
Mkutano wa G20 wa Afrika Kusini ulitarajiwa kuwa fursa kwa mataifa tajiri, yenye nguvu kutilia maanani masuala ya nchi maskini zaidi kama vile kuongezeka kwa ukosefu wa usawa na kukosekana kwa maendeleo katika vita dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
Lakini nchi tajiri, yenye nguvu zaidi, Marekani, haitashiriki mkutano huo. Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio alisema Februari 6, 2025 kwamba malengo ya G20 ya Afrika Kusini yalikuwa “mbaya sana” na hatahudhuria mikutano ya wiki ijayo na wenzake wa G20 huko Johannesburg.
Katika shambulizi kubwa zaidi dhidi ya Afrika Kusini, Rais Donald Trump alikata msaada wa kifedha wa Marekani kwa nchi hiyo, akitaja kutokubaliana na sera yake ya ugawaji wa ardhi na kesi yake ya mauaji ya kimbari dhidi ya Israel katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki.
“Msimamo wa Marekani unaonekana kulenga kuhakikisha kuwa Afrika Kusini haifanikiwi kuandaa mkutano wa G20,” alisema Ongama Mtimka, kaimu mkurugenzi wa Kituo cha Utawala na Uongozi cha Raymond Mhlaba katika Chuo Kikuu cha Nelson Mandela nchini humo.
G20 ilizinduliwa baada ya mdororo wa kifedha wa mwaka 2007/08 ikijumuisha mataifa makubwa yanayoibukia kiuchumi katika mazungumzo ambayo hapo awali yaliwekwa kwenye Kundi la Mataifa Saba Yaliyoendelea Kiviwanda, inapaswa kuwa uwanja muhimu wa ushirikiano wa kiuchumi na kifedha.
Pia, inaonekana kuwa muhimu katika kuchagiza mwitikio wa mabadiliko ya hali ya hewa, kwani mataifa ya G20 yanachukua asilimia 85 ya uchumi wa dunia na zaidi ya robo tatu ya uzalishaji wa hewa ya ukaa.
Lakini mahasimu wa utawala wa Trump wanalipa umuhimu kongamano hilo, wachambuzi walisema.
“Swali kubwa ambalo mtu anapaswa kujiuliza ni; G20 ni nini bila Marekani?” alihoji David Monyae, mkurugenzi wa Kituo cha Mafunzo ya Afrika-China katika Chuo Kikuu cha Johannesburg.
“Madhara ni makubwa zaidi kuliko Afrika Kusini…Ina maana kuporomoka kwa G20 yenyewe,” alisema. “Sidhani kama tumefika, lakini … tunaonekana tunatambaa kuelekea huko.”
Rais Cyril Ramaphosa amesema alitaka kutumia urais wa nchi yake ya G20 kushughulikia mabadiliko ya hali ya hewa na fedha za haki kwa mataifa maskini. Afrika Kusini, kama nchi nyingine nyingi, inatumia zaidi kulipa deni kuliko afya.
Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje, Chrispin Phiri alisema Afrika Kusini inafurahia “Uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa mataifa mengine ya G20” kwa ajenda yake na “itaendelea na mada na vipaumbele vyetu” bila kujali pingamizi la Marekani.
Mtimka alisema mtazamo wa Marekani unaweza kuwanufaisha wapinzani wake, kwa kukabidhi uongozi wa G20 kwa China na Urusi.
Rais Xi Jinping wa China alichukua jukumu muhimu katika mkutano wa mwisho wa G20 nchini Brazil, akitangaza hatua kadhaa za kusaidia nchi zinazoinukia kiuchumi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi atahudhuria mikutano ya Februari 20-21 mjini Johannesburg. Pia, Sergei Lavrov wa Urusi atahudhuria.
“China inatilia maanani ushirikiano wa G20 na iko tayari kufanya kazi na pande zote kuunga mkono kazi ya Ikulu ya Afrika Kusini,” ilisema Wizara ya Mambo ya Nje ya China.
Shirika la habari la Interfax la Urusi limemnukuu ofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje Jumatatu iliyopita akisema wanachama kadhaa wa G20 kutoka nchi zinazoendelea tayari wamekaribia Urusi na mapendekezo na walikuwa na nia ya kukutana na Lavrov mjini Johannesburg.
Nguvu ya G20 inatatizwa na mwingiliano wa wanachama na BRICS, kambi iliyoanzishwa ili kupinga mpangilio wa dunia unaotawaliwa na Marekani na washirika wake wa Magharibi. China, Russia, Brazil, India na Afrika Kusini ni wanachama.
Mwezi uliopita, Trump alionya wanachama wa BRICS dhidi ya kuchukua nafasi ya Dola ya Marekani kama sarafu ya akiba, akirudia kitisho la kodi cha asilimia 100 alichotoa wiki kadhaa baada ya kushinda uchaguzi wa Rais wa Marekani.
Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa G20 unatazamiwa kufuatiwa na mkutano wa mawaziri wa fedha utakaofanyika Februari 26-27, ambao Waziri wa Fedha wa Marekani, Scott Bessent hajasema iwapo atahudhuria.
Afrika Kusini inashikilia urais wa G20 hadi Desemba, itakapokabidhi kwa Marekani. Mkutano wa viongozi umepangwa kufanyika Novemba.