
Zikiwa zimepita siku sita tangu Rais Donald Trump atie saini amri ya kiutendaji inayoelekeza Marekani kujitoa kwenye Shirika la Afya Duniani (WHO), ametangaza kufikiria kubadili uamuzi wake huo.
Hatua hiyo imekuja baada ya WHO kutangaza kufanya mazungumzo na Marekani na kumuomba kiongozi huyo kufikiria upya.
Mbali na WHO, Ujerumani, mfadhili wa pili kwa ukubwa wa shirika hilo, pia ilimuomba Trump kutafakari uamuzi wake huo.
Baada ya Trump kutangaza uamuzi wake wa kujitoa WHO, Ujerumani ilichukua hatua ya kuzungumza naye.
Waziri wa Afya wa Ujerumani, Karl Lauterbach, amesema: “Tangazo la Rais wa Marekani ni pigo kubwa kwa mapambano ya kimataifa dhidi ya matatizo ya afya duniani. Tutajaribu kumshawishi Trump kufikiria upya uamuzi huu.”
Hata hivyo, akizungumza kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Las Vegas eneo la Circa Resort & Casino, jana Jumamosi, Januari 25, 2025, Trump amesema atafikiria tena uamuzi huo lakini alionekana bado hana hakika, “sijui, wanapaswa kuisafisha kidogo.”
Trump amesema uamuzi wa Marekani kujitoa WHO ulitokana na hisia kwamba nchi yake ilikuwa na mzigo mkubwa zaidi kifedha ukilinganisha na China.
Marekani, yenye watu takribani milioni 331, ilichangia Dola 500 milioni za Marekani (Sh1.242 trilioni) kwa mwaka, huku China, yenye watu bilioni 1.4, ikichangia Dola 39 milioni (Sh96.110 bilioni) pekee.
Uamuzi huo ulikuwa moja ya maagizo ya kwanza ya Trump baada ya kuapishwa Januari 20, 2025, akidai WHO haikufanya mageuzi ya haraka wakati wa janga la Uviko-19.
Hata hivyo, wakati wa urais wake wa awali (2017–2021), mpango wake wa kuiondoa Marekani kutoka WHO ulizimwa na rais Joe Biden baada ya kushinda uchaguzi wa 2020.
Wafadhili wakuu wa WHO
Marekani inaongoza kama mfadhili mkubwa wa WHO, ikifuatiwa na Bill and Melinda Gates Foundation kupitia hazina ya The Global Fund.
Gavi, shirika linaloshirikisha mashirika ya umma na serikali kwa kampeni za chanjo, ni mfadhili mwingine mkubwa.
Mataifa mengine kama Ujerumani, Tume ya Ulaya, Norway, Korea Kusini, Luxembourg, India na Hispania pia huchangia kwa kiwango kikubwa.
Mchango wa Marekani
Kwa mujibu wa takwimu za WHO kwa miaka 2018–2019, asilimia kubwa ya fedha za Marekani zilitumika Mashariki ya Kati.
Pia, nchi 22, kuanzia Morocco hadi Pakistan, zilipokea Dola 201 milioni (Sh495.466 bilioni), sawa na asilimia 36 ya mchango wa Marekani.
Bara Afrika, lilipokea Dola 151 milioni (Sh372.213 bilioni), ikiwa ni eneo la pili kwa kupokea ufadhili mkubwa wa Marekani, pia makao makuu ya WHO yalipokea Dola 101 milioni (Sh248.960 bilioni) za shughuli za uendeshaji na kampeni mbalimbali.
Kwa upande wa Amerika ya Kusini na Caribbean, mchango ulikuwa Dola 280,000 (695.771 milioni) pekee, sawa na asilimia 0.5 ya ufadhili wa Marekani.
Matumizi ya ufadhili
Zaidi ya robo ya fedha za Marekani Dola 158 milioni (Sh392.601 bilioni) zilitengwa kwa kampeni za kutokomeza polio duniani.
Miradi mingine ni pamoja na afya bora na lishe Dola 100 milioni (Sh248.489 bilioni), utoaji wa chanjo dhidi ya magonjwa yanayozuilika Dola 44 milioni (Sh109.335 bilioni) na mapambano dhidi ya kifua kikuu Dola 33 milioni (Sh81.999 bilioni).
Fedha nyingine zilitengwa kwa miradi ya kupambana na Ukimwi, homa ya ini, magonjwa ya kitropiki, afya ya uzazi, upatikanaji wa dawa na hatua za kudhibiti majanga.
Umuhimu wa WHO
WHO ilianzishwa mwaka 1948 kama sehemu ya Umoja wa Mataifa (UN) kwa lengo la kuendeleza afya bora, kuhakikisha usalama wa dunia na kuwasaidia walio hatarini zaidi.
Shirika hilo hupata fedha kutoka kwa michango ya lazima ya wanachama na michango ya hiari kutoka kwa nchi na washirika.
Michango ya lazima
Nchi wanachama 194 huchangia kulingana na utajiri wa nchi na idadi ya watu. Fedha hizi hutumika kugharamia mishahara na shughuli za kimsingi za WHO.
Michango ya hiari huwezesha kufanikisha masuala maalumu kama chanjo, afya ya wanawake na kudhibiti matumizi ya tumbaku. Kwa mfano, kati ya mwaka 2022–2023, Marekani ilichangia Dola 1.284 bilioni (Sh3.189 trilioni) kusaidia vipaumbele vya afya duniani.