Tuujue Uislamu (27)

Assalaam alaykum wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

Katika vipindi kadhaa vilivyotangulia tumekuwa tukizungumzia sifa za Mwenyezi Mungu ambazo ni za dhati kwake na hakuna kiumbe mwenye sifa kama hizo. Katika sehemu ya 27 ya mfululizo huu leo tutaendelea kuzungumzia maudhui hii. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Sifa nyingine ya Mwenyezi Mungu ni hakim yaani mwenye hekima. Kwa maana kwamba, Mwenyezi Mungu ana hekima. Umakini katika mfumo wa uumbaji, kama ambavyo unatuongoza kwenye kuwepo kwa Muumba wa ulimwengu, pia unaonyesha irada yake ya busara katika uumbaji wa ulimwengu. Mtu mwenye busara ni anayefanya kazi zake kwa uangalifu na mpangilio, na mambo yake huyafanya kwa mipango na ratiba sahihi. Tunapotazama kwa ukaribu ulimwengu wa uumbaji na mfumo wake wa kustaajabisha, tunaelewa wazi kwamba mfumo huu uliumbwa kwa njia bora zaidi na kwa njia ambayo ilistahili kuumbwa. Njia bora ya kuthibitisha hekima ya Mungu ni kufikiria juu ya mfumo wa maisha na maajabu na uzuri wake. Ndio, ikiwa mtu atatazama kwa uangalifu na kwa uchunguzi na udadisi uumbaji wa mbingu na ardhi na viumbe vya ulimwengu, atagundua kwamba nidhamu na mpangilio wote huu pamoja na uimara wake ni mambo yanayoashiria elimu na hekima ya Mwenyezi Mungu. Kila siku sayansi na elimu ya binadamu inapiga hatua mpya katika kugundua siri za ulimwengu na mambo mapya. Kwa kusoma ulimwengu wa maumbile, wanadamu wamegundua kuwa, uwepo uliumbwa kwa ustadi na nguvu maalumu, na mbunifu wa ulimwengu huu alikuwa na ustadi na busara sana kiasi kwamba aliumba kila kitu kwa njia bora zaidi na kwa umbo kamili. Bila shaka kuna tofauti kubwa baina ya hekima ya Mwenyezi Mungu na hekima ya mwanadamu.

Kuwa na hekima kunamaanisha kujua mambo jinsi yalivyo, kuyatendea ipasavyo, na kumudu kila kitu mahali pake na kazi yake ipasavyo. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 88 ya Surat al-Naml kuhusu uumbaji wake:

Na unaiona milima unaidhania imetulia; nayo inakwenda kama mwendo wa mawingu. Huo ndio ufundi wa Mwenyezi Mungu aliye tengeneza vilivyo kila kitu. Hakika Yeye anazo khabari za yote myatendayo.

Hekima ya Mungu inaweza kushuhudiwa katika uumbaji Wake, na hasa katika uumbaji wa mwanadamu, pamoja na akili na nafsi yake. Mwenyezi Mungu anatuambia kwamba alimuumba mwanadamu katika umbo bora kabisa. Aya za 4-8 za Surat Tin zinasema: Bila ya shaka tumemuumba mtu kwa umbo lilio bora kabisa. Kisha tukamrudisha kuwa chini kuliko walio chini! Lakini wale walio amini na wakatenda mema, hao watapata ujira usio kwisha. Basi ni kipi baadaye kitacho kukukadhibishia malipo? Kwani Mwenyezi Mungu si muadilifu kuliko mahakimu wote? Mwenyezi Mungu ni Mwenye hekima ambaye huwapa hikima wale anao wapenda miongoni mwa waja wake.

 Mungu anasema: Yeye humpa hikima amtakaye; na aliye pewa hikima bila ya shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili.

Kwa hakika Mungu huwapa watu fulani uwezo wa pekee wa kuchunguza matatizo na kupata masuluhisho yanayoweza kutekelezeka, ambao wanapokabiliwa na matatizo au ugumu wanaweza kupima kila jambo kwa njia ifaayo na yenye usawa. Hawa ni watu ambao wengine hushauriana nao na kuwategemea katika nyanja mbalimbali za maisha yao. Watu wengine wana hekima kuhusu masuala ya kijamii. Wengine wana hekima linapokuja suala la mahusiano baina ya watu. Wapo wenye busara linapokuja suala la uchumi.

Kama tulivyoashiria huko nyuma ni kwamba, Mwenyezi Mungu ameumba mfumo wa uwepo kwa njia kamilifu na bora zaidi na hakuna dosari ndani yake, na hakuufuta na kuuumba bure. Mwenyezi Mungu anasema katika Aya ya 38 na 39 za Surat al-Dukhan kwamba:

Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo baina yake kwa mchezo  Hatukuviumba hivyo ila kwa Haki, lakini wengi wao hawajui.

Kwa hakika haya yote yanaonyesha na kuthibitisha hekima ya Mwenyezi Mungu. Kwani kikawaida kutokuwa na uwinao, kukosa ubora na upungufu wa kila kitu huwa ni natija ya ujahili na ujinga au udhaifu na kutokuweko uwezo wa kuifanya kazi hiyo mhusika.

Tumekubali kwa sababu zilizo wazi kwamba, Mwenyezi Mungu ana ujuzi na uwezo usio na kikomo na udhibiti kamili wa ulimwengu mzima na anajua ukamilifu na kutokamilika kwa kila jambo.

Wapenzi wasikilizaji kwa leo nalazimika kukomea hapa kutokana na kuumalizika muda uliotengwa kwa ajili ya kipindi hiki. Tukutane tena wakatii mwingine katika sehemu nyingine ya kipindi hiki.