
Dar es Salaam. Wakazi 14 wa Ifakara mkoani Morogoro wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakikabiliwa na mashtaka 52 yakiwamo ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na kutakatisha Sh2,721,401.
Mashtaka mengine ni kuongeza genge la uhalifu na kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine.
Washtakiwa hao wamefikishwa mahakamani leo Ijumaa, Machi 7, 2025 na kusomewa kesi mbili tofauti za uhujumu uchumi na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Nura Manja akishirikiana na Cathbert Mbilingi mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Franco Kiswaga.
Katika kesi ya kwanza yenye mashtaka 28, washtakiwa ni Yonas Mwombeki (21) Godfrey Kunemba (29 ), Ramadhani Libandika (22), Amdalah Liwewa (22), Nagwa Chonja (22), Dotto Yanila (20) na Aloyce Mwelenga (22) ambao wamesomewa kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2025.
Washtakiwa katika kesi pili yenye mashtaka 24 ni Kelvin Sauro (25) Sadam Mugwalo (24), ELias Mkemwa (29), Sadick Chotero (30), Shafii Magwila (28) Halid Kitowelo na Mendard Numbeki ambao wamesomewa kesi ya uhujumu uchumi ya mwaka 2025.
Kabla ya kusomewa mashtaka, hakimu Kiswaga amedai kuwa, washtakiwa hawatakiwi kujibu chochote kwa kuwa Mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi.
Pia, shtaka la kutakatisha fedha linalowakabili washtakiwa hao halina dhamana kwa mujibu wa sheria.
Hakimu Kiswaga baada ya kueleza hayo, alielekeza upande wa mashtaka kuwasomea mashtaka.
Wakili Manja amedai kuwa, katika kesi ya kwanza washtakiwa wanakabiliwa na mashtaka 28, washtakiwa wanadaiwa kati ya Januari mosi, 2025 na Februari 10, 2025 eneo lisilojulikana waliongoza na kusimamia genge la uhalifu kwa lengo la kutekeleza mipango ya udanganyifu kwa kusambazaji ujumbe wa simu usio rasmi na kujipatia Sh1,922,000 kutoka watu mbalimbali.
Washtakiwa kwa nyakati tofauti kati ya Februari 2024 na Februari 2025 maeneo yasiyojulikana, kwa nia ya kudanganya kupitia simu za mkononi zenye namba tofauti walisambaza ujumbe usio rasmi kwa watu mbali mbali.
Wakili Manja amedai baadhi ya jumbe hizo zilisomeka, “TCRA-M-PESA, Imefungwa akaunti yako ya M-PESA kwa msaada tembelea ofisi zetu ukiwa na barua kutoka POLICE na kitambulisho chako upate msaada wa laini yako asante.”
“Utaingiza hiyo hela kwenye namba hii, usajili ni Juma Ally Ramadhani, “TCRA-MPESA Akaunti yako IMEFUNGWA tafadhari tembelea office zetu ukiwa na kitambulisho au namba za NIDA.”
Mashtaka mengine yalikuwa ni kutumia laini ya simu iliyosajiliwa kwa jina la mtu mwingine, makosa wanayodaiwa kuyatenda kati ya 2024 na 2025 katika maeneo tofauti ndani nchini.
Washtakiwa hao walikuwa wakitumia namba za simu zilizosajiliwa kwa majina ya watu tofauti tofauti bila ya kutoa taarifa kwa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania( TCRA).
Katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu inadaiwa Januari 17, 2025, mahali pasipojulikana mshtakiwa Kunemba kupitia simu ya mkononi alijipatia Sh45,000 kutoka kwa Albert Kwilasa kwa njia ya udanganyifu akijifanya mwenye nyumba na kwamba kodi yake imeisha anatakiwa kumtumia fedha.
Katika mashtaka ya utakatishaji fedha inadaiwa kwamba kati ya Januari mosi 2025 na Februari 10, 2025 katika sehemu isiyojulikana walijipatia Sh1,922,000 wakati wakijua fedha hizo ni za udanganyifu.
Katika kesi ya pili, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 24 likiwamo la kuongoza genge la uhalifu na kufanya utakatishaji wa Sh799,401.
Washtakiwa hao ni Kelvin Sauro (25) Sadam Mugwalo (24), ELias Mkemwa (29), Sadick Chotero (30), Shafii Magwila (28) Halid Kitowelo na Mendard Numbeki.
Katika kesi hiyo, washtakiwa hao pia, wanakabiliwa na shtaka la kuvuruga simu ya mkononi kwa kuwasilisha Imei namba za simu ya mkononi aina ya Tecno T. 301 ambazo vifaa vyake viliunganishwa na Imei namba za vifaa vya simu nyingine.
Washtakiwa baada ya kusomewa kesi zote mbili, Wakili Mbilingi alidai kuwa upelelzi wa shauri hilo haujakamilika, hivyo wanaomba tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Kiswaga ameahirisha kesi hadi Machi 20, 2025 itakapotajwa.
Washtakiwa wamerudishwa rumande kutokana na mashtaka yanayowakabili hayana dhamana kwa mujibu wa sheria.