TUONGEE KIUME: Unachotakiwa kumfanyia mwanamke anayejizeesha

Mara ya kwanza ulipokutana na mkeo, alikuwa malaika.

Alikuwa ni mwanamke mzuri, mrembo kupita maelezo. Alikuwa ni mwanamke anayeweza kubeba sifa zote tamu na bado akabaki na nafasi ya kupokea zingine.

Alikuwa ni mwanamke wa ndoto yako, mwanamke unayeweza kumtambulisha kwa ndugu na jamaa zako bila wasiwasi.

Kipindi kile ulikuwa unamuona kama Miss Tanzania, kama binti wa mfalme, kama staa wa filamu, alikuwa ameiva kama embe dodo katikati ya msimu wa maembe dodo kwa kumuangalia tu ulikuwa na kila sababu ya kumfanya mke wako.

Lakini ulipomuoa tu vitu vikaanza kwenda tofauti; wimbo wenu wa mahaba ukaanza kuimbwa nje ya ‘key’, mke wako akajisahau kwamba mwanamke ni maua, mwanamke ni pambo machoni mwa mumewe, akaanza kuishi kwa kutojijali, akaanza kujizeesha na kweli akazeeka; anashindia ‘makanga’ kutwa kucha, kichwa kina manywele kama ‘mwendawazimu’, ngozi yake haijui mafuta, hajui manukato mazuri yaani KAZEEKA.

Wakati huo wewe ukienda kazini unakutana na kina Shanteel, wanawake wanaochukia kuzeeka; ukiwatazama hivi ni kama kivutio cha utalii.

Sasa ukilinganisha haya unayoyaona nje na mkeo ni pilau na mlenda, vitu viwili tofauti. Hii hali inakukwaza sana, lakini hujui ufanyaje. Fanya hivi.

Ongea na mkeo

Wanawake wanadanganywa au wanajidanganya kwamba uzuri wa mwanamke siyo urembo ni akili na tabia, lakini ndani ya mioyo yetu wanaume tunafahamu huo sio ukweli — wanaume wote tunapenda wanawake wazuri kwa muonekano, wenye akili na tabia nzuri.

Ukitutolea kitu kimoja kati ya hayo hatutaishi kwa furaha.

Sasa kaa chini zungumza na mkeo ukweli wa jinsi unavyojisikia, mueleze jinsi gani unavyotamani kumuona hazeeki, mueleze jinsi unavyosikia raha ukimtazama akiwa amevaa magauni mazuri yaliyo kwenye fasheni, mueleze jinsi unavyopenda ukisikia ananukia, mwambie jinsi unavyopenda akisuka ‘knotless’.

Mwambie asijidanganye kwamba mwanamke ni akili ya maisha, kwamba kila senti ni lazima iende kwenye kununua mchanga wa kufyatua tofali za nyumba mnayojenga Mbezi hapana, mwambie ukweli kwamba hukumuoa aje kuwa msimamizi wa miradi ya ujenzi, bali aje kuwa mke, na mke ni uwaridi kwa mume, uwaridi kwako, lazima apendeze.

Mnunulie unavyovipenda

Waswahili wanasema; binamu yako akiwa ananuka kikwapa usimwambie kwa mdomo, nenda dukani, mnunulie pafyumu, mpelekee kama zawadi, fanya kwa kurudia ataelewa unachomaanisha.

Fanya hivyo kwa mkeo pia, nenda dukani mnunulie mabegi ya kike mazuri, magauni mazuri, manukato mazuri, mawigi mazuri na kila kitu unachopenda kumuona akiwa nacho, matokeo yake utayashangaa.

Wanawake wote ni wazuri wakiamua kuonekana wazuri, kwa hiyo Shantele wa ofisini kwako siyo mzuri kwa sababu ni mzuri kuliko mke wako, hapana, ni mzuri kwa sababu ameamua. Kwa hiyo mlazimishe mke wako aamue kuwa mzuri.