
Serikali imekuwa na juhudi za kuhakikisha huduma za afya zinaboreshwa ili wananchi waweze kupata huduma bora za afya karibu.
Maboresho hayo yameenda sambamba na ujenzi wa vituo vya kutolea huduma, ununuzi wa vifaatiba, dawa na kuajiri watumishi.
Ni dhahiri upatikanaji wa huduma za afya kwa sasa siyo kama miaka mitano iliyopita. Hali imebadilika, vituo vya afya vimesogezwa karibu na makazi, lakini pia hata hospitali za wilaya na mikoa zimekuwa na huduma bora na si bora huduma.
Wakati Serikali ikifanya juhudi za kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora karibu kwa kujenga vituo, kuajiri watumishi na kuhakikisha dawa zinapatikana, wapo wanaosababisha wananchi waendelee kuteseka kwa kushindwa kuwa na vipaumbele.
Nasema hivi kutokana na hivi karibuni wajumbe wa Kamati ya uongozi ya mpango wa kunusuru kaya maskini (Tasaf) Taifa kutembelea kituo cha afya Nyabilezi na kubaini vifaa vya zaidi ya Sh210 milioni havitumiki kutokana na kituo hicho kuwa na umeme mdogo wa njia moja.
Kituo cha afya Nyabilezi kilichopo wilayani Chato mkoani Geita, kimejengwa kwa gharama ya Sh1.4 bilioni, ambazo ni fedha za mpango wa kunusuru kaya maskini (Tasaf) awamu ya tatu na kukamilika mwaka 2023.
Kukamilika kwa kituo hicho kuliwapunguzia wananchi wa kata ya Bukome na kata jirani zaidi ya 12,000 adha ya kutembea umbali wa zaidi ya kilomita 18 kwenda hospitali ya Wilaya ya Chato kutafuta huduma.
Baada ya kukamilika, Serikali ilitoa vifaa vya kisasa ili wananchi wahudumiwe karibu na kupunguza vifo pale mgonjwa anapohitaji huduma ya haraka, hususan mama na mtoto.
Kituo hicho, ambacho moja ya huduma zinazotolewa ni ile ya uzazi, yaani kujifungua, Serikali imetoa kitanda na taa kwa ajili ya upasuaji, kwa pamoja vikigharimu Sh17 milioni, mashine ya usingizi Sh80 milion, mashine ndogo ya kutakasia vifaa vya dharura ya Sh3 milioni na seti sita kwa ajili ya upasuaji mkubwa zenye thamani ya Sh12 milioni.
Vifaa vingine ni pamoja na seti sita kwa ajili ya upasuaji wa kina mama wanaoshindwa kujifungua kwa kawaida zenye thamani ya Sh12 milioni, friji kwa ajili ya kutunzia damu salama yenye thamani ya Sh80 milioni pamoja na hadubini inayotumika kwa ajili ya vipimo mbalimbali vya maabara yenye thamani ya Sh6 milioni.
Kama tujuavyo uzazi una changamoto nyingi na wanawake wengi matarajio yao ni kujifungua kwa njia ya kawaida, ila pale inaposhindikana hulazimika kukubali njia ya upasuaji ambayo itamnusuru mama na mtoto.
Uamuzi wa Serikali kuweka vifaa hivyo ilikuwa kuwasaidia wajawazito kupata huduma za dharura za upasuaji. Kwa kukosekana umeme wa njia tatu, kwa sasa wagonjwa wanaohitaji vipimo na hata kina mama wanaojifungua hulazimika kwenda hospitali ya Wilaya ya Chato.
Lile lengo la Serikali kusogeza huduma karibu linakuwa halina maana kwa kuwa bado wale wanaohitaji vipimo hawawezi kupata huduma stahiki Nyabilezi, hivyo safari ya kwenda wilayani bado iko palepale.
Kwa mujibu wa mganga mfawidhi wa kituo hicho, vifaa vilivyonunuliwa na Serikali vina zaidi ya miezi sita havitumiki na kama tujuavyo vifaa kukaa bila kufanya kazi, huharibika.
Lakini ili kituo hicho kiweze kupata umeme mkubwa zinahitajika zaidi ya Sh20 milioni, fedha hizi ni ndogo ikilinganishwa na afya na uhai wa wananchi wanaotegemea kituo hicho. Mbali na kutegemea mapato ya ndani, Chato kuna wafanyabiashara wa aina tofauti, wakiwemo wachimbaji wa madini ya dhahabu, wapo wazawa wanaoishi nje ya Chato, lakini pia wapo wanasiasa ambao wana uongozi, huku wengine wakijipanga kuja kugombea nafasi za uongozi.
Kama ingeitishwa harambee na kuomba kuchangia, ni dhahiri fedha hizo zingepatikana na kama zisingetosheleza halmashauri ingekuwa na jukumu la kuongeza kiasi kidogo na kituo kikaweza kufanya kazi kwa malengo yaliyotarajiwa.
Haina maana ya kuwa na majengo yenye vifaa vilivyogeuka kuwa mapambo kwa sababu tu hakuna umeme, huku wananchi wakikosa huduma na kuteseka.
Ni imani yangu Halmashauri ingewasiliana na Tanesco na kuomba kufungiwa umeme mkubwa kwa kulipa kwa awamu, ni dhahiri wangefikiriwa na yamkini wangeshapata huduma.
Uwepo wa vifaa vya mamilioni visivyotumika inawezekana hili halipo Chato pekee, yamkini vipo na maeneo mengine.