
HIZI habari za timu mbalimbali maarufu barani Afrika kuanza mikakati ya kuchukua wachezaji muhimu na tegemeo wa timu zetu kubwa hapa nchini za Simba na Yanga hazitakiwi kuchukuliwa poa.
Ilianza kama utani tuliposikia Wydad Casablanca ya Morocco inamhitaji Stephane Aziz Ki. Tukaona kama ni tetesi za siku zote kumbe jamaa walikuwa siriazi buana.
Juzi kati wakaweka mpunga wa kutosha kwenye akaunti ya Yanga wakapewa ruhusa ya kumsajili kiun-go huyo wa kimataifa wa Burkina Faso na hivi sasa ataenda nao huko Marekani kwenye Fainali za Kombe la Dunia la Klabu.
Ghafla tunasikia Waarabu wengine Zamalek wamebisha tena hodi Yanga wakimhitaji straika fosi Clem-ent Mzize ambaye pia anawindwa na timu kadhaa za Libya na ana ofa pia Ufaransa na Hispania.
Hatujakaa sawa mara Nasredine Nabi na skauti wa Kaizer Chiefs wamekuja hapa nchini na inasemeka-na ujio wao ni kwa ajili ya kuwashawishi wachezaji kama Kibu Denis na Charles Ahoua wa Simba na Dickson Job wa Yanga wajiunge na timu hiyo ya Afrika Kusini.
Na hizo timu zinawataka wachezaji hao kwa kutumia ushawishi wa kiasi kikubwa cha fedha ambacho kiuhalisia klabu za hapa nchini haziwezi kuwapa kwa vile bado hazina misuli imara ya kiuchumi ambayo inaweza kuitumia kuwashawishi wachezaji kubakia.
Hili halitokei kwa bahati mbaya bali linachangiwa na timu zetu kufanya vizuri katika mashindano ya kimataifa hivyo timu vigogo Afrika zinaona kama zitaweza kunufaika na wachezaji hao ambao wamekuwa tegemeo la Simba na Yanga.
Wahenga walisema kizuri chajiuza na kibaya chajitembeza. Maana yake ni kwamba timu zetu zinapofi-ka hatua za juu ni fursa kwa wachezaji kuonekana na kuzitamanisha timu mbalimbali nje na ndani ya Afrika.
Katika Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga ilifika fainali msimu wa 2022/2024 na Simba ikaingia hatua kama hiyo msimu huu. Huo ni uchokozi tosha kwa wakubwa ndio maana nao wameamua kujibu mapigo kwa kuwazoa wachezaji wetu.