TUONGEE KIUME: Hivi kwa wanaume ndoa ni nini?

Ndoa ina tafsiri nyingi; Serikali inasema ndoa ni mwanamke na mwanamume waliokubaliana kuishi kama mke na mume.

Dini zinasema ndoa ni muungano mtakatifu unaobarikiwa na Mungu kwa madhumuni ya upendo, uaminifu, na kuendeleza kizazi.

Makabila yana tafsiri yake ya ndoa na jamii pia kwa ujumla wake ina tasfiri yake ya neno ndoa.

Lakini je, ndoa kwa mwanamume humaanisha nini?

Baadhi ya wanaume wanatafsiri ndoa kama kumuita mwanamke aje atumie pesa zako, kisha aone haitoshi, azoe marafiki zake ili washirikiane kula pesa zako zaidi.

Kisha ukianza kufulia marafiki zake waseme tumelelewa na kuhudumiwa na mama, mzee alikuwa anazingua tu, hajatusaidia kwa lolote, alikuwa mtu wa mitungi, wanawake na starehe.

Wengine husema ndoa ni kuamua kugharamika milele daima.

Mzee mmoja aliwahi kuulizwa na mwanawe, “Baba, ni gharama kiasi gani kuoa?” Akajibu, “Sijui mwanangu, bado naendelea kulipia.”

Kwa wengine, ndoa ni sawa na upofu, kwani mapenzi ni upofu.

Wapo pia wanaosema maisha ni ndoto nzuri za usiku, lakini ndoa ni kengele inayokukatiza usingizi huo mtamu.

Katika harusi za kidini, mfungishaji ndoa hutamka kuwa ndoa ni pingu za maisha. 

Jiulize, mara yako ya mwisho kuona pingu ilikuwa katika hali gani? Pengine uliziona pingu mtu alipokamatwa na polisi, ametekwa na magaidi, au zikiwa zinaning’inia kwenye kiuno cha askari anayemkamata mhalifu.

Hili linatosha kukufanya ujiulize je ndoa ni heri au ni shari hasa ukizingatia kwamba kuna methali ya Kiswahili inayosema “Ndoa ndoano”.

Wengine husema ndoa ni tatizo unalojiingiza mwenyewe ili utumie sehemu kubwa ya maisha yako kujaribu kujichomoa.

Wanasema ikitokea kwa mtekaji akasema  amemteka mkeo, jambo bora zaidi unaloweza kufanya ni kumuomba abaki naye.

Wapo pia wanaosema kuwa mwanamume bila kuoa hajatimia, lakini pia mwanamume bila kuoa hajateketea. Patamu hapo!

Wengine wanadai ukiona mwanamume anamfungulia mlango wa gari mwanamke kuna mawili, ama ndoa mpya au gari jipya.

 Ndoa pia inafananishwa na mchezo wa kadi wa ‘Last Card’, isipokuwa hapa kila kadi ni joker na zamu ya kucheza inakuwa ya mwenza wako.

Baadhi ya wanaume wanaitazama ndoa kama safari ya kupata mtu wa kukukera maisha yako yote, lakini wahenga wanasema, “Aliyebarikiwa ni yule aliyepata rafiki wa kweli, na mwenye baraka zaidi ni yule aliyepata rafiki wa kweli ambaye ni mke wake.”

 Kwa ujumla, tafsiri za ndoa kwa wanaume zina sura mbili; wapo wanaoiona kama kero isiyoisha, na wapo wanaoiona kama pepo ya amani na furaha.

 Lakini yote kwa yote, ukipata nafasi, jitahidi uoe. Ukipata ndoa njema, utafurahia maisha yako yote. Na hata ukipata ndoa mbaya, bado hutakuwa umepoteza, utakuwa mwanafalsafa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *