TTCL yapewa siku 30 kuboresha mawasiliano mipakani

Kyela. Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Maryprisca Mahundi ametoa siku 30 kwa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) kuboresha mifumo ya mtandao katika mpaka wa Kasumuru unaotenganisha Tanzania na nchi jirani ya Malawi.

Hatua hiyo imekuja baada uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) katika mpaka huo, kulalamikia changamoto hiyo kwamba inaathiri utendaji wao wa kazi hususani mwingiliano wa mawasiliano na nchi jirani ya Malawi.

Mahundi ametoa agizo hilo Alhamisi, Machi 20, 2025 akiwa kwenye ziara ya kikazi ya kukagua changamoto ya mwingiliano wa mawasiliano katika maeneo ya mipakani na kusaka mwarobaini wa kudhibiti haraka.

Akiwa wilayani Kyela, Mahundi amesema licha ya Serikali kuboresha huduma kwa kufunga mkongo wa taifa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwepo Wilaya ya Kyela, bado kuna shida ya mwingiliano wa mawasiliano.

“Lengo ni kuhakikisha wanadhibiti hilo kwa upande wa Tanzania ili kuwezesha wananchi kufurahia uwekezaji wa serikali kwa kupata taarifa za kinachoendelea nchini kupitia maeneo ya mipakani,” amesema.

Naibu Waziri wa Habari,Teknolojia na Mawasiliano ,Mhandisi ,Maryprisca Mahundi akionyeshwa moja ya kifaa cha mawasiliano katika eneo la Kasumuru Mpaka wa Tanzania na Nchi Jirani ya Malawi alipofanya ziara ya kikazi leo Alhamisi Machi 20, 2025. Picha na Hawa Mathias

Mahundi amesema kutokana na hali hiyo, ametoa maelekezo kwa uongozi wa TTCL Kanda kuhakikisha changamoto hiyo inaboreshwa haraka ili Watanzania wafurahie huduma bora.

“Serikali imefanya uwekezaji mkubwa, hivyo tunahitaji kasi ya utendaji iwe ya kiwango cha juu ili kuongeza ufanisi na kupunguza malalamiko ya wananchi,” amesema.

Katika hatua nyingine, Mahundi ameagiza Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kufanya tathmini katika maeneo ya vivutio vya utalii kwa lengo la kuboresha mifumo ya mawasiliano.

Sambamba na hilo, ameitaka mamlaka hiyo kusimamia watoa huduma kuhakikisha wananchi wanafurahia uwekezaji wa Serikali katika maeneo ya pembezoni na mipaka ya nchi jirani za Zambia na Malawi.

“TCRA imetekeleza wajibu wao kuhakikisha mawasiliano yanakuwa, lakini nimetoa maelekezo wawasiliane na mamlaka za wenzetu wa nchi jirani ya Malawi kufanya maboresho kwa kudhibiti mwingiliano uliopo kwa sasa kupitia minara yao,” amesema.

Amesema lengo la Serikali ni kuona wananchi wa maeneo ya mipakani wanafikiwa na huduma bora na mitandao.

Awali, Kaimu Meneja wa Kituo cha Pamoja cha Forodha cha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Nassib Kalombora ameeleza changamoto ya mtandao inavyoathiri utendaji wa kazi katika eneo la mpakani.

“Katika eneo hili la mpakani, mtandao kwa Tanzania uko chini, umezidiwa nguvu na upande wa nchi jirani ya Malawi, hali ambayo inazorotesha utendaji na kusababisha msongamano wa wateja,” amesema.

Meneja Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL), mikoa ya Mbeya na Songwe, Mhandisi Mujuni Kyaruzi amesema wataanza kuifanyia kazi changamoto hiyo sambamba na kuiwasilisha kwa uongozi wa juu.

Naibu Waziri wa Habari, Teknolojia na Mawasiliano,Mhandisi Maryprisca Mahundi akiangalia sehemu ya mitambo ya TTCL iliyofungwa Wilayani Kyela Mkoa wa Mbeya (haipo pichani) mara baada ya kutembelea ofisi hizo leo. Picha na Hawa Mathias

“Suala hili nalifanyia kazi kwa kushirikiana na TRA ingawa changamoto ni aina ya kifurushi kilichounganishwa hakilingani na mahitaji halisi,” amesema.

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera ameiomba wizara hiyo kuboresha mawasiliano katika maeneo ya Chunya ambako kuna changamoto ili wananchi wafurahie matunda ya kazi ya serikali yao.

“Naibu Waziri, nikuombe hilo ulibebe ulifikishe katika wizara yako sambamba na maeneo ya vivutio vya utalii kufikishiwa mawasiliano ili kuvutia watalii wengi na kuongeza mapato ya serikali,” amesema Homera.

Mkazi wa Kasumuru wilayani Kyela, Kelly Mwandambo amepongeza hatua ya serikali kufunga mkonga wa Taifa, hali ambayo itaongeza kasi ya kuchochea shughuli za kiuchumi kwa kufanya biashara mtandaoni.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *