TTCL yashindwa kuunganisha faiba mlangoni

Moshi. Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere amebaini Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), limeshindwa kufikia malengo ya huduma za maunganisho ya faiba mlangoni kwa wateja, baada kuunganisha kwa asilimia saba huku kampuni ya magazeti ya Serikali ikishindwa kuanzisha studio.

Katika taarifa ya Ripoti Kuu ya Mwaka ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa mwaka wa Fedha 2023/2024, CAG amebaini tofauti kubwa kati ya lengo la utendaji la Shirika la Mawasiliano na mafanikio halisi ya maunganisho ya faiba mlangoni kwa mwaka wa fedha 2023/24.

CAG amesema idadi halisi ya maunganisho hadi mwishoni mwa mwaka wa fedha 2023/24 ilikuwa nyumba 10,781, ambayo ni sawa na asilimia saba tu ya lengo lililopangwa la kuunganisha faiba katika nyumba 150,000 kwa kipindi hicho, kwa kutofikia lengo la kuunganisha nyumba 139,219 sawa na asilimia 93.

“Hali hii ilisababishwa na ukosefu wa rasilimali fedha kwa ajili ya miundombinu na vifaa vya kutosha kuhakikisha kuwa nyumba zinaunganishwa kwenye huduma ya faiba mlangoni,” amesema.

“Hii inaweza kusababisha kupotea kwa fursa za mapato, kuzuia utendaji wa kifedha wa shirika na uwezo wake wa kutoa huduma ya faiba kwa umma, na hivyo kuathiri ukuaji wa biashara na uchumi,” amesema.

CAG amependekeza shirika hilo litafute vyanzo mbadala vya ufadhili kama vile mikopo ya benki ili kuhakikisha kuwa lengo lililopangwa la maunganisho ya huduma za faiba mlangoni linatimizwa kama ilivyoainishwa katika Mpango Mkakati wa Shirika wa mwaka 2022/2023 hadi 2026/2027.

Kampuni ya Magazeti

Katika mapitio ya mpango mkakati wa utekelezaji wa mwaka 2022/2023 hadi 2026/2027, CAG alibaini kuwa Kampuni ya magazeti ya Serikali Tanzania ilikuwa imelenga kuanzisha studio kamili ya uzalishaji wa maudhui ya kidijitali ifikapo Desemba 2023.

Uzalishaji kamili wa maudhui ya kidijitali ungeisaidia kupanua mawanda yake, kukidhi ufanisi wa juu kulingana na gharama, kunyumbulika na kuwa na uwezo wa kushirikisha watazamaji.

Hata hivyo, CAG ameeleza kuwa hadi wakati wa ukaguzi Januari 2025, studio ya uzalishaji wa maudhui ya kidijitali haikuwa imeanzishwa.

“Tatizo hili lilichangiwa na ukosefu wa fedha za kutosha kwa ajili ya utekelezaji wa mradi, jambo ambalo linadhoofisha uwezo wa kampuni hiyo kushindana katika sekta ya habari za kidijitali. Pia, linapunguza wigo mpana wa maudhui ya habari”

Amependekeza Serikali kupitia Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kuipatia fedha za bajeti kampuni hiyo ili kusaidia utekelezaji wa uanzishwaji wa studio.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *