Tumpongeze Rais Samia sambamba na wanahabari, ila tukaze uzi

Mei 3 ya kila mwaka, dunia huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Uhuru wa Vyombo vya Habari.

Kwa wiki nzima iliyopita, nilikuwepo jijini Arusha, katika hoteli ya Grand Malia, kuhudhuria maadhimisho ya siku hii muhimu.

Kwa mujibu wa taarifa ya mwaka huu kutoka taasisi ya kimataifa ya waandishi wa habari wasio na mipaka (Journalists Sans Frontières – RSF), Tanzania imetajwa kuwa kinara wa uhuru wa habari miongoni mwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kimataifa, tumepanda kutoka nafasi ya 97 mwaka jana hadi nafasi ya 95 mwaka huu.

Mtu anayestahili pongezi za dhati kwa mafanikio haya ni Rais wetu, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan. Asante Mama kwa kutuongoza katika kuhakikisha uhuru huu muhimu wa habari unaimarika. Hata hivyo, kazi bado ipo, hasa ikizingatiwa kuwa huu ni mwaka wa uchaguzi.

Baada ya kurejea kutoka Arusha, nilipata fursa ya kushiriki kwenye Jukwaa la Wahariri (TEF), ambapo Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, aliwakumbusha waandishi wa habari na vyombo vyao kuhusu namna bora ya kuripoti kesi ya uhaini inayomhusu Tundu Lissu. Alisisitiza umuhimu wa kutoruhusu migongano kati ya waandishi na Jeshi la Polisi, ambalo lina jukumu la kulinda amani.

Balile aliwahakikishia waandishi kuwa amekutana na Kamanda Muliro ambaye alitoa dhamana kuwa waandishi hawatasumbuliwa wakiwa kazini, alimradi wawe na mavazi rasmi ya utambulisho wa ‘Press’ na vitambulisho halali. Kuwa na vifaa tu kama kamera au kipaza sauti hakutoshi kama kitambulisho.

Nilialikwa pia kwenye Kipindi Maalumu cha Star TV kujadili wajibu wa vyombo vya habari katika kuhamasisha amani kuelekea uchaguzi mkuu. Nilieleza bayana kuwa bado hatujatimiza wajibu huu ipasavyo. Vyombo vyetu vya habari vingi bado vinajikita kwenye kuripoti tu taarifa, mara nyingine kama kasuku, bila kuchambua ukweli wa kauli au taarifa, hata kama ni uongo wa wazi.

Kauli zinazohatarisha amani, kama “tutakinukisha” au zile zinazochochea uhasama, hazifai kuripotiwa kabisa.

Pia nilialikwa katika Kasri la Kikeke (Crown Media), nikiwa na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, kuzungumzia hali ya uhuru wa habari nchini.

Katika majadiliano hayo, nilieleza dhana ya “it takes two to tangle”, kuwa kwenye vurugu za kisiasa, kuna wahusika wawili:

Mvurugaji (mara nyingi ni mwanasiasa) na mlinzi wa amani (vyombo vya dola). Wakati mwingine, chanzo cha kutoweka kwa amani huweza kuwa vyombo vyenyewe vya dola.

Nilitoa mfano wa tukio la kudhibiti wafuasi wa Chadema wakati wa kesi ya uhaini kama mojawapo ya matukio ya aina hiyo.

Kwa heshima na unyenyekevu, nilimuomba Mama yetu, Rais Samia, aangalie upya kesi ya uhaini kama ilivyofanyika kwenye ile ya ugaidi iliyofutwa licha ya kuonekana kuwa na prima facie.

Kesi kama hii si tu kwamba inatishia amani yetu, bali pia inatia doa taswira ya nchi yetu kitaifa na kimataifa.

Nikamshauri Rais wetu, huyu Simba mdogo wa Kizimkazi, anaweza kulimaliza jambo hili kwa busara ile ile aliyotumia awali.

Hoja yangu kuu inabaki ileile: Je, kunaweza kuwa na uhuru wa habari pasipo uhuru wa kiuchumi kwa waandishi wa habari na vyombo vyao?

Mwandishi mwenye njaa anaweza kuwa huru kweli? Vyombo vya habari visivyojiweza kiuchumi, vinavyotegemea chanzo cha habari hata kwa usafiri, vinaweza kweli kuwa huru? Hali hii inazalisha utegemezi kwa “bahasha”, jambo linalodhoofisha uhuru wa kweli wa uandishi wa habari.

Tunayo mihimili mitatu rasmi: Serikali, Bunge, na Mahakama. Kisha tuna mhimili wa nne usio rasmi, Vyombo vya Habari.

Mihimili ile mitatu imepewa kipaumbele, fedha, heshima na ulinzi. Lakini vyombo vya habari vimeachwa kama mtoto yatima, bila anayejali, bila uangalizi. Hili ni jambo la kusikitisha.

Kwa mwananchi, nani muhimu zaidi kati ya Serikali, Bunge, Mahakama na Vyombo vya Habari? Bila shaka, ni vyombo vya habari.

Hata katika mapato ya taifa, tunatozwa tozo na kodi mbalimbali kugharimia huduma nyingine kama maji, umeme, mafuta na hata ruzuku kwa vyama vya siasa.

Lakini kwa nini vyombo vya habari, ambavyo ni nguzo ya nne muhimu ya demokrasia, havipewi ruzuku?

Tunapoelekea uchaguzi, kama tunataka kuhakikisha Watanzania wanapata habari sahihi na kwa wakati, ni lazima tufike mahali tuseme wazi kuwa Tanzania inapaswa kugharimia sekta ya habari kama ilivyo kwa mihimili mingine. Vyombo vya habari navyo vina wajibu wa kutimiza, lakini ili itimize vyema, lazima ipewe uwezo na mazingira bora ya kufanya kazi yake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *