Tuchel aanza na ushindi England, kinda Arsenal akiweka rekodi

England imeanza vyema harakati za kutafuta tiketi ya kushiriki Fainali za Kombe la Dunia 2026 baada ya kupata ushindi wa mabao 2-0 nyumbani dhidi ya Albania huku beki wa Arsenal, Myles Lewis Skelly akiandik rekodi mpya katika mechi hiyo.

Ushindi wa England jana umeifanya timu hiyo kuanza kwa kuongoza kundi K sawa na Latvia iliyopo nafasi ya pili ambayo nayo ina pointi tatu.

Mabao mawili ya Lewis Skelly na nahodha Harry Kane yaliipa England ushindi huo ambao umekuwa wa kwanza kwa kocha Thomas Tuchel tangu alipoanza kuinoa timu  na huo ukiwa ni mchezo wake wa kwanza pia.

Lakini ni bao la Lewis Skelly lililoibua historia mpya kwa kinda huyo wa Arsenal ambapo limemfanya awe mchezaji mwenye umri mdogo zaidi kuifungia England bao katika mechi ya kwanza kuichezea timu hiyo.

Skelly amefunga bao hilo akiwa na umri wa miaka 18 na siku 176 akivunja rekodi iliyowahi kuwekwa na nyota wa Aston Villa, Marcus Rashford ambaye yeye alifanya hivyo akiwa na umri wa miaka 18 na siku 209, Mei 2016 dhidi ya Australia.

Hakuishia kufunga bao tu bali pia Skelly alionyesha kiwango bora ambacho kimewakosha wengi wakimtabiria atakuwa mchezaji tegemeo kubwa kwa Arsenal na England siku za usoni.

“Hana woga. Anafanya kila kitu sahihi nje ya uwanja na ana umri wa miaka 18 tu. Nilijua atacheza kama hivyo kwenye mechi hii kwa vile amekuwa anajiamini,” amesema kiungo Declan Rice ambaye anacheza pamoja na Skelly katika vikosi vya Arsenal na England.

Kocha Tuchel amemuelezea Lewis Skelly kama mchezaji wa aina yake licha ya umri wake mdogo.

“Amekuwa wa kipekee kambini na anajiamini kupitiliza. na ni mtu mwenye uchangamfu mwingi na ana tabia za mtu aliyepevuka. Kila unachokiona uwanjani, unakiona nje ya uwanja.

“Anafanya hivyo kwa hali ya kujiamini ya asili na ndio maana anacheza soka,” amesema Tuchel.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *