
Desemba 31, 2024 Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), iliwalipa fidia ya zaidi ya Sh 6.9 bilioni, wakazi wa Kijiji cha Ngombo Wilaya ya Malinyi, ili wahame kwa hiari baada ya kijiji hicho kuwa katika eneo nyeti linalopaswa kulindwa.
Hatua hiyo ilitokana na Serikali kutangaza eneo la kijiji hicho kupandishwa hadhi kuwa sehemu ya Pori Tengefu la Kilombero, hivyo kuwataka wananchi kuhama kwa hiari na kwenda vijiji vya jirani.
Sababu iliyotajwa kwa wananchi hao kuhama ni uharibifu wa mazingira unaohatarisha uhai wa mto Kilombero, unaochangia kwa kiasi kikubwa kupeleka maji Mto Rufiji, ambao ndio chanzo kikuu cha maji ya bwawa la kufua umeme la Mwalimu Julius Nyerere.
Baadhi ya wananchi hao wamehamia mikoa ya Lindi, Ruvuma, Pwani na vijiji vya Mlimba Kilombero, Biro, Mbalinyi na vinginevyo.
Jitihada za Serikali kuwahamisha wananchi hao na kuwalipa fidia, ni jambo la manufaa kwa Taifa kuliko wananchi hao kuendelea kukaa katika eneo hilo, huku ikibainika kuwa wanaharibu mazingira kwa kutishia kupotea kwa ardhi oevu, inayochangia kuwapo kwa maji ya Mto Kilombero.
Kwa jiografia, Kijiji cha Ngombo kilipaswa kiutawala kiwe Wilaya ya Kilombero, lakini kutokana na uanzishwaji wake kuwa na utata, ikalazimika wananchi hao wapate huduma za kiutawala katika Wilaya ya Malinyi.
Hata hivyo, tangu mwaka 1950 eneo hilo la kijiji na maeneo mengine, yalikuwa tayari ni hifadhi ya pori tengefu la Kilombero na kuanzia miaka ya 1990, Serikali ilianza juhudi za kurejesha maeneo hayo kutokana na umuhimu wake kiikolojia.
Kiukweli, mchakato wa kuwahamisha wananchi wa Kijiji cha Ngombo, ulikuwa mgumu na wenye kila aina ya changamoto kwa serikali ya mkoa wa Morogoro na aliyekuwa Naibu waziri wa mifugo na uvuvi wakati huo, Abdalla Ulega.
Nakumbuka Desemba 12, 2018, Ulega alifanya mkutano wa hadhara wa kuwashawishi wananchi hao kuhama, lakini ushawishi huo uligonga mwamba kutokana na sababu mbalimbali.
Hivyo kuhama kwa wananchi hawa sio ushindi pekee kwa Serikali, bali ni manufaa kwa Taifa kutokana na kile watalaamu wetu walichobaini kuwa eneo la kijiji hicho, ni sehemu nyeti yenye ardhi chepechepe na ardhi oevu, ikisaidia kutiririsha maji kwenda katika Mto Kilombero na kuunda mito Luwegu na Ruaha mkuu ambayo inalisha Mto Rufiji.
Ni vizuri kwa Serikali kupitia idara zake ikakumbusha majukumu yao ya kulinda maeneo yenye maslahi mapana ya taifa kama kulinda na kuhifadhi maeneo ya vyanzo vya maji, misitu na mapori, mipaka ya hifadhi za taifa za wanyamapori kwani maeneo hayo yanafanyiwa mno uharibifu.
Uharibifu unaofanyika kwa kasi kubwa ni uchomaji mkaa, kilimo holela, kukata miti kwa ajili ya kuvuna mbao ambapo zaidi ya hekta 469,420 za misitu kuharibiwa kila mwaka na kuhatarisha nchi kuingia katika hatari ya mabadiliko ya tabianchi.
Mradi huu wa kufua umeme wa Bwawa la Mwalimu Nyerere ilitarajiwa hadi kufikia mwishoni mwa Januari 2024, ujenzi wake uwe umefikia asilimia 96.28 na kuzalisha megawati 2,115 za umeme ambapo kiasi cha Sh6.5 trilioni kinatarajiwa kutumika.
Fedha hizo ni za Watanzania, sasa kwa nini fedha nyingi kiasi hicho zije kupotea kwa mradi kulegalega eti kwa sababu tu mitambo inakosa maji ya kutosha?
Tanzania, Afrika na dunia kwa jumla zipo katika kampeni ya kuondokana na matumizi ya kuni, mkaa na kuingia katika matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi, umeme na nishati nyingine ambazo ni salama kwa afya ya mtumiaji.
Uzalishaji wa umeme Bwawa la Mwalimu Nyerere unaonyesha mwanga katika kuelekea kwenye kuondokana na nishati ya kuni na mkaa ili Taifa liendelee kupiga hatua zaidi kiuchumi.
Hivyo ni lazima udhibiti ufanyike katika vyanzo vya mito ya Ruaha Mkuu, Kilombero na Luwegu. Tudhibiti kilimo kando ya mito, wafugaji wa asili, uvunaji miti katika misitu yetu usiozingatia sheria ili mito hiyo iendelee kutiririsha maji kwenda Mto Rufiji.
Natamani kuona hatua ya kuwahamisha wakazi wa Ngombo ili kurejesha uoto wa asili, ielekee na maeneo mengine yenye uharibifu mkubwa wa mazingira kando ya mito.
Tukicheza na nyani, tutakuja kuvuna mabua. Mito niliyoitaja ikiachwa ikaharibiwa, tujue Bwawa la Nyerere liko shakani.