
Kwa mujibu wa mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto na pia Sera ya Maendeleo ya mtoto vyote vinatafsiri kwamba ili uwe katika kundi la mtoto ni lazima uwe na umri chini ya miaka 18.
Katika umri huo, mtoto anahitaji malezi ili aweze kuishi vizuri ,kushirikishwa ,kulindwa na kuendelezwa kiakili jambo ambalo kutokana na maendeleo ya teknolojia na ukuaji wa dijitali linakuwa gumu kutekelezwa na wenye jukumu hilo.
Malezi ni suala gumu zama hizi tofauti na zama zilizopita kwa sababu ya wimbi hilo la ukuaji wa teknolojia.
Serikali ya Tanzania kwa kujua umuhimu wa malezi na maadili katika zama hizi, mtoto akiwa shule, Wizara ya Elimu, inamlea na kumsimamia kupitia waraka wa elimu namba 6 wa mwaka 2022.
Japokuwa shuleni misingi na maadili imewekwa kumlinda mtoto lakini swali ni je, anapokuwa nyumbani ambapo kwa sasa wazazi hawapo karibu naye tena bali ‘tablets’ na kompyuta ndiye mlezi wake mku, nani anamsimamia?
Ukuaji huu wa teknolojia unamfanya mtoto kuona na kujifunza mambo mengi ambayo pengine mengine ni mabaya kwake, hapa ndipo wazazi na walezi tunakumbushwa kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia ili kudhibiti haya.
Mataifa mbalimbali duniani yamekua yakifanya jitihada za kuhakikisha kwamba kila taifa linalinda na kukuza utamaduni wa maadili yake kwa lengo la kudumisha amani, mshikamano umoja na maendeleo hasa kwa kuwachunga na kuwakuza watoto katika misingi bora.
Mwanasikiolojia Macqueline Francis amewahi kunukuliwa akisema: “Maendeleo ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano yamesababisha dunia kuwa ndogo kutokana na urahisi wa kupata taarifa mbalimbali chanya na hasi kupitia vya mawasiliano, hivyo watoto wana uwezo wa kupata taarifa zote zitakazowaathiri kimalezi.”
Macqueline aliongeza kuwa: “Mwingiliano wa tamaduni mbalimbali duniani kijamii, kiuchumi, kisiasa umesababisha kuporomoka kwa maadili na desturi yetu iliyopelekea malezi ya watoto kufuata tabia zisizofaa.”
Tafiti mbalimbali kuhusu makuzi na maendeleo ya mtoto zimeonesha kwamba tabia na maadili aliyonayo mtu mzima ni matokeo ya malezi aliyoyapata wakati wa miaka minane ya awali katika maisha yake, tujiulize katika maelezi ya watoto wa sasa hivi wakiwa watu wazima tabia zao zitakuwaje?
Kutokana na kasi kubwa ya ukuaji wa utandawazi ambao kwa kiwango kikubwa imeendelea kuathiri mila na na tamaduni za kitanzania na jamii kwa ujumla Dk Haji Mnasi ameandika kitabu kinachoitwa “Elimu na Malezi kwa Watoto Zama za kidijitali”
kitabu hicho kinatajwa kuwa miongoni mwa masuluhisho ya maadili na malezi katika zama hizi za utandawazi na ukuaji wa teknolojia.
Miongoni mwa mapendekezo ya Dk Mnasi katika kitabu hicho ni kuwaomba wazazi pamoja na jamii kufundisha watoto zaidi kuhusu desturi zetu.
Aidha, kitabu hicho kimependekeza kuwe na juhudi za Serikali katika kuimarisha mabaraza na madawati ya ulinzi na usalama wa mtoto ili kuhakikisha suala la maadili linajadiliwa katika vikao vyote kama ajenda ya kudumu.
Pia walezi kuwafundisha watoto usalama wa mitandaoni, kuwapa muda wa kucheza nje sambamba na kuongeza mawasiliano ya ana kwa ana na mtoto.