga kuhakikisha Zanzibar inakuja na mapinduzi makubwa ya kimaendeleo kwa kutoa taarifa sahihi zenye weledi zinazohusu miradi mikubwa inayotekelezwa na Serikali kwa faida ya umma.
Naye Mkurugenzi wa IPRT Tanzania, Dk Titus Solomon amesema tuzo hizo zimeandaliwa kwa ajili ya kuwatambua na kuwahamasisha wadau wa habari wakiwemo waandishi wa habari, maofisa habari wa mashirika na taasisi za serikali Zanzibar.
“Tukio la leo linatupa umahiri wa kuchochea uoni miongoni mwa wanahabari na maofisa habari kwenye taasisi mbalimbali za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na tunatambua kwamba uwazi na ushirikiano ni muhimu katika kuinua viwango vya utoaji wa habari na huduma kwa wananchi,” amesema.
Dk Titus alisema tuzo hizo zitakuwa na mchango mkubwa katika kuboresha mawasiliano ya umma hasa kutoa taarifa zinazogusa maslahi ya umma na zinazohusiana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotelekezwa na SMZ.
Mratibu wa tuzo kutoka IPRT Tanzania, Lufunyo Mlyuka, amesema ni za kimkakati zimelenga kuhamasisha matumizi mazuri ya lugha ya mawasiliano katika uandishi wa habari katika kufikia malengo ya habari.
Mapema, Meneja Uhusiano kutoka Shirika la Bima Zanzibar (ZIC Takaful) ambao ndio wadhamini, Juma Mmanga amesema hiyo ni fursa kwani kitu hicho hakikuwahi kufanyika Zanzibar
Akizungumza kwa niaba ya wadau wa habari, Salim Said Salim, alipongeza kufanyika kwa tuzo hizo Zanzibar kwani lina umuhimu mkubwa katika taaluma ya uandishi wa habari nchini.