
Demokrasia ya vyama vingi vya siasa nchini kwa sasa ina umri wa zaidi ya miaka 30, lakini kuanzia mwaka 2019 tulishuhudia maadui wawili wa demokrasia yetu ambao ni wagombea kupita bila kupingwa na uenguaji holela wa wagombea.
Tunalipongeza Bunge la Tanzania kwa kutuondolea adui wa wagombea kupita bila kupingwa baada ya kutunga sheria ya uchaguzi mkuu wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2024 iliyozuia mgombea yeyote kushinda bila kupigiwa kura.
Kabla ya sheria hiyo, tulishuhudia vituko vya aina yake katika nafasi ya ubunge na udiwani, ambapo magenge ya kihalifu yanayoungwa mkono na baadhi ya vyama vya siasa au wagombea, yalikula njama ili washindani wao wasirudishe fomu.
Tulishuhudia baadhi ya wagombea wa upinzani wenye ushawishi katika majimbo au kata, wakikamatwa na Polisi siku moja kabla ya siku ya mwisho ya kurejesha fomu au wengine kutekwa na magenge hayo hadi muda wa kurejesha fomu upite.
Wapo baadhi ya wagombea na wapambe wao walijenga urafiki na baadhi ya wagombea na kuwalewesha pombe na kujikuta wanalewa chakari hadi muda wa kurudisha fomu unapita na anapozinduka labda ni saa 10:30 au 12 jioni.
Lakini kubwa zaidi, wapo baadhi ya wagombea ubunge na udiwani wenye nguvu ya kifedha, waliweza kuwarubuni kwa rushwa, baadhi ya wagombea kutoka vyama vya upinzani ili wasirudishe fomu au watangaze kujitoa kugombea.
Sisemi wale wabunge wote 28 na madiwani zaidi ya 400 waliotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa walipita bila kupingwa kuwa walipitia njia hiyo, la hasha, ila lisemwalo lipo kuwa baadhi walitengeneza kupita bila kupingwa.
Katika uchaguzi wa serikali za mitaa nao wa mwaka 2019, CCM ilishinda kwa karibu asilimia 99, huku ikizoa mitaa yote 4,262 nchini na katika uchaguzi huo wagombea wao walipita bila kupingwa katika vijiji 12,028 na vitongoji 62,927.
Tunapongeza ujio wa sheria ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2024 katika vifungu vya 38, 54 na 66 vinavyoharamisha mgombea urais, ubunge na udiwani mtawalia, kupita bila kupigiwa kura katika sanduku la kura.
Vifungu hivyo vinasema endapo Tume itamtangaza mgombea pekee iwe ni kiti cha Rais, Bunge au Udiwani, basi mgombea huyo atalazimika kupigiwa kura ya ndiyo au hapana na atakuwa amechaguliwa kihalali kama atapata kura nyingi.
Leo sitazungumzia uzoefu nilioupata katika upigaji kura za ndiyo au hapana na mifumo ya kisheria ya uchaguzi kama inatoa hakikisho la uchaguzi huru na haki, lakini angalau sheria imeharamisha kupita bila kupingwa. Tunalipongeza Bunge.
Sasa nilitangulia kusema tuna maadui wakubwa wawili katika demokrasia yetu, lakini angalau adui yetu wa kupita bila kupingwa amekufa kupitia sheria niliyoitaja, sasa tuelekeze nguvu kwenye adui na kirusi cha kuengua wagombea.
Zimwi hili la uenguaji wagombea tulianza kuliona kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa 2019 kama nilivyoeleza na uchaguzi mkuu wa 2020 na sasa tumeshuhudia uchaguzi wa viongozi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024.
Ni katika uchaguzi huo, dunia ilishuhudia maelfu ya wagombea wa upinzani katika nafasi za vijiji, vitongoji na mitaa wakienguliwa na kuwafanya wagombea wa CCM kupigiwa kura ya ndiyo au hapana na kuifanya CCM kushinda kwa asilimia 99.
Sababu za kuenguliwa nyingine unaweza kuziona kama kichekesho cha karne, kwa sababu wapo walioenguliwa kwa sababu wameambiwa hawajui kusoma wala kuandika, lakini wakati wanaelezwa hivyo hawajawahi kupewa mitihani hiyo.
Wengine walienguliwa kwa sababu tu waliporudisha fomu zao, walikuwa wamejaza vizuri tu majina, umri na tarehe ya kuzaliwa, lakini zilipobandikwa ili kuruhusu mapingamizi, zilikutwa zimeongezwa herufi au tarakimu.
Wenzetu Kenya katika uchaguzi wao mkuu 2020, wagombea walienguliwa kwa sababu zenye mashiko kwelikweli, kwa mfano wapo wagombea walienguliwa kwa sababu shahada walizonazo zilitoka katika vyuo visivyosajiliwa na Serikali.
Wapo walioenguliwa kwa sababu waliwahi kuondolewa katika ofisi za umma (impeached), kuwasilisha vyeti feki vya kitaaluma, waliwahi kutiwa hatiani kwa makosa ya jinai na hawajawahi kukata rufaa na kukosa saini za wadhamini.
Kichekesho zaidi ni kuwa ukisoma takwimu za sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022, inaonyesha asilimia 83 ya watu wenye umri wa kuanzia miaka 15 na kuendelea, wanajua kusoma na kuandika.
Yaani takwimu hazidanganyi. Ni wakati muafaka sasa kukataa uenguaji kiholela wa wagombea, fomu zikaguliwe kama kuna dosari ndogo ndogo kama jina, tarehe ya kuzaliwa, basi mgombea apewe muda wa kurekebisha kama utaratibu wa mahakama katika kufungua kesi.
Tukiruhusu ushindi huu wa mezani, tunapata viongozi wasio na uhalali kisiasa na ndio hao wanang’ong’wa mitaani.
0656600900