
Rais wa Marekani Donald Trump atazungumza kwa simu na Vladimir Putin siku ya Jumatatu kama sehemu ya juhudi zake za muda mrefu za kumaliza vita vilivyosababishwa na uvamizi wa Moscow nchini Ukraine mnamo mwaka 2022.
Imechapishwa:
Dakika 3 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Wakati wa kampeni za uchaguzi wa Marekani, Trump aliahidi kumaliza mzozo huo ndani ya saa 24 baada ya kuchukua madaraka, lakini juhudi zake za kidiplomasia hadi sasa hazijapiga hatua.
Wajumbe wa Urusi na Ukraine walifanya mazungumzo ya moja kwa moja mjini Istanbul wiki iliyopita kwa mara ya kwanza katika takriban miaka mitatu, lakini mazungumzo hayo yalimalizika bila ahadi zozote za kusitisha mapigano.
Pande hizo mbili zilirushiana matusi, huku Ukraine ikiishutumu Moscow kwa kutuma ujumbe “wa uwongo” wa maafisa wa chini.
Kufuatia mazungumzo hayo, Trump ametangaza kuwa atazungumza kwa njia ya simu na rais wa Urusi ili kujaribu kumaliza “umwagaji damu” nchini Ukraine, ambao umeharibu maeneo makubwa ya nchi hiyo na kusababisha mamilioni ya watu kuyahama makazi yao.
Trump pia amesema kuwa atakutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na maafisa wa NATO, akielezea matumaini kwamba “usitisha mapigano utaanzishwa na vita hivi vikali sana … vitakwisha.”
Tangu aingie madarakani mwezi Januari mwaka huu, Trump amesisitiza ahadi yake ya kumaliza mzozo huo na hivi karibuni aliunga mkono wito wa kusitisha mapigano bila masharti kwa siku 30.
Kufikia sasa, amejikita zaidi katika kuongeza shinikizo kwa Ukraine na kujiepusha na kumkosoa Putin.
Moscow na Washington tayari zimesisitiza haja ya kufanyika kwa mkutano kuhusu mzozo kati ya Putin na Trump.
Rais wa Marekani pia alisema “hakuna kitakachofanyika” kwenye mzozo huo hadi atakapokutana na Putin ana kwa ana.
Kuongeza vikwazo dhidi ya Urusi
Katika mazungumzo ya Istanbul, ambayo pia yalihudhuriwa na maafisa wa Marekani, Urusi na Ukraine zilikubaliana kubadilishana wafungwa 1,000 kila mmoja na kubadilishana mawazo juu ya uwezekano wa kusitisha mapigano, lakini bila ya ahadi zozote madhubuti.
Kiongozi mkuu wa ujumbe wa Ukraine, Waziri wa Ulinzi Rustem Umerov, alisema hatua inayofuata itakuwa mkutano kati ya Putin na Zelensky.
Urusi ilisema imezingatia ombi hilo.
“Tunazingatia hili linawezekana, lakini tu kupitia kazi na kufikia baadhi ya matokeo kwa njia ya makubaliano kati ya pande hizo mbili,” msemaji wa Kremlin alisema.
Washirika wa Magharibi wa Ukraine wamemtuhumu Putin kwa kupuuza kwa makusudi wito wa kusitishwa kwa mapigano na kutaka kuwekewa vikwazo vipya dhidi ya Urusi.
Viongozi wa Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Italia walizungumza kwa njia ya simu na Trump siku ya Jumapili.
“Kabla ya mazungumzo ya simu kati ya rais Trump na rais Putin kesho, viongozi hao walijadili haja ya kusitishwa kwa mapigano bila masharti na haja ya rais Putin kuchukua mazungumzo ya amani kwa uzito,” msemaji wa Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer amesema.
“Pia walijadili matumizi ya vikwazo ikiwa Urusi haikushiriki kwa dhati katika mazungumzo ya kusitisha mapigano na amani,” msemaji huyo aliongeza.
Zelensky pia alijadili vikwazo vinavyowezekana na Makamu wa Rais wa Marekani J.D. Vance wakati wa mkutano wao huko Vatican siku ya Jumapili baada ya Misa ya kuapishwa kwa Papa Leo XIII.
“Tulijadili mazungumzo ya Istanbul, ambapo Urusi ilituma wajumbe wa ngazi ya chini, bila mamlaka ya kufanya maamuzi,” Zelensky aliandika kwenye Telegram baada ya mkutano huo.
“Tulijadili pia hitaji la vikwazo dhidi ya Urusi, biashara ya nchi mbili, ushirikiano wa kiulinzi, hali katika uwanja wa vita na zoezi lijalo la kubadilishana wafungwa.”
Afisa mkuu wa rais wa Ukraine, ambaye hakutaka jina lake litajwe, aliiambia AFP pia walijadili maandalizi ya mazungumzo ya simu ya siku ya Jumatatu kati ya Trump na Putin.