Tuujue Uislamu (26)

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni tena katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

 Sehemu ya 26 ya mfululizo huu leo itaendelea kuzunghumzia sifa za Mwenyezi Mungu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

Miongoni mwa sifa zingine zinazotajwa kuwa ni za Mwenyezi Mungu au anazosifiwa nazo ni kwamba, Samiun Basir yaani Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusikia na Mwenye kuona, sifa ambazo zimekaririwa pia katika Qur’ani Tukufu.

Makusudio ya kumnasibisha Mungu kwa sifa hizi mbili, sio kuona na kusikia kwa kawaida na kidhahiri kama ulivyo miongoni mwa wanadamu na wanyama, hata ahitajie masikio na macho. Uonaji kwa upande wa wanadamu na wanyama ni kwamba picha ya vitu inaonyeshwa kwenye retina ambayo ni nyama iliyo nyuma ya mboni ya jicho, kupitia mboni na lenzi ya jicho na huipeleka kwenye ubongo na kutoka hapo hadi kwa chanzo cha utambuzi. Kusikia kwa wanadamu na wanyama pia ni kwa njia ambayo mawimbi ya sauti hufika kwenye sikio, ambalo lina utando, mifupa na mishipa ya kusikia, na hupitishwa kutoka hapo hadi kwenye ubongo na kisha kwenye chanzo cha udiriki wetu. Lakini sivyo ilivyo kwa Mungu.

Yeye hahitaji macho na masikio na viungo vya kusikilizia. Kwa sababu yeye ni uwepo ambao si wa kimaada na ni muumbaji wa ulimwengu wa uwepo. Mwenyezi Mungu anaona lakini sio kwa kutumia vitu kama macho, na anasikia lakini sio kwa msaada wa viti kama masikio. Hii ni katika hali ambayo, wanadamu huona na kusikia kwa msaada wa vitu hivi.

 

Imam Ja’afar Swadiq (as) anasema kuhusiana na hili kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwenye kusikia na mwenye kuona, anasikia bila ya kutumia kitu cha kusikilizia na anaona bila ya vyenzo vya kuhisi, bali Yeye anasikia na kuona kwa dhati yake. Kama tutakuwa makini kidogo, tutaona kuwa, hakika na ukweli wa kuona na kusikia wa wanadamu ndio ule ni ufahamu wake wa kile kinachoweza kuonekana na kusikika, na viungo kama vile macho na masikio ni utangulizi wa kazi hii. Lakini anayeona au kusikia kwa maana halisi ni mwanadamu mwenyewe ambaye anaona vitu kwa udiriki wake au kusikia sauti kwa utambuzi wake na sio macho yake au masikio yake kusikiliza.

Lakini kwa kuwa yeye ni kiumbe wa kimaada, hana budi kutumia vitu vya kimaada ili aweze kuona na kusikia. Lakini kwa Mwenyezi Mungu hali ni kinyume kabisa, kwani Allah yupo mbali na ametakasika kabisa na sifa za kimaada na kwa msingi huo hana haja na nyenzo za kimaada ili aweze kufahamu kitu fulani. Yeye ana ujuzi na ufahamu wa yote yanayoweza kusikika na kuonekana. Bila shaka, kunasibisha sifa ya kuona na kusikia kwa Mwenyezi Mungu hakukomei kwa wakati fulani. Kwa sababu kuona na kusikia kunahesabiwa kuwa ni katika sifa zake za dhati na asili. Yeye ni Mwenye kuona iwe ni kabla au baada ya viumbe kuumbwa.

 

Ukweli wa mambo ni kuwa, msikiaji ambaye si Mwenyezi Mungu husikia kwa njia ya ala ya kimwili, ambayo huwa na nguvu yenye kikomo, na Muumba (swt) yu kinyume na hali hiyo, na hivyo hivyo kuhusu kauli yake “na kila mwenye kuona asiyekuwa yeye huwa kipofu” hivyo basi wanaosikia miongoni mwa wanyama na wanadamu nguvu ya usikivu wao ina mpaka uliowekwa, kwa hiyo sauti zilizo hafifu usikivu wao hauzifikii, kwa hiyo ni viziwi kwenye sauti hizo. Na zilizo kubwa miongoni mwa sauti zitokazo nje ya hali ya kawaida haziwezi kuvumilika, uziwi hutokea kwa kuraruriwa nazo, na zilizo mbali miongoni mwa sauti katika hali ya kwamba mawimbi ya hewa yanayozichukua sauti hizo hayafiki, yote hayo kwa asiyekuwa Yeye swt, ama yeye mtukufu kwake inakuwa sawa sauti ndogo na kubwa, ya karibu na ya mbali; kwa sababu mnasaba wa vitu Kwake ni mmoja, na mfano kama huo husemwa katika kuona na vionavyo.

Kwa hakika kuona na kusikia kwa Mungu bila ya kutumia nyenzo kunaonyesha ujuzi wake mkubwa na kunaonyesha ufahamu Wake usio na kikomo. Kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye muumbaji na muumba wa wanadamu, Anasikia wanayosema, anajua kikamilifu kile kinachoendelea ndani ya mioyo yao, na hakuna chochote kilichofichika Kwake.

Aya ya 19 hadi 20 za Surat Ghaafir zinaashiria jambo hili. Aya hizo zinasema: (Mwenyezi Mungu) anajua khiyana ya macho na yanayo ficha vifua. Na Mwenyezi Mungu huhukumu kwa haki; lakini hao wanao waomba badala yake hawahukumu chochote. Hakika Mwenyezi Mungu ndiye Mwenye kusikia Mwenye kuona.

 

Wapenzi wasikilizaji kutokana na kumalizika muda wa kipindi hiki sina budi kukomea hapa kwa leo nikitaraji kuwa mtajiunga nami katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh