Rais wa zamani Donald Trump ambaye anaongoza kwa mujibu wa kura zilizohesabiswa dhidi ya Makamu wa Rais Kamala Harris katika kinyang’anyiro cha urais wa 2024 tayari amejitangaza kuwa mshindi huku akitazamia kurejea kwa muhula wa pili katika Ikulu ya White House.
Vyombo vya habari vya Marekani vimekadiria kuwa Trump amepata ushindi katika majimbo 26, yakiwemo Texas, Florida na Ohio pamoja na majimbo mengine kadhaa yanayoegemea upande wa Republican.
Harris amepata ushindi katika majimbo 19, yakiwemo majimbo makubwa ya California, New York na Washington.
Kufikia sasa, Trump ameshinda kura 267 na Harris 224 za wajumbe wa kamati maalumu ya uchaguzi nchini Marekani maarufu kama Electoral College. Matokeo yote si rasmi hadi maafisa wa uchaguzi wa maeneo yote watakapothibitisha matokeo rasmi katika siku zijazo.
Akiwahutubia wafuasi wake katika Kituo cha Mikutano cha West Palm Beach huko Florida Jumatano asubuhi, Trump ametangaza ushindi wake lakini Harris bado hajakubali kushindwa.

Usalama umeimarishwa katika viwango visivyo vya kawaida kutokana na wasiwasi juu ya uwezekano wa kutokea machafuko na ghasia za baada ya uchaguzi.
Kila mgombea anahitaji kura 270 za Electoral College ili kupata ushindi kamili.
Kwa kuzingatia yale yaliyojiri katika uchaguzi uliopita, inaweza kuchukua siku kadhaa kwa matokeo ya jumla kutangazwa.
Huko Ulaya, matarajio ya muhula wa pili wa Trump yameonekana kuwasumbua sana baadhi ya viongozi, huku baadhi ya wafuasi wa Trump katika chama cha Warepublican wakitishia mara kwa mara kujiondoa kutoka muungano wa kijeshi wa NATO.
Waziri mkuu wa utawala haramu wa Israel Benjamin Netanyahu hakusubiri matokeo ya mwisho kutolewa, na amekimbilia kumpongeza Trump.
Kuhusu uhusiano wa Marekani na Iran, Harris na Trump wote daima wamekuwa na misimamo mikali kuhusu Jamhuri ya Kiislamu.