Trump apeleka wanajeshi zaidi Los Angeles

Hii inajiri baada ya serikali ya Rais Donald Trump kuamuru kupelekwa kwa karibu wanajeshi 700 wa kitengo maalum kusaidia kupambana na machafuko yanayoendelea mjini humo.

Wizara ya ulinzi Pentagon imeridhia kupelekwa wanajeshi hao Los Angeles kuvisaidia vikosi vya Ulinzi wa Taifakukabiliana na maandamano ya wahamiaji. Wanajeshi hao wamefunga safari kutoka kituo chao cha Twentynine Palms katika jangwa la California.

Gavana wa California Gavin Newsom, Mdemokrat, ameiita hatua hiyo kuwa ni uzembe na “isiyoheshimu wanajeshi wa Marekani”. Alisema hatua hiyo haikuhusu usalama wa umma bali ilihusu kuiridhisha kiburi cha Rais”

Mkuu wa Polisi wa Los Angeles Jim McDonnell anasema ana imani na uwezo wa idara ya polisi kushughulikia maandamano makubwa na kwamba kuwasili kwa wanajeshi maalum bila kuratibu na idara ya polisi kunaweka “changamoto kubwa ya nyenzo na uendeshaji” kwao.

Maandamano ya kupinza misako dhidi ya wahamiaji California
Waandamanaji wanaopinga kukamatwa kwa wahamiaji wamekusanyika Los Angeles kwa siku ya nne mfululizoPicha: David Ryder/REUTERS

Rais Trump aliamuru Jumapili askari wa Ulinzi wa Taifa kupelekwa katika maandamano ya Los Angeles, hatua ambayo Mwanasheria Mkuu wa jimbo la California Rob Bonta aliita “kinyume cha sheria” na akasema “iliuhujumu uhuru” wa jimbo hilo.

Katika kujibu hatua hiyo, Bonta aliushitaki mahakamani utawala wa Trump.

Gavana Newsom, aliiambia televisheni ya MSNBC kwamba anapanga pia kuwasilisha kesi Jumatatu dhidi ya utawala wa Trump kuubatilisha uamuzi wa kutumiwa vikosi vya Ulinzi wa Taifa, ambao aliuita “kitendo haramu, kitendo kisicho cha maadili, na kitendo kisicho cha kisheria.”

Hii inaonekana kuwa mara ya kwanza katika miongo kadhaa kwa Jeshi la Ulinzi wa Taifa kutumika jimboni bila ombi kutoka kwa gavana wake.

Trump ametaja kipengele cha kisheria kinachomruhusu kuvitumia vikosi vya shirikisho wakati kukiwa na “uasi au hatari ya uasi dhidi ya mamlaka ya Serikali ya Marekani.”

Gavana wa California Gavin Newsom
Gavana wa California Gavin Newsom, ameitaja hatua ya kutumiwa wanajeshi Los Angeles kuwa inayojumu uhuru wa jimboPicha: Steven Senne/AP/dpa/picture alliance

Kiasi ya askari 1,000 wa Ulinzi wa Taifa waliwasili mjini humo kufikia Jumatatu, na Trump alisema aliagiza askari 2,000 kutumika ikiwa patakuwa na haja.

Kuwasili kwa vikosi hivyo kulifuatia siku mbili za maandamanao ambayo yalianza Ijumaa mitaani Los Angeles baada ya maafisa wa shirikisho wa uhamiaji kuwakamata Zaidi ya watu 40 kote mjini humo.

Umoja wa Mataifa umepaza sauti kuhusu namna polisi wanavyowakabili waandamanaji California. Kupitia msemaji wake Farhan Haq, umetoa wito kwa ngazi zote za serikali, ikiwa ni pamoja na mamlaka za majimbo na shirikisho, kuzuia kile ulichoita “matumizi zaidi ya wanajeshi” kwenye machafuko hayo.

AP

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *