
Kwa hali ilivyo sasa na kwa kuwa hakuna dalili zozote za mabadiliko, watu wa Zanzibar wanaelekea kushiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba mwaka huu katika mazingira yanayofanana kwa kiasi kikubwa na yale ya uchaguzi wa mwaka 2020.
Uchaguzi huo ulidaiwa na baadhi ya vyama vya siasa na wapigakura kwamba uligubikwa na mizengwe isiyoelezeka.
Hata viongozi wa ngazi za juu wa Serikali ya Muungano na Chama cha Mapinduzi (CCM) walikiri hadharani kwamba yaliyojiri katika uchaguzi huo hayakutoa picha ya uchaguzi ulio huru, wazi na wa haki.
Licha ya kukosekana kwa hatua madhubuti za marekebisho ili kuonyesha kwamba kuna nia ya kuheshimu Katiba na sheria zilizopo, hasa zile zinazolalamikiwa, hakuna dalili zinazoashiria mabadiliko ya kweli.
Kwa kifupi, hali ya sasa inalingana na methali maarufu ya Kiswahili ya Zanzibar: “Kilichobadilika ni soji, punda ni yuleyule.”
(Soji ni mfuko mkubwa wa magunia unaobebwa na punda mgongoni pande zote mbili, hasa kubebea nazi.)
Sababu kubwa ya hali hii ni kwamba, Mkurugenzi wa Uchaguzi na wasaidizi wake waliosimamia uchaguzi wa mwaka 2020 bado ni walewale.
Aidha, Tume ya Uchaguzi imedai kuwa idadi ya wapigakura wapya imeongezeka kwa kiwango kikubwa kuliko ilivyotarajiwa, lakini mamia ya raia wa Zanzibar wanalalamika kunyimwa haki ya kujiandikisha.
Swali linabaki; inawezekanaje idadi ya wapigakura ipande, wakati idadi ya waliolalamikia kunyimwa haki hiyo pia ni kubwa?
Viongozi wa Serikali na wa Tume wamekuwa wakihimiza wananchi kushiriki uchaguzi kwa kusema kutofanya hivyo ni kukosa uzalendo. Lakini hali hii ni sawa na kumwambia mtu anayeteseka na njaa ale ashibe, ilhali hajapewa chakula.
Ni kauli zenye muonekano wa propaganda ya kitoto ya kama kumwamuru mtu akimbie wakati ulishamfunga miguu kwa minyororo.
Jambo hili la watu kunyimwa haki ya kupiga kura halijazungumzwa wazi na Tume.
Ikiwa madai hayo hayana ukweli, basi Tume inapaswa kufanya mikutano kila wilaya na kuwaalika wale waliodai kunyimwa haki wajitokeze, ili ukweli ujulikane.
Pia, Katiba ya Zanzibar inaeleza wazi kuwa uchaguzi ufanyike kwa siku moja. Lakini kumeibuka sheria mpya inayoelekeza uchaguzi ufanyike kwa siku mbili, hii ni kinyume cha Katiba. Tume haijatoa maelezo iwapo inafuata Katiba au sheria hiyo mpya ambayo inaonekana kukinzana na Katiba.
Badala yake, imeendelea kuwa kimya kana kwamba haitambui wala haisikii malalamiko haya, huku ikidai kuwa shughuli zake zinaendeshwa kwa uwazi.
Katika uchaguzi uliopita, mgawanyo wa majimbo ya uchaguzi pia ulizua utata. Kisheria, kila jimbo linapaswa kuwa na wapigakura wasiopungua 7,000.
Hata hivyo, kuna jimbo jipya la Fuoni lenye wapigakura 1,600 tu. Eneo lake ni dogo kiasi cha kulinganishwa na uwanja wa mpira.
Hili lilihitaji maelezo, lakini badala yake linazua maswali; je, jimbo hili liliundwa kwa mujibu wa sheria, au kwa ajili ya kumpendelea mtu fulani? Au ni “jimbo maalumu” la wanamichezo na viongozi wao?
Katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Habari yaliyopita, ofisa mmoja wa Tume alidai kuwa si sawa kwa waandishi wa habari kutangaza matokeo yaliyoandikwa na kutiwa saini na maofisa wa vituo na kisha kubandikwa ukutani.
Lakini kama ni siri, kwa nini matokeo hayo yabandikwe hadharani? Hili linaibua mashaka kuhusu uendeshaji wa uchaguzi.
Nimesisitiza mara kadhaa, na narudia tena, mwenendo wa maandalizi ya uchaguzi mkuu unatia mashaka. Inapaswa pawepo na maridhiano ya kitaifa ili kuepusha machafuko kama yale ya chaguzi zilizopita, ambayo yamesababisha vifo, ulemavu, watoto yatima na uharibifu wa mali.
Chaguzi zilizopita zilishuhudia makundi ya vijana wahuni tu, wakizunguka mitaani, wakiingia kwenye nyumba na kuwapiga raia.
Sasa hivi, kuonekana kwa vijana wanaofanya mazoezi mitaani na viwanjani kumeibua hofu kwamba huenda “mazombi” au “Janjaweed” hao wakarudi tena wakati wa kampeni na uchaguzi.
Waandishi wa habari pia wanalalamika kuwa vibali vya kuripoti kuhusu uchaguzi vinatolewa kwa waandishi “maalumu” tu, wanaoitwa “wanaokubalika”.
Hili linaibua maswali kuhusu upendeleo na uhuru wa habari. Tume inapaswa kuhakikisha kila mwandishi mwenye sifa anapewa haki ya kuripoti habari za uchaguzi, bila kujali chombo anachofanyia kazi.
Huu ndio uwazi unaotarajiwa kwa uchaguzi wowote unaoitwa ni wa huru, haki na uwazi.