Tusichoke kuwapa vijana elimu ya afya ya uzazi

Nafahamu kuna mambo ni magumu mno kwa mzazi kuzungumza na mtoto wake, likiwemo hili la afya ya uzazi, wengi tunaamini kwamba kujadili masuala hayo ni kuhalalisha mtoto kuingia kwenye uhuni.

Dhana hii ipo kwa wazazi wengi, lakini ukweli ni kwamba usipozungumza na mtoto wako mwenye miaka kuanzia 10 na kuendelea basi tambua kwamba atatafuta wa kuzungumza naye na upo uwezekano akapewa ushauri ambao utamuangamiza badala ya kumsaidia.

Sasa kabla ya hilo kutokea uamuzi ni wako uzungumze na mtoto wako na kujibu maswali yake au umuache akatafute majibu hayo kwa watu baki ambao wanaweza wasiwe wazuri na wakamuonyesha njia isiyofaa.

Hivi karibuni nilipata fursa ya kushiriki mkutano wa wadau uliolenga kufanya tathmini ya mradi wa CONNECT unaotekelezwa na shirika la Save The Children mkoani Dodoma, ukijikita katika kuendeleza utekelezaji wa mbinu zinazoboresha matumizi ya uzazi wa mpango kwa wamama vijana wa mara ya kwanza.

Niliposikiliza kwa makini kilichobainika wakati wa tathmini ya mradi huo, nilibaini bado kuna kazi kubwa inahitajika kuhakikisha elimu ya afya ya uzazi inawafikia vijana, tofauti na hapo tutaendelea kuwaona watoto wengi wenye watoto.

Wasichana wengi huangukia kwenye mimba za utotoni kwa kukosa elimu na hurudia kuzaa tena kwa sababu hiyo hiyo.

Ingawa mimi si mtaalamu wa afya, huwa naguswa na miradi ya aina hii kwa sababu inawezekana ndiyo njia rahisi kwa vijana hasa wa rika balehe kupata elimu ya afya ya uzazi kwa kuwa mbele ya macho ya wazazi wanaweza kuonekana kuwa bado wadogo.

Binafsi naona ni heri mzazi ukawa tayari kuingia kwenye nafasi hii ya kuzungumza na kijana wako huenda ukamuepusha asiangukie mikononi mwa watu wabaya, nasema haya kwa kuwa utake au usitake ni lazima atafute majibu ya maswali yake.

Nakiri kuna ugumu na hata wataalamu katika eneo hili wanaeleza ilivyo ngumu kiasi gani kwa wazazi kuzungumza na watoto kuhusu mambo haya, lakini inawezekana kabisa endapo mzazi atatengeneza ukaribu na mtoto wake kiasi kwamba atakuwa huru kuzungumza naye chochote.

Kama una kawaida ya kuzungumza na mwanao tangu akiwa mdogo, kadiri anavyokua na kukutana na mabadiliko kwenye mwili wake itakuwa rahisi kwake kukwambia na hapo ndipo utakapomueleza kuhusu yaliyo mbele yake kutokana na mabadiliko hayo.

Kwa kufanya hivi tunaweza hata kupunguza idadi ya mimba za utotoni, kwa kuwa watoto watafahamu matokeo na athari za kujihusisha na vitendo vya ngono katika umri mdogo. Likifanikiwa hili, hata vifo vitokanavyo na uzazi vitapungua kwa vijana na watoto, kwa sababu wapo wanaopoteza maisha wakijifungua kwa sababu viungo vyao vya uzazi havijakomaa vya kutosha.

Nasema haya kwa kuwa nina ushuhuda wa mabinti kadhaa waliopata ujauzito bila kutarajia na ukifuatilia undani utabaini hawakuwahi kupata elimu ya kina kuhusu afya ya uzazi zaidi ya ile waliyofundishwa kwa pamoja kama mada darasani.

Kinachofundishwa shuleni kinaweza kisitoshe kama mzazi au mlezi hutaweka msisitizo, kwenye zama hizi za utandawazi wazazi hatupaswi kuona aibu kuzungumza na watoto wetu, tena kwa uwazi kabisa maana usipoziba ufa utajenga ukuta.

Kama wewe mzazi huwezi kuzungumza na mtoto wako kwa kuhisi kwamba umri wake ni mkubwa, basi mpeleke kwenye vituo vya afya ambavyo vinatoa huduma hizi au wakati mwingine muache awe huru kwenda mwenyewe akajifunze, ama kwa hakika atayafanyia kazi yale yanayomfaa.