Tubadili mtindo wa maisha kupata watoto wasio na usonji – Dk. Mollel

Na Nora Damian, Mtanzania Digital

Wakati Dunia ikiadhimisha Siku ya Usonji, Serikali imepaza sauti kwa jamii kupunguza uwezekano wa kupata watoto wenye tatizo hilo kwa kubadili mtindo wa maisha.

Kulingana na Shirika la Afya Duniani (WHO), mtoto mmoja kati ya 100 duniani anapatwa na ugonjwa huu, huku tafiti za Kituo cha Kudhibiti Magonjwa (CDC) za mwaka 2018 zikionesha kuwa watoto wa kiume wanaathiriwa mara nne zaidi kuliko watoto wa kike.

Hapa nchini hakuna takwimu rasmi za idadi ya watoto wenye Usonji, hivyo kutokana na makadirio ya WHO, Tanzania inakadiriwa kuwa na watoto 20,000 wanaozaliwa na tatizo hilo kila mwaka.

Naibu Waziri wa Afya, Dk. Godwin Mollel, amesema siku hiyo inayoadhimishwa Aprili 2 kila mwaka inalenga kuhamasisha uelewa juu ya uwepo wa tatizo hilo ikiwa ni pamoja na kuimarisha huduma za kiafya na kielimu.

“Ingawa hatuwezi kuzuia wazazi kupata mtoto mwenye usonji, tunaweza kuongeza uwezekano wa kupata watoto wenye afya nzuri kwa kufanya mabadiliko muhimu katika mtindo wa maisha.

“Hii ni pamoja na kula mlo bora, kufanya mazoezi mara kwa mara na kuhakikisha uchunguzi wa afya kabla na wakati wa ujauzito.

“Ni muhimu kushirikiana na wataalam kuhusu matumizi ya dawa na kuepuka vinywaji vyenye kileo kama pombe, kwani vinaweza kuathiri ukuaji wa mtoto na kuongeza hatari ya matatizo ya kiafya, ikiwa ni pamoja na ulemavu wa mfumo wa fahamu,” amesema Dk. Mollel.

Aidha amesema Serikali imeanzisha mafunzo ngazi ya Diploma ili kuongeza wahitimu wenye ujuzi na weledi ambao watatoa elimu kwa watoto wenye changamoto za usonji nchini.

Kwa mujibu wa Dk. Mollel, mafunzo hayo yanayojumuisha mbinu na mikakati ya kufundisha watoto wenye usonji, kutambua dalili za usonji, na jinsi ya kuwasiliana na watoto wenye usonji yanatolewa katika Chuo cha Ualimu Patandi Arusha.

Naibu Waziri huyo ametoa wito kwa jamii kutowaficha watoto wenye changamoto hizo na kuwataka wazazi na walezi kuwasiliana na wataalamu ili kupata elimu na kujifunza jinsi ya kuwatunza watu wenye usonji na kuwawezesha kujisimamia katika maisha yao ya kila siku.

Naye Mkurugenzi Msaidizi Magonjwa Yasiyoambukiza katika Wizara ya Afya, Dk. Omary Ubuguyu, amesema usonji ni ugonjwa unaoathiri mfumo wa fahamu na ukuaji na kusababisha hali ya upekee inayohusiana na utofauti katika namna mtu anavyofikiri, anavyojifunza, na jinsi anavyohusiana na wengine.

Amesema hali hiyo pia inaweza kuambatana na magonjwa mengine ya akili na mfumo wa fahamu ikiwemo kifafa au ‘hali ya kukosa utulivu’ (ADHD) na kwa baadhi ya wagonjwa kuwa na uwezo wa chini kabisa wa ufahamu.

Amesema pia wapo watu wenye tatizo la usonji ambao tatizo kubwa linabaki kwenye mawasiliano na mahusiano pekee, bila ya kuonesha dalili yeyote ya ugonjwa.

“Dalili za kwanza za usonji huonekana kabla ya mtoto kufikia umri wa miaka mitatu, na kabla ya umri huo, ni nadra kuona dalili hizi.

“Hata hivyo, kisababishi hasa cha hali hii hakijulikani bado, ingawa inadhaniwa kuwa ni matokeo ya mchanganyiko wa vinasaba na visababishi vya kimazingira,” amesema Dk. Ubuguyu.

Dk. Ubuguyu amesema mpaka sasa Serikali imesajili watoto 1,416 ambao wanapata huduma katika shule 18 maalumu zenye walimu 157.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *