Tuujue Uislamu (25)

Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji tunapokutana katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.

Sehemu ya 25 ya mfululizo huu leo na katika kukamilisha mjadala huu wa elimu ya Mwenyezi Mungu tutatumia Aya za Qur’ani Tukufu. Kuweni nami hadi mwisho wa kipindi hiki.

 

Kama tulivyoashiria katika kipindi kilichopita ni kwamba, elimu ya Mwenyezi Mungu haina mpaka na Aya mbalimbali za Qur’ani Tukufu zinaashiria hili. Miongoni mwa Aya hizo, ni hii Aya ya 59 ambayo iko katika Surat al-An’am ambayo inasema:

Na ziko kwake funguo za ghaibu; hakuna azijuaye ila Yeye tu. Na Yeye anajua kilioko nchi kavu na baharini. Na halidondoki jani ila analijua. Wala punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinacho bainisha. Kwa hakika kujua Mwenyezi Mungu kilichoko nchi kavu na baharini ni ishara ya wazi kabisa kwamnba, elimu yake imeenea kila mahali.

Kwa hakika hii ina maana kwamba, Allah anajua na ana habari ya mabilioni ya viumbe hai wadogo kwa wakubwa walioko chini ya bahari, mtikisiko wa matawi ya miti misituni, katika mabonde, milima na kuchanua na kufunguka maua na kadhalika. Kwa mujibu wa Aya iliyotangulia, hakuna jani linalondoka isipokuwa Alla anajua. Kwa maana kwamba, idadi ya majani na lahadha ya kutengana kwake na tawi la mti, wakati wa kuzunguka kwake hewani mpaka kufika ardhini. Kama ambavyo, hakuna punje katika giza la ardhi, wala kinyevu, wala kikavu ila kimo katika Kitabu kinachobainisha, yaani katika elimu ya Mwenyezi Mungu.

 

Kwa hakika Aya iliyotangulia inapinga mtazamo wa wale wanaamini kwamba, elimu ya Mwenyezi Mungu inaashia tu katika masuala jumla na makubwa na kwamba, hana elimu ya mambo madogo madogo. Ili kuchora ramani ya njia au mstari wa elimu isiyo na kikomo ya Mwenyezi Mungu, Qur’ani Tukufu inasema katika Aya ya 27 ya Surat Luqman:

Na lau kuwa miti yote iliyomo duniani ikawa ni kalamu, na bahari (ikawa wino), na ikaongezewa juu yake bahari nyengine saba, (ili kuandika maneno ya Alla), maneno ya Mwenyezi Mungu yasingeli kwisha. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu, Mwenye hikima.

Kwa mujibu wa Aya hii ni kwamba, lau miti yote iliyomo duniani itafanywa kuwa kalamu, haiwezi kuandika elimu ya Mwenyezi Mungu. Kwa maana kwamba, elimu ya Mwenyezi Mungu haina mwisho wala kikomo. Sifa nyingine ya Mwenyezi Mungu ambayo imetajwa katika utamaduni wa Qur’an ni uwezo na nguvu. Mwenyezi Mungu ni mmoja na kuwa na nguvu na uwezo ni miongoni mwa sifa zake za dhati na asili. Hapana shaka kuwa, nguvu za Mwenyezi Mungu kama zilivyo sifa zingine ni kamilifu na zisizo na kikomo. Mwenyezi Mungu ni Muweza mutlaki na ana uwezo wa kufanya jambo lolote.

 

Neno Qadir yaani mwenye uwezo ni katika sifa za Mwenyezi Mungu. Yeye ni muweza mutlaki. Kwa maana kwamba, Mwenyezi Mungu akitaka kufanya jambo lolote anaweza na hakuna wa kumzuia katika hilo. Yeye ni muweza wa kila kitu.

Ibara isemayo:: اِنَّ اللهَ علی کُلِّ شَیءٍ قَدیر

Yaani: Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu. Imerejewa mara nyingi katika Qur’ani tukufu. Mfumo na nidhamu inayotawala katika ulimwengu ni hoja ya wazi kwamba, Muumba ni muweza na mwenye uwezo. Aya ya 12 katika Surat al-Talaq inatubainishia na kutuwekea wazi uhakika huu:

Mwenyezi Mungu ni yule ambaye ameziumba mbingu saba, na ardhi kwa mfano wa hizo. Amri zake zinashuka baina yao, ili mjue kwamba Mwenyezi Mungu ni Mwenye uweza juu ya kila kitu, na kwamba Mwenyezi Mungu amekizunguka kila kitu kukijua vilivyo kwa ilimu yake.

Nukta moja muhimu katika maudhui ya uwezo wa Mwenyezi Mungu ni kwamba, akitaka kitu basi uwezekano wa kukifanya upo. Hata hivyo kufanya vitu ambavyo kimsingi ni muhali na visivyoingilika akilini ni jambo ambalo halina nafasi katika maudhui hii.

Kwa mfano mbili jumlisha mbili jibu lake ni nne. Sasa atokee mtu na kusema je, Mwenyezi Mungu anaweza kulifanya jibu la mbili jumlisha mbili likawa tano au tatu badala ya nne? Bila shaka jibu ni hapana. Na sababu ya hilo ni kwamba, hakuna jibu jingine lolote ghairi ya nne linaloweza kuchukua nafasi ya namba nne katika swali la mbili jumlisha mbili. Hii ni kutokana na kuwa, kufanya hivyo ni kinyume na akili na mantiki.

 

Wapaenzi wasikilizaji kwa leo tunakomea hapa. Tukutane tena siku nyingine katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh