TRC yaongeza safari za treni, barabara Dar zikifungwa

Dar es Salaam. Kufuatia mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi za Afrika unaofanyika kwa siku mbili jijini Dar es Salaam, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeongeza treni mbili za safari katikati ya jiji hilo ili kukidhi mahitaji ya usafiri.

Taarifa iliyotolewa leo, Jumatatu, Januari 27, 2025, na Mkuu wa Kitengo cha Habari na Uhusiano, Fredy Mwanjala, imezitaja treni hizo kuwa ni za Stesheni ya Kamata na Pugu, zitakazofanya safari saa 12:00 asubuhi kutoka Kamata na saa 12:05 jioni kutoka Pugu.

“Shirika la Reli Tanzania linapenda kuwatangazia kuwa, kutokana na kufungwa kwa barabara za kuingia katikati ya Jiji la Dar es Salaam kufuatia mkutano wa nishati wa wakuu wa nchi za Afrika, shirika limeongeza treni mbili za mjini kati ya Stesheni ya Kamata na Pugu jijini Dar es Salaam kwa tarehe 27 na 28, Januari 2025,” imeeleza taarifa hiyo.

Hata hivyo, Mwanjala amesema kuwa, pamoja na hatua hiyo, ratiba za awali za treni zitabaki kama kawaida.

 Amefafanua kuwa treni hizo za ziada zitafanya kazi kwa saa zilizotajwa pekee, kipindi ambacho abiria wengi huenda kazini asubuhi na kurejea nyumbani jioni.

Katika ratiba ya kawaida ya treni za Pugu ipo ya saa 10:45 asubuhi (DSM kwenda Pugu), saa 12:00 mchana (Pugu kwenda DSM), saa 1:10 mchana (DSM kwenda Pugu), saa 2:10 mchana (Pugu kwenda DSM), saa 3:10 alasiri (DSM kwenda Pugu) na saa 4:10 alasiri (Pugu kwenda DSM).

Wakati mchana ipo ya saa 9:45 asubuhi (DSM kwenda Pugu), saa 11:00 mchana (Pugu kwenda DSM), saa 12:05 jioni (DSM kwenda Pugu), saa 1:00 usiku (Pugu kwenda DSM), saa 2:15 usiku (DSM kwenda Pugu) na saa 3:10 usiku (Pugu kwenda DSM).