Trump asitisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine

Washington. Rais wa Marekani, Donald Trump, ameagiza kusitishwa kwa msaada wote wa kijeshi kwa Ukraine siku chache baada ya mvutano mkali kati yake na Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, katika Ikulu ya White House.

Hatua hiyo imekuja baada ya mkutano wa faragha kati ya viongozi hao wawili, ambapo Trump anadaiwa kumpa Zelensky sharti la kukubali mazungumzo ya amani na Russia ikiwa anataka msaada wa Marekani kuendelea.

Mkutano wa wawili hao uligeuka kuwa na mvutano mkali, ambapo Trump alimwambia Zelensky arejee tu kama yuko tayari kutafuta suluhu ya kidiplomasia badala ya kutegemea msaada wa silaha.

Makamu wa Rais wa Marekani, JD Vance, ameunga mkono uamuzi wa Trump, akimtuhumu Zelensky kwa kusitasita kuingia kwenye mchakato wa amani.

Hata hivyo, Vance amesema anaamini kiongozi huyo wa Ukraine hatimaye ataelekeza juhudi zake katika suluhisho la kidiplomasia.

Uamuzi huu wa kusitisha msaada wa kijeshi unahusisha silaha na vifaa vya thamani ya zaidi ya Dola bilioni 1 (Sh2.624 trilioni), jambo linaloweza kuwa na athari kubwa kwa Ukraine, ambayo imekuwa ikitegemea msaada wa Marekani katika vita dhidi ya Russia.

Wachambuzi wa masuala ya kimataifa wanasema hatua hiyo ya Trump huenda ikaathiri zaidi uhusiano kati ya Marekani na Ukraine, huku viongozi wa Ulaya wakiharakisha juhudi za kutafuta makubaliano ya amani ili kuziba pengo litakalosababishwa na kusitishwa kwa msaada huo.

Hali inaendelea kuwa ya sintofahamu, huku wadau wa kimataifa wakifuatilia kwa karibu iwapo Ukraine itaweza kuendelea kupambana na Russia bila msaada wa moja kwa moja wa Marekani.

Chanzo cha mvutano White House

Mvutano kati ya Rais Trump, na Zelensky, ulizuka Ikulu ya White House baada ya Zelensky kumwomba Trump msaada zaidi wa kijeshi ili kuendelea kupambana na uvamizi wa Russia. 

Hata hivyo, Trump alikataa ombi hilo na kumtaka Zelensky kwanza akubali kuingia katika mazungumzo ya amani na Russia.

Mkutano huo uligeuka kuwa wa mvutano mkali baada ya Trump kumwambia Zelensky kwamba Marekani haitatoa msaada wowote wa kijeshi hadi Ukraine ionyeshe nia ya kweli ya kutafuta suluhu ya kidiplomasia badala ya kutegemea msaada wa silaha. 

Imeandikwa na Evagrey Vitalis kwa msaada wa mashirika ya habari.