
Dar es Salaam. Rais wa Marekani, Donald Trump ameibua wimbi jipya la mvutano wa kiuchumi duniani kwa kutangaza ushuru unaolenga mataifa kadhaa, ikiwamo China na washirika wa karibu kama Canada na Mexico.
Hatua hii inayoonekana kama silaha ya kiuchumi imeibua mtafaruku katika masoko ya fedha duniani, huku wasiwasi kuhusu mustakabali wa biashara za kimataifa ukizidi kuongezeka.
Tangazo hilo, lililotolewa Aprili 2, 2025, limezua taharuki kubwa katika masoko ya hisa ya Ulaya, Asia na Marekani, na kulazimisha wawekezaji kuchukua tahadhari.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la BBC, Aprili 7, 2025, masoko ya kimataifa yameshuhudia kuporomoka kwa thamani kwa kiwango kikubwa tangu Trump atangaze ushuru huo.
Barani Ulaya, CNN iliripoti kuwa Soko la FTSE 100 la London lilishuka kwa asilimia 4, huku Hang Seng Index ya Hong Kong ikiporomoka kwa asilimia 13 – kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu 1997.
Hali ilikuwa mbaya zaidi kwa sekta ya teknolojia ya China, CNBC imeeleza kuwa, MSCI Tech 100 ya China imeshuka kwa asilimia 17, ikifuta faida zote zilizopatikana tangu Trump arudi madarakani.
Uamuzi wa Trump unalenga kurekebisha kile anachokiita “unyonywaji wa muda mrefu wa Marekani,” kwa kutumia sera ya ushuru ili kulinda viwanda vya ndani na kuimarisha ajira kwa Wamarekani. Akizungumza na vyombo vya habari Aprili 7, alisema: “Tumepata nafasi moja ya kufanya hivi, hakuna Rais mwingine atakayefanya ninachofanya.”
China, ambayo ndio shabaha kuu ya mashambulizi ya kiuchumi ya Marekani, imejikuta katikati ya mzozo huu.
Ushuru mpya wa Marekani dhidi ya bidhaa za China umeongezeka hadi kufikia asilimia 34, kutoka asilimia 20 ya awali.
Trump ameonya kuwa, kama China haitapunguza ushuru wake ifikapo Aprili 8, 2025 Marekani itaongeza ushuru hadi asilimia 50 kwa bidhaa zote kutoka China, hatua ambayo Beijing imeitaja kuwa ya “unyanyasaji wa kiuchumi.”
Katika taarifa yake kupitia mtandao wa kijamii wa Truth Social, Trump alisema, “mazungumzo yote na China kuhusu mikutano waliyoiomba na sisi yatakatishwa!”
Ishara ya wazi ni kuwa, vita hivi havitamalizika kwa mazungumzo mepesi.
China, kupitia Gazeti la People’s Daily, lilijibu kuwa: “Mbingu hazitaanguka. Tangu 2017, tumekuwa tukionyesha ustahimilivu na kadiri shinikizo linavyoongezeka, ndivyo tunavyokuwa na nguvu zaidi.”
Wataalamu wa uchumi wanaonya kuwa mwelekeo wa mapambano ya ushuru unaweza kuharibu uchumi wa dunia. Hii ni kwa sababu China na Marekani ni nguvu kuu za uchumi wa dunia, na mzozo wao unaathiri mataifa mengine kupitia minyororo ya usambazaji wa bidhaa, uwekezaji na bei za bidhaa kimataifa.
Athari kwa Afrika na Tanzania
Afrika, licha ya kutokuwa kiini cha vita hivi, haiwezi kuepuka athari zake. Ushuru wa asilimia 30 dhidi ya bidhaa kutoka Afrika Kusini na asilimia 50 kwa Lesotho, unaashiria kuwa bara hili linaingia kwenye jicho la dhoruba la mvutano wa kiuchumi.
Kwa nchi kama Tanzania, zinazotegemea masoko ya kimataifa kuuza bidhaa kama kahawa, pamba na tumbaku, matokeo yanaweza kuwa kupungua kwa bei, usumbufu kwenye usafirishajina kushuka kwa mapato ya kigeni.
BBC iliripoti Aprili 3, 2025 kuwa ushuru wa Marekani dhidi ya nchi za Afrika unaweza kupunguza ushindani wa bidhaa barani humo, hasa ikizingatiwa kuwa nchi nyingi zinategemea mnyororo wa usambazaji kutoka China na Ulaya.
Vilevile, gharama za uagizaji wa bidhaa kutoka China, kama vifaa vya ujenzi, teknolojia na mashine zinatarajiwa kupanda, jambo litakalokwamisha miradi ya maendeleo na kuongeza gharama kwa sekta binafsi barani Afrika.
Dunia iko wapi?
Katika mazingira haya ya vita vya kibiashara vilivyovaa sura ya vita vya kiuchumi, dunia inatazama kwa tahadhari kubwa hatua za China na Marekani.
Huku Trump akisisitiza sera ya ‘Marekani Kwanza’ bila kuonesha dalili za kulegeza msimamo, wasiwasi ni unaweza kupinduka na kuwa mzozo mkubwa wa uchumi wa kimataifa.
Kwa Afrika, ambayo tayari inakabiliwa na changamoto nyingi za maendeleo, hali hii inaweza kuzidisha utegemezi, kupunguza uwekezaji wa kigeni na kuongeza ukosefu wa ajira. Kwa Tanzania, changamoto ziko katika biashara, usafirishaji na utegemezi wa bidhaa kutoka nje.
Hali inayoendelea ni somo kwa mataifa yanayoendelea kuangalia njia za kujitegemea kiuchumi, kupanua masoko ya ndani na kupunguza utegemezi wa nchi chache zenye nguvu. Vita vya kiuchumi kati ya China na Marekani sasa si suala la mataifa hayo mawili tu ni suala la dunia nzima.