Hata hivyo, Umoja wa Ulaya umetangaza hatua chanya katika mazungumzo yake na Marekani, licha ya Trump kuongeza ushuru wa vyuma na aluminium.
Hatua mpya za kibiashara zilizochukuliwa na Donald Trump zimekuja wakati mawaziri kutoka nchi wanachama wa Shirika la Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (OECD) wakikutana mjini Paris kujadili mustakabali wa uchumi wa dunia, kufuatia msimamo mkali wa Marekani ambao umetikisa masoko ya kimataifa.
Trump ameweka ushuru wa hadi asilimia 145 kwa bidhaa kutoka China, hali iliyosababisha China kujibu kwa ushuru wa asilimia 125 kwa bidhaa za Marekani. Ingawa pande hizo mbili zilifikia makubaliano ya muda mwezi uliopita ili kupunguza mvutano, matumaini ya kufikia makubaliano ya kudumu yanaendelea kuyumba.
Mazungumzo ya EU na Marekani
Wakati mvutano kati ya Marekani na China ukiendelea, Umoja wa Ulaya umeeleza kuwa mazungumzo yake na Washington yanaendelea vizuri, licha ya Trump kuongeza ushuru wa vyuma kutoka asilimia 25 hadi 50.
Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Katherina Reiche, ameonya kuwa suluhisho la haraka linahitajika kabla ya utekelezaji wa ushuru huo mpya kuanza mwezi ujao.
Kamishna wa Biashara wa Umoja wa Ulaya, Maros Sefcovic, baada ya mazungumzo na Mwakilishi wa Biashara wa Marekani, Jamieson Greer, kando ya mkutano wa OECD mjini Paris. alisema:
“Kwa sasa, mazungumzo yetu yanahusu masuala yote; ni ya kina sana. Tunazungumzia usalama wa kiuchumi, tunapitia viwango vya ushuru, tunajadili upatikanaji wa masoko, na pia tunatafakari nini tunaweza kufanya siku za usoni kuhakikisha kwamba uhusiano wetu wa kibiashara ambao, ndiyo mkubwa zaidi duniani – utakuwa wa usawa na haki kwa pande zote mbili.” Alisema Sefcovic.
Sefcovic aliongeza kuwa, licha ya changamoto, pande hizo “zinaendelea kupiga hatua” kuelekea makubaliano.
Bidhaa kutoka mataifa 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya zitakabiliwa na ushuru wa asilimia 50 kuanzia Julai 9, iwapo hakutakuwa na makubaliano na Washington. Umoja wa Ulaya umesisitiza kuwa utajibu kwa hatua madhubuti.
Kwa upande mwingine, Mexico imetangaza kuwa itaomba kusamehewa ushuru huo mpya. Waziri wa Uchumi wa nchi hiyo, Marcelo Ebrard, amesema hatua hiyo si ya haki kwa kuwa Marekani inauza vyuma zaidi kwa Mexico kuliko inavyonunua kutoka humo.
Wakati hayo yakiendelea, Kundi la Nchi Saba zenye uchumi mkubwa duniani (G7) linatarajiwa kujadili suala hilo katika mkutano wake wa biashara, huku muda ukizidi kuyoyoma kuelekea tarehe ya mwisho ya utekelezaji wa ushuru mpya.