
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni katika sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Tuujue Uislamu. Hii ni sehemu ya 22 ya mfululizo huu ambapo tutabainisha sifa za Mwenyezi Mungu.
Moja ya dalili na ishara nyingine ya kuwa Mwenyezii Mungu ni mmoja, ni kutokuwa kwake na mpaka, na kwa kuwa hana mpaka basi yeye ni mmoja. Katika kubainisha maudhui hii tunapaswa kusema kuwa, viumbe vyote ni vyenye mipaka. Kuwa na mpaka na kikomo kwa kitu chochote kunamaanisha kuishi mahali fulani. Kwa mfano, tukisema umri wa kawaida wa mwanadamu una mpaka wa miaka 120 ina maana kwamba, baada ya mwisho wa kipindi hiki, hakuna tena suala la kuishi na kubakia hai mwanadamu huyu. Lakini kama kutakuweko kitu ambacho hakina mpaka na muda maalumu, basi uwepo wa kitu hicho utakuwa hauna mpaka wala mwisho. Hii ni kutokana na kuwa, katika uwepo wa kitu hiki hakuna kitu kinachoitwa mpaka wa muda, sehemu na kadhalika. Sifa hii yenyewe ni hoja ya uwepo wa Mungu mmoja, kwani haiwezekani kutasawari viwepo viwili visivyo na mpaka. Sababu na hoja nyingine inayotolewa na wasomi kuhusiana na kumpwekesha Mwenyezi yaani ya kuwa Mungu ni mmoja tu ni kwamba, dhati ya Allah haijapatikana kwa kuunganika sehemu kadhaa, yaani, haijaundwa na sehemu tofauti kama ulivyo mwili ambao unaundwa na viungo kadhaa. Bali kimsingi uwepo wake hauna kiungo au sehemu.
Kwa mujibu wa yale tuliyoyaeleza katika maelezo ya tauhidi na kumpwekesha Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa mtazamo wa ulimwengu wa Uislamu, Mungu ni mmoja.
Kwa hakika Yeye Mwenyezi Mungu ndiye muumbaji na mratibu wa uwepo na hana mshirika au mwenzake duniani. Kwa mtazamo wa Tawhidi ya Kiislamu imani ya utatu, yaani Mungu baba, Mungu mwana na roho mtakatifu ambayo imeenea baina ya Wakristo ni batili na haikubaliki. Kwa mujibu wa nyaraka na ushahidi wa kihistroria, karne mbili au tatu baada ya kudhihiri Issa Masih (as), Wakristo walikuwa wakimuabudu Mungu mmoja.
Lakini baadaye, kwa sababu ya ushawishi wa mawazo na maoni ya dini na shule zingine, na vile vile kupotoka kifikra kwa viongozi wengine wa kanisa, mawazo ya ushirikina yaliingia katika jamii za Kikristo na wakatumbukia katika fikra ya Utatu. Katika Aya nyingi za Qur’an, Mwenyezi Mungu anakataa kwa uwazi kabisa mtazamo wa utatu na anasisitiza upweke wa Mwenyezi Mungu na usafi wa dhati yake na kujiweka mbali uhusiano huu usio wa haki.
Miongoni mwa Aya hizo ni Aya ya 72 ya Surat al-Maida ambayo inasema:
Hakika wamekufuru waliosema: Mwenyezi Mungu ni Masihi mwana wa Maryam! Na hali Masihi mwenyewe alisema: Enyi Wana wa Israili! Muabuduni Mwenyezi Mungu, Mola wangu Mlezi na Mola wenu Mlezi. Kwani anaye mshirikisha Mwenyezi Mungu, hakika Mwenyezi Mungu atamharimishia Pepo, na mahala pake ni Motoni. Na walio dhulumu hawatakuwa na wa kuwanusuru
Aidha Aya inayofuata ya 73 katika Sura hii nayo inasema:
Kwa hakika wamekufuru walio sema: Mwenyezi Mungu ni wa tatu wa Utatu. Hali hakuna Mungu ila Mungu Mmoja. Na ikiwa hawaachi hayo wanayo yasema, kwa yakini itawakamata adhabu chungu wale wanaokufuru.
Kwa hakika Qura’ni Tukufu inapinga vikali nadharia ya utatu na inabainisha bayana kwamba, Issa ni Mtume wa Allah.
Aya ya 75 ya Suta al-Maidah inasema:
Masihi mwana wa Maryam si chochote ila ni Mtume. Wamekwisha pita Mitume kabla yake. Na mama yake ni mwanamke mkweli. Wote wawili walikuwa wakila chakula. Angalia jinsi tunavyo wabainishia Aya, kisha angalia vipi wanavyo geuzwa.
Aya ya 171 ya Surat al-Nisaa pia imebainisha hakika na ukweli huu kwa kusema:
Enyi Watu wa Kitabu! Msipite kiasi katika dini yenu, wala msimseme Mwenyezi Mungu ila kwa lilio kweli. Hakika Masihi Isa mwana wa Maryamu ni Mtume wa Mwenyezi Mungu, na neno lake tu alilo mpelekea Maryamu, na ni roho iliyo toka kwake. Basi Muaminini Mwenyezi Mungu na Mitume wake. Wala msiseme: Utatu. Komeni! Itakuwa kheri kwenu. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mungu mmoja tu. Ametukuka Yeye na kuwa na mwana. Ni vyake Yeye vyote viliomo katika mbingu na katika ardhi. Na Mwenyezi Mungu ni Mtegemewa wa kutosha.
Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki umefikia tamati tukutane tena katika sehemu nyingine ya mfululizo huu.
Wassalaam Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh