Tuamini nini kama Tanesco haiaminiki?

Kuna jambo ambalo linazidi kushika kasi katika jamii yetu, hasa linapokuja suala la maandalizi ya mikutano mikubwa ya kitaifa na kimataifa. Ni jambo ambalo, kwa mtazamo wa haraka linaweza kuonekana kuwa la kawaida, lakini kwa undani linaibua maswali ya msingi kuhusu imani yetu kama taifa katika huduma tunazozitoa wenyewe.

Ni tabia ya kuzima umeme wa Tanesco (Shirika la Umeme la Taifa) na kuwasha jenereta la dharura mara tu viongozi waandamizi wanapokuwa karibu kuingia ukumbini.

Ni kweli kabisa kuwa kuhakikisha mazingira salama na yenye utulivu ni muhimu kwa mafanikio ya mikutano. Hata hivyo, kinachonitatiza ni mantiki ya kuamua kuacha kutumia umeme wa Tanesco kwa sababu ya hofu ya kukatika, hata katika maeneo ambayo huduma hiyo ni thabiti na ya kuaminika.

Kwa kufanya hivyo ni kujipa ujumbe usio wa kujiamini: kwamba hata sisi wenyewe hatuamini huduma zetu, yaani hata mahali alipo Rais umeme unaweza usiwe wa uhakika.

Tanesco ni mtoa huduma pekee wa umeme wa gridi ya taifa nchini. Serikali kwa miaka mingi imewekeza kwa kiasi kikubwa katika kuzalisha na kusambaza umeme kupitia miradi mikubwa kama vile Bwawa la Julius Nyerere (JNHPP), miradi ya upepo, jua na gesi asilia.

Ripoti ya Ewura ya Machi 2025 inaonyesha kukatika kwa umeme kulipungua kwa asilimia 48 kutoka mara 26 mwaka 2022/2023 hadi mara 14 mwaka 2023/2024. Pia muda wa kukatika umeme ulipungua kwa asilimia 64 kutoka dakika 1,536 mwaka 2022/2023 hadi dakika 554 mwaka 2023/2024.

Lakini pamoja na haya yote, bado kwenye mikutano ya hadhi ya juu tunashuhudia umeme wa Tanesco ukizimwa na jenereta kuwashwa. Kuna tangazo la haraka linatolewa: “Tunasitisha matumizi ya umeme wa Tanesco kwa muda kisha tutawasha jenereta.

Utaratibu huo unafuta dhana nzima ya jenereta kama umeme wa dhararu (standby generetor), bali imekuwa chanzo kikuu, hili halipaswi kuwa kawaida, tunapaswa kuacha tabia hiyo.

Kwa mtazamo wangu, hili si suala dogo. Lina athari za kisaikolojia kwa umma. Wananchi wanaposhuhudia kuwa hata serikali, kupitia taasisi zake au mikutano yake, haitumii huduma ya Tanesco pale inapoonekana muhimu zaidi, ni rahisi kwao kujiuliza: “Kama serikali haina imani na umeme wa Tanesco, sisi tutakuwa na sababu gani ya kuamini?”

Hii inadhoofisha dhamira ya taifa ya kujiamini, kujitegemea, na kujenga taasisi imara.

Naam, ni kweli kunaweza kuwa na hofu ya kukatika kwa umeme kunakoleta aibu mbele ya viongozi au wageni wa kitaifa na kimataifa. Lakini je, huo ndio mwelekeo sahihi? Je, hatuwezi kuona matukio hayo kama fursa ya kujifunza na kuboresha?

Tukiendelea kuepuka kukabiliana na changamoto halisi kwa kuziziba kwa njia mbadala kama jenereta, tutakosa nafasi ya kukuza huduma zetu na kuongeza uwajibikaji.

Jenereta ni kifaa cha dharura. Inapaswa kutumika pale ambapo hali imechacha au wakati umeme wa kawaida umekatika ghafla. Kukiwa na upatikanaji wa huduma ya umeme ya uhakika, tuutumie.

Tukubali kuwa ni sehemu ya safari yetu kama taifa ya kuboresha huduma za kijamii. Viongozi wanapokutana na changamoto kama wananchi wa kawaida, mara nyingine huleta matokeo chanya. Inaweza kuwapa msukumo wa kufanya maamuzi ya haraka na ya msingi katika kuboresha sekta husika.

Aidha, tunapozungumzia masuala ya mabadiliko ya tabianchi, matumizi ya jenereta kwa kiwango kikubwa kwenye matukio siyo tu kwamba ni gharama kubwa, bali pia yanaongeza uchafuzi wa mazingira kupitia uzalishaji wa hewa ukaa (carbon emissions).

Hii ni kinyume na ajenda ya kitaifa ya kutumia nishati safi na salama. Kama taifa linalojivunia kuwa kinara wa mageuzi ya kijani, tunapaswa pia kuonyesha mfano katika matumizi ya nishati endelevu.

Kwa hayo yote, ni muhimu sasa kuanza kujenga utamaduni wa kuamini huduma zetu. Kama kuna mapungufu, tuyarekebishe. Kama kuna maeneo yenye changamoto kubwa ya kukatika kwa umeme, basi tuyatambue rasmi na kutoa suluhisho la muda na la kudumu.

Nionavyo mimi, si sahihi kujenga nadharia ya kukwepa huduma yetu rasmi na kutumia mbadala kila mara tunapokutana kwenye hafla rasmi au mikutano ya viongozi.

Ni wakati wa kujiamini. Ni wakati wa kuonyesha kuwa tuna uwezo wa kutoa huduma bora kwa kutumia rasilimali zetu. Tanesco ni taasisi ya taifa. Badala ya kuiweka pembeni, tuipe nafasi ya kuonekana na kuthibitisha ubora wake. Tukifanya hivyo, tutaongeza imani kwa wananchi na kutoa ujumbe chanya kwa wadau wa maendeleo ndani na nje ya nchi.

Ephrahim Bahemu ni Mhariri wa Biashara na Uchumi wa gazeti la Mwananchi anapatikana kwa namba 0756939401

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *