TRA yakabidhi serikalini gari lililoingizwa kimagendo nchini

Songea. Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Ruvuma, Nicodemas Mwakilembe, amekabidhi gari aina ya Isuzu kwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, baada ya mmiliki wake kushindwa kulipa gharama ya Sh60 milioni ikiwa ni gharama za ushuru na adhabu ya kuingiza gari hilo nchini bila kufuata utaratibu wa forodha.

Akizungumza wakati wa makabidhiano hayo yaliyofanyika leo Jumatano Mei 7, 2025 katika Ofisi za TRA Mkoa wa Ruvuma, Meneja huyo amesema gari hilo lilikamatwa katika Kijiji cha Lusewa, Wilaya ya Tunduru, likiwa linapakia mazao.

“Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) waliokuwa wakifanya doria walilitilia shaka baada ya kugundua kuwa lina namba za usajili za kigeni. Walipowasiliana na TRA, mfumo ulionyesha gari hilo liliingia nchini kwa mara ya kwanza Februari 2024 na kisha kuondoka, kabla ya kurejea tena kwa njia ya magendo,” amesema Mwakilembe.

Amesema TRA iliwasiliana na mtu aliyekutwa na gari hilo ambaye alitoa mawasiliano ya mmiliki halisi ambaye aliahidi kulikomboa kwa kulipa kiasi cha fedha hizo.

Hata hivyo, ofisa huyo amesema mpaka sasa hajalipa fedha hizo.

Amesema kwa mujibu wa sheria za forodha, mali inayokamatwa inapaswa kulipiwa ndani ya siku 90, na endapo hilo halitafanyika, mali hiyo hukabidhiwa kwa taasisi ya serikali.

“Kutokana na kushindwa kulipia ndani ya muda uliopangwa kisheria na uchunguzi kuonyesha kuwa chasis ya gari imefanyiwa mabadiliko yasiyo halali, ilionekana kuwa hatari kuliuza kwa mtu binafsi. Kwa hiyo, kamati ya kodi chini ya uenyekiti wa Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas, ilipendekeza gari hilo likabidhiwe kwa ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa,” amesema Mwakilembe.

Ameongea kuwa; gari hilo ni zima na linatembea, hivyo linaweza kufanyiwa marekebisho madogo na kutumika kwa shughuli za serikali.”

Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Mary Mwakondo ameishukuru TRA kwa msaada huo akisema gari hilo litachangia katika kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi, hasa katika sekta ya elimu, usafirishaji wa mitihani na vifaa vya uchaguzi.

“Litatusaidia pia litatupunguzia utegemezi wa magari ya halmashauri katika shughuli muhimu za kiserikali,” amesema.

Ameelekeza Wakala wa Ufundi na Umeme wa Serikali (Tamesa) kulifanyia ukaguzi gari hilo na kuwasilisha ripoti ya vifaa vinavyohitajika ili lifanyiwe matengenezo lianze kazi mara moja.

Fundi Mkuu wa Tamesa, Pato Mkanura, ameipongeza TRA kwa kukabidhi gari hilo kwa serikali na ameahidi kulifanyia ukaguzi wa kina kama alivyoelekezwa na Katibu Tawala wa Mkoa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *