
Rais wa Tunisia Kaïs Saïed ameamua siku ya Alhamisi usiku, bila kutoa sababu zozote rasmi, kumfukuza kazi Waziri Mkuu Kamel Madouri, mtaalamu ambaye aliteuliwa mwezi Agosti mwaka jana wakati wa mabadiliko makubwa ya baraza la mawaziri, kulingana na taarifa kutoka ofisi ya rais.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Dakika 2
Matangazo ya kibiashara
Nafasi yake imechukuliwa na Sarra Zaafrani Zenzri, Waziri wa Vifaa, huku mawaziri wengine wakiendelea kushikilia nyadhifa zao, kulingana na tangazo rasmi.
Mnamo Februari 6, Rais Saied alimfukuza Waziri wake wa Fedha, Sihem Boughdiri Nemsia, katikati ya usiku, na nafasi yake kuchukuliwa na hakimu Michket Slama Khaldi.
Matatizo makubwa ya kiuchumi
Kaïs Saïed alionyesha kutoridhika katika wiki za hivi karibuni na hatua za serikali yake.
Tunisia inakabiliwa na matatizo makubwa ya kiuchumi na kifedha, huku kukiwa na ukuaji duni wa 0.4% mwaka 2024, kiwango cha ukosefu wa ajira cha 16% na deni sawa na karibu 80% ya pato lake la ndani (GDP).
Rais ana mamlaka kamili ya kuwafuta kazi mawaziri na mahakimu.
Mabadiliko makubwa mnamo mwezi wa 2024
Mnamo mwezi Agosti 2024, alifanya mabadiliko makubwa ambapo alimteua Kamel Madouri, mtumishi mkuu wa zamani aliyebobea katika masuala ya kijamii. Pia alibadilisha mawaziri 19, akihalalisha uamuzi wake kwa “maslahi ya juu ya Serikali” na masharti ya “usalama wa taifa.”
Mabadiliko ya waziri mkuu yanakuja huku kukiwa na hali ya wasiwasi ya kisiasa huku makumi ya wapinzani wakifungwa, wengine kwa miaka miwili, pamoja na wafanyabiashara na wanahabari. Katika msimu wa joto wa mwaka 2021, Kaïs Saïed alimfuta kazi waziri mkuu wake na kusimamisha bunge.
Tangu wakati huo amerekebisha Katiba ili kurejesha utawala wa rais ambapo yeye ndiye mwenye mamlaka yote.
Mashirika yasiyo ya kiserikali yanashutumu kurudishwa nyuma kwa haki na uhuru
Tangu kujipa mamlaka kamili, upinzani na mashirika yasiyo ya kiserikali nchini Tunisia na ya kigeni yamechukizwa na kurudishwa nyuma kwa haki na uhuru nchini Tunisia.
Kaïs Saïed alichaguliwa tena Oktoba 6, 2024, kwa kura nyingi (zaidi ya 90%) katika uchaguzi uliyogubikwa na idadi ndogo ya waliojitokeza kupiga kura kwa ushiriki wa kiwango cha chini cha 30%.
Kaïs Saïed ambaye ana uhusiano wa karibu na nchi jirani ya Algeria, ambayo inasaidia Tunisia kwa mikopo na usafirishaji wa hidrokaboni kwa bei nzuri, alivunja mazungumzo zaidi ya mwaka mmoja uliopita na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ambalo lilikuwa limetoa mkopo wa dola bilioni 2 (faranga za Uswisi bilioni 1.7) badala ya mfululizo wa mageuzi, hasa katika ruzuku ya bidhaa za nishati.