
Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Ukraine Volodymyr Zelensky wanatarajiwa kusaini makubaliano yatakayowapa Marekani sehemu ya rasilimali adimu za madini za Ukraine.
Imechapishwa:
Dakika 1
Matangazo ya kibiashara
Rais wa Ukraine anataka kukamilisha makubaliano ya mfumo wa uchimbaji wa madini ya Ukraine na kumuuliza mwenzake wa Marekani kama ana nia ya “kusitisha” msaada kwa Ukraine.
“Kuna tarehe ya kufanya kazi (…) Ijumaa,” Bw. Zelensky ameeleza wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Kyiv. “Swali langu (kwa Bw Trump) litakuwa la moja kwa moja: je, Marekani itasitisha msaada huo au la? Je, tunaweza kununua silaha, ikiwa hakutakuwa tena na msaada?”
Kwa upande wake Rais wa Marekani Donald Trump amesema anaridhia ziara inayoweza kufanywa na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy nchini humo. Wanatarajiwa kusaini makubaliano yatakayoiruhusu Marekani kuchimba madini ya Ukraine.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi yake ya Oval wiki hii, Trump alIsema yuko tayari kukutana na Zelensky ambaye kulingana naye amesikia anakwenda Washington siku ya Ijumaa. “Ndiyo, nasikia anakuja Ijumaa, sina tatizo. Na atapenda kusaini na mimi. Na ninajua kwamba ni makubaliano makubwa. Na nadhani Wamarekani wanafurahia kwa sababu, Biden alikuwa anatapanya tu pesa kama pipi. Haya ni makubaliano makubwa. Yanaweza kufikia dola trilioni 1 na ni madini adimu sana duniani.” Alisema Trump.
Mazungumzo haya yanakuja baada ya utawala wa Trump kushangaza washirika wake wa Magharibi kwa kufanya mazungumzo ya kwanza ya ngazi ya juu na Moscow tangu Urusi ilipoivamia Ukraine zaidi ya miaka mitatu iliyopita.
Awali, Trump alionekana kumlaumu Zelensky kwa vita hivyo na kumkosoa kwa kushindwa kuanzisha mazungumzo ya amani mapema.
Hata hivyo, Alhamisi hii, baada ya kukutana na Waziri mkuu wa Uingereza, Sir Keir Starmer, Trump aliwaambia waandishi wa habari kuhusu mazungumzo yake yanayokuja na Zelensky: “Nadhani tutakuwa na mkutano mzuri sana kesho asubuhi. Tutashirikiana vizuri sana.”
Zelensky anatarajia kupata aina fulani ya dhamana ya usalama kwa ajili ya Ukraine ambayo itasaidia katika makubaliano yoyote ya amani yanayoweza kufikiwa.