Trump atangaza kiama Hamas isipowaachia mateka wote wa Israel

Washington. Rais wa Marekani, Donald Trump ametangaza kile alichokiita onyo la mwisho kwa wapiganaji wa kundi la Hamas akiwataka kuwaachia mateka wote walioko eneo la Gaza, huku akitangaza kiama endapo hawatofanya hivyo.

CNN imeripoti leo Alhamisi Machi 6, 2025, kuwa Trump ametangaza uamuzi huo baada ya Marekani kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na kundi la Hamas.

“Waachilieni mateka wote sasa hivi na siyo baadaye na mrejeshe mara moja miili ya watu mliowaua la sivyo “mtakuwa mmekwisha.” Trump aliandika kwenye akaunti yake ya Truth Social, muda mfupi baada ya kukutana na mateka wanane waliokuwa wameachiwa kutoka Gaza.

Trump aliandika kuwa ataitumia Israel kila kitu inachohitaji kukamilisha kazi na akaonya kuwa: “Hakuna hata mshirika mmoja wa Hamas atakayekuwa salama msipofanya ninavyosema.”

Matamshi hayo yalitolewa saa chache tu baada ya Marekani kuthibitisha ripoti kwamba ilikuwa inafanya mazungumzo ya moja kwa moja na Hamas kuhusu mateka na usitishaji mapigano Gaza, hatua ambayo ni kinyume na sera yake ya kawaida ya kutofanya mazungumzo na makundi inayoyachukulia kuwa ya kigaidi.

Tovuti ya Axios ilikuwa ya kwanza kuripoti kuhusu mazungumzo hayo kati ya Marekani na kundi la Hamas.

Marekani ambayo iliitangaza Hamas kama kundi la kigaidi mwaka 1997, kwa kawaida haizungumzi na mashirika ya kigaidi, ingawa kumeonekana kutoeleweka mwa utekelezaji wa sera hiyo, hususan kwenye utawala wa Rais Barack Obama na Trump ambapo viongozi hao waliwahi kufanya mazungumzo na kundi la Taliban, ambalo lilitangazwa kuwa kundi la kigaidi baada ya shambulio la 9/11.

Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Karoline Leavitt alipolizwa Jumatano kwa nini Marekani inafanya mazungumzo moja kwa moja na kwa mara ya kwanza kabisa na Hamas alijibu: “Kuhusu mazungumzo unayoyataja, kwanza kabisa, mjumbe maalumu anayehusika na mazungumzo hayo ana mamlaka ya kuzungumza na mtu yeyote,” alisema Leavitt.

Leavitt alisema hivyo akimrejelea, Adam Boehler, ambaye aliteuliwa na Trump kama mjumbe wa taifa hilo kwenye maridhiano ya kuachiliwa kwa mateka hao.

“Israeli ilishauriwa kuhusu suala hili na imekuwa ikifanya mazungumzo na watu kote ulimwenguni kwa ajili ya kufanya kile kilicho katika masilahi ya raia wa Marekani.

“Rais ameonyesha kuamini ni jitihada zenye nia njema kufanya kile kilicho sahihi kwa watu wa Marekani,” Leavitt aliongeza.

CNN imewasiliana na Baraza la Usalama wa Taifa la Marekani kwa maoni, hata hivyo bado haijajibiwa kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, Ofisi ya Waziri Mkuu wa Israeli, ilisema ilikuwa imeipatia Marekani msimamo wake kuhusu mazungumzo ya moja kwa moja na Hamas bila kuainisha msimamo huo ni wa aina gani.

Taarifa ya Israeli haikufafanua ikiwa Israeli ilikuwa na taarifa mapema kuhusu mazungumzo hayo ama ilipata taarifa baada ya kuwa suala hilo limefanyika. Pia, haikufichua wazi msimamo wa Israeli.

Mapema Jumatano, chanzo cha habari ambacho hakikutaka kutajwa jina lake kiliiambia CNN kuwa Israel ilikuwa na ufahamu wa mazungumzo hayo.

Jitihada za CNN kufahamu maazimio ya mazungumzo hayo kutoka kundi la Hamas zimegonga mwamba baada ya kundi hilo kutotoa jibu kuhusu suala hilo.

Hata hivyo, Mwanadiplomasia Mwandamizi wa Israeli alionekana kurejelea mazungumzo kati ya pande hizo katika moja ya mahojiano na Kituo cha Televisheni cha Fox Business.

“Badala ya kuiweka Israeli chini ya shinikizo, Rais (Donald) Trump anaiwekea Hamas shinikizo na hili ndilo jambo sahihi kufanya,” alisema Ofir Akunis, Balozi wa Israeli nchini Marekani.

“Ikiwa Ikulu ya Marekani inataka kuzungumza moja kwa moja na Hamas na kuwawekea shinikizo kuwaachia mateka zaidi, tutaona furaha kubwa kuona mateka zaidi wakirudi kwa familia zao na nchini Israeli,” aliongeza.

Hamas: Kauli ya Trump inahujumu maridhiano

Katika matamshi yake kwenye mtandao wa Truth Social, Trump aliwaeleza watu wa Gaza akisema kuwa wanaelekea kukutana na mustakabali mzuri mbele yao, hata hivyo suala hilo litageuka mara tu watakapokwama kuwaachia mateka wote wanaowashikilia.

“Ikiwa hamtawaachia basi mmekufa wote fanyeni uamuzi wenye busara. Waachilieni mateka sasa, la sivyo mtakutana na kiama baadaye’ Trump aliandika.

Trump hapo awali alisema anaiona Gaza kama eneo kubwa la ardhi lenye fursa ya maendeleo, akitaja kuwa inaweza kuwa “Riviera ya Mashariki ya Kati.”

Hamas ilionya kuwa matamshi ya Trump Jumatano yalihatarisha kuhujumu usitishaji mapigano na makubaliano ya kuachiliwa mateka wa Israel wanaoshikiliwa Gaza.

Msemaji wa Hamas, Hazem Qassem, aliambia CNN kuwa matamshi hayo yatatatiza mambo kuhusu makubaliano ya usitishaji mapigano na kuipa serikali ya Israeli ujasiri wa kukengeuka katika utekelezaji wa makubaliano hayo.

Qassem alisema Hamas tayari imetekeleza masharti ya awamu ya kwanza chini ya makubaliano yaliyopatanishwa na Marekani, huku akidai kuwa serikali ya Israeli inakwepa mazungumzo ya awamu ya pili.

Alitaka Marekani kuiwekea Israeli shinikizo ili iingie kwenye awamu ya pili ya mazungumzo kama ilivyoainishwa kwenye makubaliano ya awali.

Jumapili, siku moja baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza, Israeli ilizuia misaada ya kibinadamu kuingia Gaza, baada ya Hamas kukataa pendekezo jipya la Israeli la kuongeza usitishaji mapigano bila ahadi yoyote ya kumaliza vita au kuondoa vikosi vyake kikamilifu.

Kwa mujibu wa Wizara ya Afya ya Gaza, mapigano kati ya Jeshi la Israeli (IDF) yaliyoanza Oktoba 7, 2023, yamesababisha vifo vya Wapalestina 61,709 eneo la Gaza huku 111,845 wakijeruhiwa.

Pia, Israel inasema uvamizi wa wapiganaji wa Hamas ulisababisha vifo vya watu takriban 1,139 huku 251 wakichukuliwa mateka na kupelekwa eneo la Gaza.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.