
Washington. Wakati soko la Kimataifa la bidhaa za Marekani likiripotiwa kudorora kwa kasi huku raia wakilia uchumi kuporomoka, Rais wa Marekani, Donald Trump amesitisha ghafla ushuru aliowekea mataifa mengi duniani kwa kipindi cha siku 90.
Pamoja na kusitisha ushuru huo kwa mataifa mengine, Trump ameongeza maumivu kwa taifa la China kwa kuongeza ushuru kutoka asilimia 85 hadi asilimia 125.
Hatua hiyo ilionekana kama jaribio la kupunguza kile kinachoitwa vita vya kibiashara visivyo na mfano kati ya Marekani na mataifa mengi duniani, huku vikionekana kutawaliwa na Marekani na China.
Kwa mujibu wa ripoti ya masoko nchini humo, kielelezo cha hisa cha S&P 500 kilipanda kwa asilimia 9.5 baada ya tangazo la Trump la kusitisha ushuru. Lakini mvutano kuhusu ushuru wa Trump bado haujaisha huku Serikali ikijiandaa kwa mazungumzo ya nchi kwa nchi.
Kwa sasa, mataifa yaliyopata msamaha huo yatalipishwa ushuru wa asilimia 10.
Rais alichukua hatua hiyo kutokana na shinikizo kubwa kutoka kwenye masoko ya fedha yaliyokuwa yakiyumba, hali iliyomsukuma kufikiria upya kuhusu ushuru huo, ingawa baadhi ya maofisa wa Serikali walisisitiza kuwa mabadiliko hayo ni sehemu ya mpango wa tangu awali.
Wakati hisa na dhamana zikishuka thamani nchini humo, wapigakura walikuwa wakishuhudia akiba zao za uzeeni zikipungua na wafanyabiashara wakionya kuhusu kushuka kwa mauzo kuliko ilivyotarajiwa na kupanda kwa bei.
Mataifa mengi yanayoonekana kuiwekea ngumu Marekani dhidi ya ushuru huo wa Trump ulioanza kutekelezwa Jumatano, Aprili 2,2025, jambo lililodhihirisha kuwa Rais wa Marekani hakutafakari vyema juu ya uamuzi wake.
Kufikia jana mchana, Trump alichapisha kwenye mtandao wake wa Truth Social kuwa kwa sababu zaidi ya nchi 75 zilikuwa zimewasiliana na Serikali ya Marekani kwa nia ya mazungumzo ya kibiashara na hazikujibu kwa njia za kisasi.
“Nimeruhusu msamaha wa siku 90, na ushuru wa asilimia 10 katika kipindi hiki, unaoanza mara moja,” amesema Trump.
Trump baadaye aliwaambia waandishi wa habari kuwa aliondoa ushuru kwa mataifa mengi lakini siyo China kwa sababu raia wa Marekani walionyesha wanapaniki na kuogopa kutokana na kushuka kwa soko la hisa.
Rais Trump alisema alikuwa akifuatilia soko la dhamana na watu walikuwa wameanza kuchoshwa na mwenendo wa kushuka kwa bei ya dhamana huku kukiwa na kupanda kwa viwango vya riba, jambo ambalo limeonekana kushusha uaminifu wake miongoni mwa Wamarekani.
“Soko la dhamana ni gumu sana,” Trump alisema. “Nilikuwa nikiangalia. Lakini sasa, ukiangalia, ni zuri.”
Rais huyo baadaye alisema alikuwa akiwaza kuhusu kusitisha ushuru kwa siku chache zilizopita, lakini amelifanikisha hilo mapema asubuhi ya leo.
Alipoulizwa kwa nini wasaidizi wake wa Ikulu walikuwa wakisisitiza kwa wiki kadhaa kuwa ushuru haukuwa sehemu ya majadiliano, Trump alisema: “Mara nyingi, si majadiliano hadi yanapokuwa hivyo.”
Ushuru wa asilimia 10 ndio kiwango cha msingi kilichoanza kutekelezwa Jumamosi kwa mataifa mengi. Ni cha chini sana kuliko ushuru wa asilimia 20 aliokuwa ameweka kwa bidhaa kutoka Umoja wa Ulaya, asilimia 24 kwa bidhaa kutoka Japan na asilimia 25 kwa bidhaa kutoka Korea Kusini.
Hata hivyo, asilimia 10 ni ongezeko ikilinganishwa na ushuru wa awali uliokuwa ukitozwa na Serikali ya Marekani. Canada na Mexico wataendelea kulipishwa hadi asilimia 25 kutokana na agizo tofauti la Trump la kudhibiti usafirishaji wa dawa za kupunguza maumivu za Fentanyl.
Waziri wa Hazina wa Marekani, Scott Bessent, alisema kuwa mazungumzo na nchi moja moja yatakuwa ya kipekee, ikimaanisha kuwa siku 90 zijazo zitahusisha mazungumzo ya makubaliano mengi.
Bessent, ambaye ni meneja wa zamani wa mfuko wa uwekezaji, aliwaambia waandishi kuwa kusitisha ushuru hakukutokana na kuyumba kwa masoko ya fedha, bali ni kwa sababu mataifa mengine yaliomba mazungumzo kauli ambayo baadaye ilipingwa na rais mwenyewe.
“Hakikisho pekee tunaloweza kutoa ni kwamba Marekani itajadiliana kwa nia njema, na tunadhani washirika wetu nao pia watafanya hivyo,” alisema Bessent.
Waziri wa Biashara, Howard Lutnick, baadaye alikanusha maelezo ya rais kwa kusema siyo masoko yaliyochangia Trump kusitisha ushuru, bali ni maombi ya mazungumzo kutoka nchi nyingine.
Kabla ya mabadiliko hayo, wakuu wa biashara walikuwa wakionya kuhusu uwezekano wa mdororo wa uchumi unaosababishwa na sera zake, baadhi ya washirika wakuu wa kibiashara wa Marekani walikuwa wakisema ushuru huo unayumbisha soko la hisa.
Msemaji wa Ikulu, Karoline Leavitt, alisema kuwa hatua hiyo ilikuwa sehemu ya mkakati wa mazungumzo wa Trump.
Alisema vyombo vya habari “vilishindwa kabisa kuelewa anachofanya Rais Trump.
“Mlidai kuwa dunia nzima ingemkimbilia China, lakini tumeona kinyume chake. Dunia nzima inaiita Marekani, si China, kwa sababu wanahitaji masoko yetu.”
Mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), Ngozi Okonjo-Iweala, alisema vita vya kibiashara kati ya Marekani na China vinaweza kuharibu pakubwa mtazamo wa uchumi wa dunia, na akaonya kuhusu uwezekano wa kugawanyika kwa biashara ya dunia kwa misingi ya kisiasa.
Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika ya habari.