Trump ashambulia maficho ya ISIS Somalia

Washington. Rais Donald Trump wa Marekani amesema aliagiza mashambulizi ya anga ya kijeshi dhidi ya mpangaji mkuu wa mashambulizi na wanachama wengine wa kundi la kigaidi la ISIS nchini Somalia.

“Wauaji hawa, ambao tuliwakuta wakijificha kwenye mapango, walikuwa tishio kwa Marekani na washirika wetu,” Trump aliandika kwenye mitandao ya kijamii.

“Mashambulizi hayo yaliharibu mapango waliyoishi na kuwaua magaidi wengi bila kuwaathiri raia,” Shambulio lilifanyika jana asubuhi Februari Mosi, 2025.

Katika chapisho kwenye X, ofisi ya Rais wa Somalia imearifu kuhusu shambulio la Marekani lililolenga uongozi wa juu wa ISIS kaskazini mwa nchi hiyo.

Hata hivyo, Trump kwenye chapisho lake kwenye X hakutaja majina ya watu waliolengwa katika mashambulizi hayo.

Trump amehitimisha ujumbe wake kwa kusema: “Ujumbe kwa ISIS na wote wanaotaka kuwashambulia Wamarekani ni kwamba ‘tutakupata na tutakuua’.

Katika chapisho jingine kwenye X, ofisi ya Rais wa Somalia, Hassan Sheikh Mohamud, ilisema inatambua, “msaada thabiti wa Marekani katika mapambano dhidi ya ugaidi wa kimataifa na inakaribisha ahadi inayoendelea chini ya uongozi madhubuti wa Rais Donald Trump.”

Chapisho hilo pia lilisema operesheni hiyo ya hivi karibuni: “Inaimarisha ushirikiano wa kiusalama kati ya Somalia na Marekani katika kupambana na vitisho vya itikadi kali.”

Katika taarifa yake, Waziri wa Ulinzi wa Marekani, Pete Hegseth amesema: “Tathmini yetu ya awali inaonyesha kuwa waendeshaji wengi wa ISIS wameuawa katika mashambulizi haya ya anga na hakuna raia aliyeathirika.”

Hegseth amesema mashambulizi hayo yamepunguza zaidi uwezo wa ISIS kupanga na kutekeleza mashambulizi ya kigaidi na yanatuma ujumbe wazi kuwa Marekani iko tayari wakati wote kuwatafuta na kuwaangamiza magaidi.

Amesema mashambulizi hayo yalitekelezwa katika milima ya Golis, kaskazini mashariki mwa Somalia. 

Serikali ya Puntland, eneo la kaskazini mashariki mwa Somalia, ilishukuru marafiki wa kimataifa waliotoa msaada katika mashambulizi hayo ambayo yaliwaua viongozi waandamizi wa ISIS.

Historia ya ISIS Nchini Somalia

Kundi la ISIS lilipata umaarufu wa kimataifa katika miaka ya 2010, hasa nchini Syria na Iraq, lakini kwa sasa uwepo wake umebaki katika baadhi ya sehemu za Afrika.

Tawi la ISIS nchini Somalia liliundwa mwaka 2015 na kundi la waasi waliojiengua kutoka al-Shabab, kundi lenye mafungamano na Al-Qaida ambalo ndilo kubwa zaidi la itikadi kali nchini Somalia. 

Kwa mujibu wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Ujasusi wa Taifa wa Marekani, ISIS nchini Somalia inajulikana kwa kuwatoza kodi kwa nguvu wananchi wa kawaida na mara nyingi hutekeleza mashambulizi madogo na yasiyokuwa ya mara kwa mara.

Mgawanyiko wa sera za Marekani 

Katika taarifa yake Jumamosi, Trump pia alimshambulia mtangulizi wake (Joe Biden), akidai kuwa jeshi la Marekani limekuwa likimlenga mpangaji huyo wa mashambulizi wa ISIS kwa miaka mingi, lakini akamlaumu Biden na washirika wake kwa kutoshughulikia suala hilo kwa haraka vya kutosha.

Hata hivyo, mnamo 2023, majeshi ya Marekani yaliwaua kiongozi wa ISIS, Bilal al-Sudani na wanachama wake 10 katika pango lililoko milimani kaskazini mwa Somalia, katika operesheni iliyoagizwa na Biden.

Moja ya hatua za mwisho Trump alizochukua kabla ya kuondoka Ikulu mwaka 2020 ilikuwa ni kuwaondoa mamia ya wanajeshi wa Marekani nchini Somalia.

Trump chini ya wiki mbili baada ya kurejea madarakani, ameagiza mashambulizi ya kwanza dhidi ya taifa hilo.

Trump amekuwa akisisitiza kuwa hataki Marekani kushiriki katika migogoro ya mataifa mengine, wakati Biden alitaka kumaliza ushiriki wa Marekani katika vita vilivyoanza baada ya mashambulizi ya Septemba 11, 2001. 

Hata hivyo, Marekani ina mtazamo tofauti kuhusu Somalia. Marekani imewekeza kwa kiasi kikubwa nchini humo kwa miongo kadhaa, ikilenga kudhibiti tishio linalotokana na al-Shabab.

Katika muhula wake wa kwanza, Trump aliamuru mashambulizi dhidi ya magaidi licha ya kuwaondoa wanajeshi wake katika hatua za mwisho za urais wake.

Biden aliporejea madarakani mwaka 2021, alibadili uamuzi huo ili kuhakikisha Marekani inaendelea kuwa na uwepo wa kijeshi nchini Somalia.

Hadi sasa katika muhula wake wa pili, Trump ameendelea kuweka wanajeshi nchini humo.

Hata hivyo, kuna uwezekano kuwa anaweza kuchukua mwelekeo tofauti baadaye, si tu kuhusu Somalia bali bara la Afrika kwa ujumla.

Waziri wake wa zamani wa ulinzi, Mark Esper, aliandika katika kitabu chake cha kumbukumbu kwamba Trump hakuona thamani kubwa ya kuwepo kwa Wamarekani iwe wanajeshi au wanadiplomasia barani Afrika.

Hili linaweza kuwa kweli zaidi kwa Somalia, ambako al-Shabab inaonekana kuendelea kuwa na nguvu, na Marekani inaweza kuamua kuwa haina umuhimu kuendelea kuwekeza rasilimali zake huko.

Katika muhula wake wa kwanza, Trump hakutilia mkazo mahusiano ya Marekani na Afrika alialika viongozi wawili tu kutoka Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara na hakuwahi kutembelea bara hilo.

Katika muhula wake wa pili, Trump anaweza kuangalia Afrika kwa mtazamo wa ushindani zaidi, hasa kutokana na kuongezeka kwa ushawishi wa Urusi na China katika biashara na uwekezaji barani humo.