Tuzo za uandishi bunifu; mcheza kwao hutuzwa?

Hayawi, hayawi, sasa yemekuwa. Hatimaye Tuzo ya Taifa ya Mwalimu Nyerere ya Uandishi Bunifu inatimiza miaka mitatu toka ianzishwe. Hatua inayofuata ni kuwatuza washindi ifikapo siku ya maadhimisho ya kuzaliwa kwa muasisi huyo wa Tanzania aliyekuwa mwandishi bunifu.

Majaji wamekwishachuja miswada bora na kuwasilisha orodha teule ya maandishi bunifu katika nyanja za riwaya, ushairi, tamthiliya na hadithi za watoto.

Majina 37 yamekwishatangazwa na tunachosubira sasa ni kujulishwa Jumapili ya Aprili 13 nani hasa watatuzwa kati yao. Majadiliano yanayoendelea sasa ni pamoja na ya kutabiri washindi na kubashiri miswada hiyo ina mada gani.

Bado tupo tunaojiuliza kuna faida gani kwa taifa kuwekeza katika uandishi bunifu katika zama hizi za sayansi na teknolojia. Badala ya kutafuta uhusiano katika ya maandishi bunifu na ubunifu wa kisayansi na kiteknolojia tunashangaa ya Wachina. Bahati nzuri historia ni Mwalimu mzuri tu.

Kisa kinasimuliwa kuhusu mazungumzo baina ya mwanasayansi maarufu, Albert Einstein na mama aliyetaka mwanaye awe mwanasayansi. Kila alipomuuliza mtoto wake asome nini inasemekana gwiji huyo alisema asome maandishi bunifu zaidi na zaidi. Kilichotokea ni kuwa mama alipinga akitaka jibu makini zaidi lakini, kwa mujibu wa blogu ya Maktaba ya Bunge la Marekani, mwanasayansi huyo alisisitiza kuwa maandishi bunifu huchochea ubunifu wa kisayansi.

Inaonekana mapinduzi yote ya viwanda, kuanzia ya kwanza hadi ya tatu na ya sasa ya nne yanayohusiana na teknolojia za kiroboti na kadhalika, yameendana na kuibuka kwa aina za uandishi bunifu unaochochea ugunduzi, uvumbuzi, na ubunifu.

Inathibitika hili liko wazi zaidi kwenye aina ya uandishi bunifu wa kisayansi wenye tabia ya kuandika kuhusu vitu vya kiteknolojia ambavyo bado jamii hata haijafikiria vinaweza kuwepo na kutumika. Inadhihirika vitu vilivyoanza kuzoeleka sasa kama magari yanayojiendesha yenyewe na mashine zinazofikiri kama sisi binadamu kupitia akili mnemba/bandia kwa kiasi kikubwa vilianzia kwenye maandishi bunifu.

Siyo jambo la kushangaza basi kuona kuwa baadhi ya waandishi bunifu waliowasilisha miswada yao kwenye Tuzo ya Mwalimu Nyerere wanatumia ubunifu wao kugusia au kubuni masuala ya kisayansi na kiteknolojia. Sijui kama wanajua kuhusu hicho kisa cha Einstein ambacho hata chenyewe kimekuzwa sana hadi kuonekana kuwa ni andishi bunifu. Sina hakika wanajua kuwa kazi zao zitakuwa kichocheo kwa watoto na vijana wa Tanzania kuwa wanasayansi na wanateknolojia lakini naamini kadri kazi zao zinavyosomwa zitachochea ubunifu wa vizazi vyetu.

Nimeona vyema kuwarejea wabunifu wetu wa kale, yaani wahenga, waliosema mcheza kwao hutuzwa kwa sababu hiyo.

Ni tuzo za aina hii za uandishi bunifu zinazotuleta pamoja kama taifa kukuza utamaduni, uzalendo, na ubunifu wa kitaifa. Nikiwa mdogo nilikuwa navutiwa sana na majalada ya matoleo ya vitabu vilivyokuwa vinaitwa ‘Fasihi ya Kisasa ya China’ kwenye maktaba nyumbani kwetu na nilikuwa najiuliza kwa nini wanavyo vingi hivyo. Nimeelewa sasa ukubwani.

Gwiji wa uandishi bunifu nchini, Shaaban Robert, atakuwa ameshalielewa hilo aliponena kuwa, “Lugha ni alama ya umoja wa taifa” na kusisitiza sana kuwa “umoja wa taifa hutaka sana lugha ya watu wote iwe kiungo cha kufahamiana na chombo cha kuchukua watu katika elimu na mapatano.”

Tunavyozalisha kazi nyingi za maandishi bunifu hasa kwa lugha inayoeleweka zaidi katika jamii yetu ndivyo mawanda yetu ya kiubunifu kama taifa yanavyopanuka.

Tunavyochochea uandishi bunifu katika maeneo mengi ndivyo tunavyopanua uchakataji wa maarifa. Tunavyowahamasisha waandishi bunifu katika tanzu anuwai ndivyo tunavyokuza wabunifu wengi wataotufikisha mbali.

Ukipitia mathalan orodha ya miswada kumi ya hadithi za watoto iliyoshinda mwaka jana utapata picha ya namna vinavyoweza kuchochea ubunifu kwa mtoto. Utakutana na majina ya miswada yenye mvuto kama ‘Tausi Msafiri’, ‘Kitabu cha Ajabu’ na ‘Ndoto ya Koja’. Ukitazama na orodha teule ya miswada bora ya hadithi za watoto inayowania tuzo ya taifa ya mwaka huu utaona kuna ‘Tembo Zimamoto’, ‘Siafu na Majimoto’, ‘Hatma Yangu’, ‘Mwisho wa Dharau, ‘Dirisha la Ajabu’, ‘Maua na Mji wa Maweni’, na ‘Maziwa ya Kuku’. Utagundua yanamvuta mtoto atafakari.

Anayedhani lugha yetu ya Taifa ni changa na maskini hata isiweze kubeba dhana za kisayansi na kiteknolojia ajitose kusoma vitabu vilivyochapishwa kupitia tuzo hii ajionee. Anayesema lugha yetu haiwezi hiki au kile afungue vifungo vya ubunifu vya akili yake aone jinsi maneno yatakavyoibuka kichwani. Anayeamini lugha yetu haitoshi arejee historia ya zaidi ya miaka elfu toka enzi za kutumia maandishi yatumiayo herufi za Kiarabu kuandika Kiswahili yaitwayo Ajami.

Jihoji una mchango gani katika kukuza na kuutuza uandishi bunifu. Jiulize kama leo Mwalimu Nyerere angefufuka angesema nini kuhusu mwamko huu wa ubunifu kwa Kiswahili.

Jibu lako lilinganishe na beti hizi za shairi la ‘Kilio cha Shaaban Robert’ alililochapisha katika gazeti la Ngurumo  tarehe 28 mwezi wa sita mwaka 1962 baada ya taifa kumpoteza gwiji huyo wa ushairi:

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *