Tuuheshimu mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani

Waislamu wa Zanzibar, kama wenzao wa Bara na sehemu nyingine duniani, walianza mwishoni mwa wiki kutekeleza ibada ya kufunga mwezi Mtukufu wa Ramadhani.

Kwa Waislamu, saumu ni moja ya nguzo tano za Uislamu, ambayo inawajibisha waumini kufunga. Ibada hii huambatana na matendo ya huruma kama kuwasaidia masikini, kufanya mema, na kujiepusha na maovu. Katika mwezi huu, Waislamu wanatakiwa kuepuka kula, kunywa, kuvuta sigara, kusema uongo, au kushiriki vitendo vya mahaba hata na wanandoa wao wakati wa saumu, ambayo huanza alfajiri na kumalizika jua linapotua.

Watu wa Zanzibar na wageni wanakumbushwa kufuata sheria na taratibu zilizowekwa na serikali katika kipindi hiki. Mwaka huu, tahadhari imetolewa zaidi kutokana na baadhi ya watu kupuuza sheria kwa kufanya vitendo vinavyowakwaza waumini wa Kiislamu, kama kula hadharani au kuvaa mavazi yasiyo na heshima.

Wale wanaokiuka sheria hizi huweza kupewa adhabu ya kifungo cha mwaka mmoja bila msamaha. Miaka ya nyuma, usimamizi wa sheria za mwezi wa Ramadhani ulikuwa mkali, lakini hivi karibuni kumekuwa na malalamiko kuhusu baadhi ya watu kuzivunja bila kuchukuliwa hatua stahiki.

Zanzibar pia ina sheria kuhusu mavazi, ambayo huweza kufumbiwa macho kwa nyakati nyingine, lakini husimamiwa kwa umakini zaidi katika mwezi wa Ramadhani. Mwanamke kuvaa mavazi mafupi kupita kiasi, kufichua mgongo, au kuvaa nguo nyepesi zinazoonyesha maumbile hadharani huchukuliwa kuwa kosa la jinai. Wanaokamatwa kwa makosa haya huweza kusukumwa jela au kuchapwa viboko.

Miaka ya nyuma, watalii waliokuwa wakifika Zanzibar wakiwa wamevaa mavazi mafupi walipewa masharti ya kununua kanga au kitenge kufunika miili yao. Waliokataa walitakiwa kurejea walikotoka, kwani Zanzibar haikuruhusu watu kutembea nusu uchi hadharani.

Sheria hii ilikuwepo tangu enzi za utawala wa Sultani na ilisimamiwa kwa ukali wakati wa uongozi wa Rais wa kwanza wa Zanzibar, Sheikh Abeid Amani Karume, hadi kifo chake mwaka 1972. Mzee Karume alisisitiza kuwa mtu ana uhuru wa kuvaa anavyotaka nyumbani kwake, lakini akifanya hivyo barabarani, atapelekwa jela na kuvalishwa mavazi ya gerezani.

Nimeeleza haya ili kuwakumbusha wageni, wakiwemo Wakristo kutoka Bara wanaofika Zanzibar kipindi hiki, kuwa endapo watafanya vitendo kama kula, kunywa, kuvuta sigara au kushiriki mahaba hadharani, wanaweza kukumbana na adhabu.

Ni muhimu kuheshimu sheria, mila na desturi za wenyeji, hasa zinapohusiana na imani yao. Kila nchi ina sheria zake, ambazo zinapaswa kuheshimiwa. Katika baadhi ya mataifa, kuvaa hijabu ni kosa la jinai na wanaovunja sheria hiyo hukumbana na adhabu kali. Kwa hivyo, haipaswi kuwa ajabu kwa Zanzibar kuwa na sheria zake zinazotofautiana na sehemu nyingine.

Rais Hussein Mwinyi, katika hotuba zake za kuukaribisha mwezi wa Ramadhani, amewataka waumini wa dini zote kuheshimu mwezi huu kwa kuepuka matendo yanayoweza kuwakera Waislamu walioko kwenye saumu.

Mara kwa mara, imetokea watu wanaokula hadharani au kuvaa mavazi mafupi kwenye maeneo ya wazi wakati wa Ramadhani kushambuliwa na watu wenye hasira, wanaoamini kuwa dini yao inadharauliwa.

Katika kipindi hiki, ambapo siasa na michezo zimeleta mgawanyiko miongoni mwa watu, mwezi wa Ramadhani umeendelea kuwa kitu kimoja kinachowaunganisha Wazanzibari.

Kwa miaka mingi, Waislamu na Wakristo wa Bara na Visiwani wameishi kwa kupendana na kuheshimiana licha ya tofauti zao za kidini. Utamaduni huu wa kuheshimiana unapaswa kuendelezwa.

Katika mwezi huu, wenye uwezo wa kifedha huwasaidia wale wenye hali duni kupata chakula na mavazi. Watu hutoa sadaka ya vyakula, vinywaji, na pesa, huku wengine wakigharamia futari kwa wasiojiweza katika misikiti na maeneo mengine.

Wapo pia wanaotoa msaada wa kifedha ili masikini waweze kusherehekea Sikukuu ya Idd el-Fitr baada ya kumalizika kwa mfungo. Viongozi wa serikali na wafanyabiashara wa Bara na Visiwani huandaa futari kwa makundi mbalimbali ya watu. Hata hivyo, kwa bahati mbaya, mara nyingi wanaonufaika si wale wenye uhitaji zaidi, bali watu wenye uwezo, huku masikini wakisahaulika.

Katika mialiko mingi ya futari, waliohudhuria hutumia magari ya kifahari, huku wale wasio na uwezo wakihesabika kwa vidole. Futari hizi mara nyingi huwa za kifahari kupita kiasi, hali inayokiuka maana halisi ya kusaidia wahitaji.

Ingawa Uislamu unahimiza kufuturisha, ni muhimu kuzingatia kuwa walengwa wanapaswa kuwa wale wanaohitaji msaada wa chakula baada ya kukaa mchana kutwa bila kula.

Kwa bahati mbaya, shughuli nyingi za kufuturisha siku hizi zimegeuka kuwa sehemu ya propaganda za kisiasa na matangazo ya biashara, badala ya kufuata maelekezo ya kidini ya kusaidia masikini.

Ni vyema Wazanzibari kulitafakari jambo hili kwa kina na kurejea katika maamrisho ya dini kuhusu futari na msaada kwa wahitaji katika mwezi huu mtukufu.