Trump amuunga mkono kuwania ubunge wa US mwanasiasa anayewachukia Waislamu

Rais mteule wa Marekani Donald Trump amemhimiza mbunge wa Florida ambaye alisherehekea mauaji ya raia wa Marekani yaliyofanywa na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kuwania kiti cha bunge la Congress.

Trump amesema katika andiko aliloweka kwenye mtandao wa kijamii mapema leo kwamba ikiwa Seneta wa Jimbo Randy Fine ataamua kuwania kiti cha ubunge kwa jimbo la Florida, atapata “Uidhinishaji wake Wote na Kamili”.

Fine, ambaye ana rekodi ndefu ya utoaji kauli chafu dhidi ya Waislamu, alizua hasira mapema mwaka huu aliposifu mauaji ya Aysenur Ezgi Eygi, mwanaharakati Mmarekani aliyeuawa kwa kupigwa risasi na jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kwa mabavu.

“Rusha mawe, pigwa risasi. Punguza mmoja #GaidiMuislamu. #Sema tu,” ndivyo alivyoandika Fine kwenye ujumbe alioweka katika mtandao wa kijamii mnamo mwezi Septemba.

Eygi alikuwa akishiriki maandamano ya amani katika Ukingo wa Magharibi alipopigwa risasi na askari wa Kizayuni. Israel na serikali ya Marekani inayomaliza muda wake ya Joe Biden zimepuuzilia mbali mauaji yake kwa kuyaita kuwa ni ajali.

Rasha Mubarak, mwanaharakati Mmarekani mwenye asili ya Palestina kutoka jimbo la Florida amesema, “Randy Fine si rafiki wa mtu yeyote isipokuwa ufashisti”. 

Mubarak ameongeza kuwa hatua ya Trump ya kumuidhinisha kijazba mbunge huyo wa bunge la Florida kuwania kiti cha Kongresi inaashiria kuimarika mshikamano na vitendo ya machafuko, ya kifashisti ndani ya tabaka la ubepari, ambao masilahi yake yanakidhiwa kwa kupanda mbegu za mgawanyiko na kuendeleza utawala wa kibeberu”…/