Rais mteule wa Marekani Donald Trump amemteua mbunge wa chama cha Republican Elise Stefanik, muungaji mkono mkubwa wa utawala wa Kizayuni wa Israel na mpinzani mkali wa Iran kuwa balozi ajaye katika Umoja wa Mataifa.
Trump amesema katika taarifa kwa vyombo vya habari jana Jumatatu: “nina heshima kumteua Mwenyekiti Elise Stefanik kuhudumu katika Baraza langu la Mawaziri kama Balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa. Elise ni mpiganaji hodari sana, madhubuti na mwerevu wa Marekani Kwanza”.
Iwapo ataidhinishwa na Seneti, Stefanik, ambaye ni mbunge wa New York, atachukua nafasi ya mwanadiplomasia Linda Thomas-Greenfield, ambaye amekuwa akiiwakilisha Marekani katika Umoja wa Mataifa tangu 2021.
Katika andiko aliloweka kwenye X siku ya Jumapili, Stefanik alisema, Marekani iko “tayari kurejea kwenye kampeni ya Rais Trump ya SHINIKIZO LA JUU KABISA dhidi ya Iran” akidai kwamba Tehran “imetiwa moyo na udhaifu wa serikali ya Biden na Harris.”

Mbunge huyo wa chama cha Republican amekuwa mmoja wa wakereketwa na waungaji mkono wakubwa wa utawala wa Kizayuni wa Israel wakati wa vita vyake vya kinyama na mauaji ya kimbari unayoendelea kufanya dhidi ya Wapalestina wa Ghaza na dhidi ya wananchi wa Lebanon.
Stefanik aliunga mkono pia uamuzi wa utawala wa Kizayuni wa kulipiga marufuku Shirika la Misaada na Kazi la Umoja wa Mataifa kwa Wapalestina (UNRWA).
Mapema mwezi huu, alisikika akisema: “serikali ya Biden na Harris imetuma zaidi ya dola bilioni moja kwa ajili ya UNRWA tangu 2021, kujaza hazina ya safu hii ya kigaidi. Hili lazima likomeshwe”…/