
Ni wasaa na wakati mwingine wapenzi wasikilizaji tunapokutana katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu.
Katika sehemu ya 23 ya mfululizo huu leo, tutaendelea kujadili maudhui ya sifa za Mwenyezi Mungu. Ni matumaini yangu kuwa, mtakuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi. Karibuni.
Qur’ani tukufu inamsifu Mwenyezi Mungu Muumba wa ulimwengu kwa sifa bora kabisa. Wasomi na wanazuoni wakitegemea Qur’ani Tukufu na hadithi wamezigawanya sifa za Mwenyezi Mungu katika makundi kadhaa.
Kundi la kwanza ni sifa ambazo ni sehemu ya dhati ya Mwenyezi Mungu ambazo anasifiwa nazo ambazo kimsingi ni sifa azali na za milele katika ujudi na uwepo Wake. Kwa mfano tunasema, Mwenyezi mungu yu hai, mjuzi na Mwenye uwezo. Yeye anaona kila kitu, ana ufahamu juu ya mambo yote na daima yupo.
Kadhalika kwa kuwa dhati ya Mwenyezi Mungu ni kamilifu kwa kila hali na namna, yuko mbali kabisa na sifa zote ambazo zinaashiria nakisi, mapungufu, udhaifu, kutokuwa na uwezo na hali ya kuwa ni mhitaji.
Kuna sifa ambazo pia hunasibishwa na Mwenyezi Mungu baada ya Yeye Mola Muumba kufanya amali au jambo. Kwa mfano Yeye ni Muumba au mtoa riziki.
Sifa nyingine muhimu zaidi miongoni mwa sifa za Mwenyezi Mungu ni kutoonekana kwake kwa macho na kutokuwa na mwili. Kumesemwa mengi na kutolewa hoja mbalimbali kuhusiana na sababu za Mwenyezi Mungu kutoonekana kwa macho na kutokuwa kwake na mwili.
Kabla ya kuingia katika mjadala huu, tunakumbusha kwamba, kwa kawaida tunatambua kuwepo kwa vitu na matukio katika mazingira yetu kwa hisia zetu tano. Lakini ulimwengu wa uwepo haukomei tu katika kile ambacho hisia zetu huona. Katika mazingira yetu ya maisha, kuna vitu ambavyo haviwezi kuonekana na viko nje ya eneo la hisia ya nje na wakati huo huo, haviwezi kukataliwa kwa njia yoyote.
Kwa mfano, hatuwezi kuona nguvu ya mvutano kwa macho yetu, lakini tunaweza kuona athari yake kila mahali. Uhai na maisha, upendo wa mama kwa mtoto, furaha na huzuni, hasira na ghadhabu, upendo au chuki ambapo hakuna hata moja ya haya ambalo linaweza kuonekana kwa macho, lakini kupitia athari zake mtu anaweza kutambua uwepo wa haya. Mtu haioni hasira lakini anaweza kuona athari zake. Haiwezekani kuiona furaha lakini ni rahisi kuona athari za furaha na kadhalika. Kadhia ya Mwenyezi Mungu nayo iko namna hii. Haiwezekani kukana uwepo wa Mwenyezi Mungu kwa kutumia hoja kwamba, hatuwezi kumhisi kupitia hisia tano. Kwani ishara za uwepo wa Mwenyezi Mungu ni nyingi ulimwenguni kote kama vile mbingu, ardhi, nyota na kadhalika.
Ukweli wa mambo ni kuwa, Mwenyezi Mungu ambaye ataonekana kwa macho ya mwanadamu, kimsingi huyo sio Muumba, kwani atakuwa ana mpaka na mhitaji ambaye atakuwa anafungamana na zama na sehemu. Hii ni katika hali ambayo Mwenyezi Mungu yupo kila mahali na hakuna sehemu fulani ya ulimwengu ambayo iko tupu na uwepo wa Mwenyezi Mungu.
Katika Qur’ani imeelezwa bayana kwamba, hakuna uwezekano wa kumuona Mwenyezi Mungu. Lakini kuna Aya zinazobainsha Liqaullah yaani kukutana na Mwenyezi Mungu. Makusudio ya kukutana na Mwenyezi Mungu ni kukutana kihisia na sio kama ilivyo kukutana kwa mtu na mwenzake, kwani Mwenyezi Mungu hana mwili na wala haonekani kwa macho ya dhahiri. Baadhi ya wafasiri wa Qur’ani Tukufu wanasema kuwa, makusudio ya Aya hizo ni kushuhudia athari za nguvu za Mwenyezi Mungu katika medani ya Kiyama, ujira, adhabu na neema Zake. Maana nyingine iliyoelezwa ni kushuhudia kibatini na kwa moyo.
Siku moja Bwana mmoja alimuuliza Imamu Ali (as): Hivi umewahi kumuona Mungu wako? Imamu Ali akamjibu kwa kumwambia: Siwezi kumuabudu Mungu ambaye sijamuona. Bwana yule akamuuliza: Umemuona vipi? Imam (as) akajibu kwa kusema: Macho ya dhahiri katu hayawezi kumuona, bali nyoyo zinamuona na kumdiriki kupitia nuru ya imani.
Qur’ani ikiwa na lengo la kuweka wazi na bayana maudhui hii inazungumzia kisa cha Nabii Mussa (as) cha kutaka kumuona Mwenyezi Mungu. Aya ya 143 katika Surat al-A’raf inashiria tukio hili kwa kusema:
Na alipo kuja Musa kwenye miadi yetu, na Mola wake Mlezi akamsemeza, alisema: Mola wangu Mlezi! Nionyeshe nikutazame. Mwenyezi Mungu akasema: Hutoniona. Lakini utazame huo mlima. Ukibaki pahala pake basi utaniona. Basi alipo jionyesha Mola Mlezi wake kwa mlima, aliufanya uvurugike, na Musa akaanguka chini amezimia. Alipo zindukana alisema: Subhanaka, Umetakasika! Natubu kwako, na mimi ni wa kwanza wa Waumini.
Kwa leo tunakomea hapa. Tukutane tena katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.