Tuwalee wanafunzi kwa hoja si kwa viboko

Katika gazeti hili toleo la tarehe 5/3/2025 kulikuwa na kichwa cha habari: “Mwanafunzi afariki dunia kwa kipigo.”

 Halafu katika tolea la tarehe 6/3/2025, mhariri akaandika maoni ya gazeti  kwa kichwa cha habari kisemacho: “Viboko hadi kifo vikomeshwe shuleni.”

 Nampongeza mhariri kwa maoni hayo mazuri. Na kesho yake tarehe 7/3/2025 tukaona tena habari hii: “Sababu mwili wa mwanafunzi aliyechapwa viboko kuchelewa kuzikwa.”

Mimi kama mzazi na babu nasikitika sana kuona watoto na wajukuu zetu wakifia shuleni, ati wamepewa kipigo na mwalimu.

Nimetafakari maumivu ya wazazi wa mtoto Mhoja Maduhu (18) ambaye alifariki kutokana na kipigo cha mwalimu katika Shule ya Sekondari Mwasamba wilayani Busega mkoani Simiyu.

Siku si nyingi zilizopita, jambo kama hili lilitokea tena mkoani Kilimanjaro kwa mwanafunzi Jonathan Makanyaga wa darasa la kwanza.

Tena si hao tu. Tumesikia huko mwanzoni kuhusu wanafunzi kadhaa kufariki shuleni kutokana na vipigo vya walimu.

Tarehe 30/3/2021 niliandika makala katika gazeti hili iliyokuwa na kichwa cha habari: “Elimu bila viboko inawezekana”.

Naendelea na msimamo huo kwamba tunaweza kutoa elimu bora bila kuwachapa watoto au kuwaadhibu kisaikolojia,  kwa kuwadhalilisha kwa maneno au kwa matendo.

 Mimi nasimama na hoja hii kwamba tunaweza kulea watoto vizuri bila kuwachapa na tunaweza kutoa elimu bora kwa wanafunzi bila kuwachapa.

Ninaamini kwamba haya yanawezekana. Naomba niutetee hapa huo msimamo wangu.

Hoja yangu

Nianze na kueleza hapa utaratibu uliotolewa na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia,  kuhusu kuchapa wanafunzi shuleni.

Utaratibu ni kwamba wizara inarushusu mwanafunzi achapwe si zaidi ya viboko sita ikiwa ni kosa kubwa sana. Kawaida iwe ni kiboko kimoja, viwili, vitatu au vine. Tena anayeruhusiwa kuchapa ni mkuu wa shule au mwalimu mkuu.

Mwalimu mwingine anaweza kutoa hivyo vichapo kwa masharti kwamba ana ruhusa ya maandishi kutoka kwa mkuu wake.

Napongeza utaratibu huu ulio na nia ya kumlinda mwanafunzi asichapwe ovyo na asipate adhabu ya mateso makali.

Lakini mimi napinga kabisa adhabu yoyote ya kuchapa wanafunzi au kuchapa watoto nyumbani.

Napinga pia kumpa mwanafunzi au mtoto adhabu yoyote ya kumtesa kimwili, kiroho na kisaikolojia, akiwa peke yake au mbele ya wengine.

Kwa kifupi, napinga adhabu yoyote ya kumchapa, kumtesa, kumuumiza au kumdhalilisha mtu yeyote awe mtoto, mwanafunzi au mtu mwingine yeyote. Nitatoa sababu.

Mimi binafsi nilichapwa kidogo sana nyumbani na shuleni. Nakumbuka baba alinichapa fimbo chache siku moja na akaacha mara moja pale mama aliponikingia kifua. Tangu hapo sikuchapwa tena. Wadogo zangu hali kadhalika hawakuchapwa.

 Leo watoto wote tupo vizuri kimaisha, kijamii na kiuchumi. Hatukufika hapa kwa njia ya vichapo.

Tulilelewa kwa mafundisho ya kila siku, kwa mifano mizuri, kwa heshima kutoka kwa wazazi, babu, bibi, wanaukoo na jamii nzima kwa ujumla.

Wapo watoto majirani waliochapwa sana, sioni kwamba kuchapwa kuliwasaidia kufikia pale walipo sasa. Watoto wawili au watatu wa jirani waliochapwa sana hawajaendelea vizuri katika maisha.

Kitu kilicho wazi ni kwamba wao ni mabingwa wa kuchapa sana watoto wao na wake zao. Kumbe mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.

Sipingi kuchapwa kutokana na historia yangu binafsi, napinga kwa sababu kuchapa au kutoa adhabu nyingine yoyote ya kimwili au kisaikololojia,  ni mpango wa uonevu, mateso na udhalilishaji wa utu wa mtu mwingine.

Huko Marekani, sheria ya nchi hiyo inakataza mzazi au mlezi kumwadhibu kimwili au kisaikolojia mtoto.

Mwalimu au mzazi anayetoa adhabu anakabiliwa na vyombo vya sheria. Nchi nyingine kama za Ulaya, Canada, Japan na kadhalika zina utaratibu huo huo.
 Tunaziita nchi hizo ni nchi zilizoendelea. Naamini, pamoja na changamoto nyingi za kiuchumi, kifamilia na kijamii katika nchi hizo, bado wameendelea sana katika nyanja hizo bila kuchapa watoto wao na wanafunzi wao.

Sisi tunaochapa watoto na wanafunzi, mbona tunaendelea kuitwa nchi zinazoendelea na si zilizoendelea?

Kuna wazazi fulani hapa Tanzania walisema ati ni lazima mtoto kwa Kiafrika achapwe ndipo apate nidhamu. Upuuzi wa ajabu!

Watoto wote wanazaliwa sawa. Wote wanazaliwa na vipaji lukuki bila kujali taifa walimozaliwa. 

Wakoloni walitufanya watumwa, wakatuchapa kama punda, halafu sisi tunaendeleza ukoloni huu kwa watoto wetu na wanafunzi wetu.

Njia mbadala

Tufanye nini badala ya kuchapa na kutoa adhabu nyingine za kutesa watoto na wanafunzi?

Kwanza tukumbuke kwamba mtoto anazaliwa bila kosa lolote. Upungufu wote tunaouona katika watoto wetu, wameiga kwa watu wengine.

Wewe na mimi tunajitahidi kila siku kupunguza na kutokomeza upungufu wetu kama watu wazima, hivyo tuwape watoto nao wapate nafasi ya kujirudi na kujisahihisha.

Wewe unamchapa mtoto, nani anakuchapa wewe? Au unamchapa kwa vile yeye ni mdogo?

Mtoto au mwanafunzi huathirika kimwili na kisailokolojia anapochapwa au kuteswa kwa vipigo au kwa maneno ya kumdhalilisha. Kwanza anateswa kimwili na hii si haki. Pia anateswa kisaikolojia kwa kudhalilishwa mbele ya wengine.
Mtoto huyu au mwanafunzi huyu,  hupoteza kujiamini na hata kujiona kwamba yeye hana akili.

Watoto wanaochapwa na baba au mama huwaogopa wazazi wao. Hawana upendo kwa wazazi wao. Wanaishi kwa hofu.

 Mwalimu akiingia na fimbo darasani yule aliyechapwa jana anaogopa kiasi kwamba kufikiri kwake kunapungua, na hii humletea hofu ya kuchapwa tena.

Ni mzunguko wa kuchapwa, hofu, kuchapwa tena na kadhalika. Anayechapwa anaumia na anayechapa anakosa fursa ya kufikiri.

Wote wawili wanahitaji wapate uhuru, mwanafunzi uhuru wa kuwa mtu anayeheshimika, na mchapaji apate uhuru wa kutumia akili yake na kubuni njia mbadala za kumsaidia mtoto.

 Ziko njia nyingi za kuwasaidia watoto wanapokosea kitu. Kwanza tukumbuke kukosa ni ubinadamu.

Mtoto au mwanafunzi akifanya kosa, asahihishwe kwa utulivu na kwa busara. Mtu mzima unapomchapa mtoto ni kwamba unatumia hoja ya nguvu, si nguvu ya hoja. Unatumia nguvu za mwili wako, si nguvu ya akili yako na roho yako.

Ni rahisi kutumia nguvu ya mwili kuliko nguvu ya akili, lakini watu wenye busara na hekima hutumia akili na busara kuwakuza na kuwalea watoto na wanafunzi.  

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *