Rais mteule wa Marekani, Donald Trump, amemtangaza Tom Homan, aliyekuwa mkurugenzi wa Idara ya Uhamiaji na Utekelezaji wa Forodha (ICE), kuwa msimamizi mkuu wa mpango wa kuwarejesha wahamiaji wote walioingia Marekani kinyume cha sheria.
Pia, Homan atakuwa na jukumu la kusimamia mipaka ya Marekani, ikiwa ni pamoja na ile ya kusini, kaskazini, baharini na usalama wa anga na atahakikisha wahamiaji haramu wanarejeshwa katika nchi zao za asili.
Hatua hii ni sehemu ya ahadi alizotoa Trump wakati wa kampeni yake na alisisitiza angeanzisha operesheni kuwafukuza wahamiaji wasio na vibali kutoka Marekani atakapochukua madaraka ya nchi.
Trump aliyetawala kwa muhula mmoja wa 2016-2020 alijitahidi kudhibiti uhamiaji haramu, na alikuwa na imani kwamba wahamiaji wanastahili kuchukuliwa kama tishio kwa usalama wa Taifa.
Alikuwa na mpango wa kujenga ukuta katika mpaka wa Mexico na kuanzisha mbinu nyingine za kuzuia wahamiaji kuingia Marekani.
Trump alisisitiza mara kadhaa kwamba wahamiaji haramu wanatishia usalama wa Wamarekani na aliwafananisha na wahalifu wabaya na wamwagaji damu.

Katika mkutano mmoja wa hadhara huko Raleigh, North Carolina, Trump alikiri kuwa wahamiaji haramu wanapaswa kufukuzwa haraka iwezekanavyo, akiwaita wahalifu waliokimbilia Marekani.
Kauli hizo zilijenga picha ya wahamiaji kama tishio kubwa, na iliwafanya wapigakura wa Trump kuunga mkono sera zake kali za uhamiaji.
Trump alikiri kuwa kuna wahamiaji zaidi ya milioni 20 wanaoishi Marekani kinyume cha sheria, na kwamba kundi hilo lingekuwa la kwanza kulengwa katika kampeni ya kuwarejesha makwao.
Uteuzi wa Homan
Uteuzi wa Homan ambaye aliongoza ICE kwa kipindi cha utawala wa awamu ya kwanza ya Trump, alijulikana kwa kusimamia hatua kali za kukamata wahamiaji na kuongeza idadi ya wahamiaji waliokamatwa kwa karibu asilimia 40 mwaka 2017, ukilinganisha na mwaka uliotangulia.
Homan, aliyejulikana kwa msimamo wake mkali kuhusu uhamiaji, alikiri kwamba operesheni ya kuwarejesha wahamiaji haramu nchini mwao itakuwa ngumu, lakini aliamini ni muhimu kwa usalama wa Taifa.
Aliwaambia waandishi wa habari kuwa kama sehemu ya mpango huo, familia nyingi zinaweza kutenganishwa wakati wa utekelezaji wa kuwarejesha wahamiaji, jambo ambalo liliibua maswali kuhusu haki za binadamu na madhara kwa familia za wahamiaji.
Homan alijibu kwamba familia zinapaswa kuwa tayari kufukuzwa pamoja, na kwamba operesheni hiyo haikuwa ya ubaguzi, bali ilikuwa hatua ya kulinda jamii dhidi ya wahamiaji haramu.
Alisema kuwa operesheni hiyo itaendeshwa kwa msaada wa Jeshi la Marekani ambalo litakuwa na jukumu la kuzingira na kuwafukuza wahamiaji haramu.
Homan alisisitiza kwamba hakuna atakayekosa kutekeleza hatua hizo, kwani ahadi za Trump kuhusu uhamiaji ni kipaumbele chake kikubwa katika utawala wake.
Katika mikutano mingine, Homan alizungumzia mpango wa ‘kubaki Mexico’, ambao ni sehemu ya sera ya Trump ya kudhibiti uhamiaji.
Alisema kuwa upande wa Mexico utakuwa na jukumu la kushughulikia maombi ya hifadhi kwa upande wake wa mpaka, na wahamiaji watasubiri uamuzi wa maombi yao huko.
Homan alipinga madai kwamba kambi za mateso zitatumika kukusanya wahamiaji haramu.
Alisema operesheni hiyo itakuwa tofauti na vile vyombo vya habari vinavyosema, na kwamba mipango ya kushughulikia wahamiaji haramu itakuwa ya haki na kwa usahihi.
Kwa upande mwingine, Trump alionyesha furaha kubwa kwa kumteua Homan kama msimamizi wa mipaka ya Marekani.
Aliandika kwenye mitandao ya kijamii kuwa, Homan ni mtaalamu wa kudhibiti mipaka na atakuwa na jukumu la kuhakikisha usalama wa Taifa kwa kufanikisha utekelezaji wa mpango wa kuwarejesha wahamiaji haramu.
Katika taarifa yake, Trump alisema kwa usimamizi wa Homan, Serikali ya Marekani itakuwa na uwezo wa kukabiliana na tatizo la wahamiaji haramu kwa nguvu ya kijeshi na mbinu nyingine kali.
Hii ni hatua nyingine ya Trump inayolenga kuboresha sera za uhamiaji nchini Marekani, lakini pia inakuja na maswali mengi kuhusu haki za binadamu na athari za kijamii kwa wahamiaji na familia zao.