Mwanza. Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF Net) mkoa wa Mwanza umeadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani (IWD) kwa kuwatembelea na kutoa msaada wa mahitaji kwa wagonjwa waliolazwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure.
Miongoni mwa wagonjwa waliolazwa Sekou Toure waliofikiwa na msaada wa TPF Net mkoani Mwanza ni pamoja na wodi wazazi kwa njia ya upasuaji.
Akizungumzia msaada huo leo Jumatano Machi 5,2025, Mkazi wa Mabatini mkoani Mwanza, Winfrida Temba amesema changamoto ya kulazwa hospitalini imesababisha ukata kwa ndugu jambo lililomuwia vigumu kupata mahitaji ya msingi ikiwemo taulo za kike na sabuni. Hata hivyo amesema msaada huo utasaidia kupunguza gharama ya kununua mahitaji hayo.

Mwenyekiti wa TPF Net Mkoa wa Mwanza, Virginia Sodoka akikabidhi boksi la taulo za kike kwa mwanamke aliyejifungua hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mwanza ya Sekou Toure. Picha na Mgongo Kaitira
“Nawashukuru sana Polisi wanawake kwa huruma yao, wanawake tunapaswa kupendana hivi na kukumbukana hasa ambao tumelazwa hospitalini. Na mimi nimejisikia vizuri kuwa kumbe wanawake wenzangu wanatukumbuka,” amesema Temba.
Akizungumza huku akiugulia maumivu, Elizabeth Philbert aliyefanyiwa upasuaji wakati wa kujifungua hospitalini hapo, amewaomba wanawake wanapoadhimisha siku yao kuwakumbuka wenzao wanaopitia changamoto ikiwemo magonjwa hata kwa maombi.
“Tumefurahi kwa kututembelea na kutupatia msaada huu wa mahitaji ya wanawake, Mungu awabariki. Tuendelee kuombeana na sisi tupone turejee kwenye shughuli zetu za uzalishaji,” amesema Elizabeth.
Akizungumzia uamuzi huo, Mganga Mfawidhi Hospitali ya Sekou Toure, Dk Bahati Msaki amesema kwa nyakati tofauti kumekuwepo na changamoto (bila kutaja takwimu) ya wagonjwa kushindwa kujigharamia mahitaji yao ya msingi wanapokuwa wamelazwa hospitalini hapo.
Dk Msaki amesema miongoni mwa njia zinazotumika kuwasaidia wagonjwa wa aina hiyo ili kuwawezesha kuendelea na matibabu bila hofu ni pamoja na mahitaji ya msingi kutoka kwa wadau wakiwemo Jeshi la Polisi.
“Niwaombe wadau wakiwemo kampuni na mashirika ya umma hususan wanawake kuendelea kujitokeza kwa wingi kuadhimisha Siku ya Kimataifa ya Wanawake kwa kuwa sehemu ya faraja kwa wagonjwa hospitalini kwetu,” amesema Dk Msaki.
Pia amesema Sekou Toure inaadhimisha kilele cha siku hiyo kwa kutoa huduma ya uchunguzi wa magonjwa bila malipo hususan uchunguzi wa saratani ya matiti, mlango wa shingo ya kizazi na magonjwa yasiyoambukiza.
Awali, Mwenyekiti wa TPF Net Mkoa wa Mwanza, Virginia Sodoka amesema msaada huo ni sehemu ya kurejesha kwa jamii kuelekea kilele cha Siku ya Kimataifa ya Wanawake Duniani, huku akisema kufanya hivyo kutalisogeza Jeshi la Polisi na jamii.

“Lengo la kufanya hivi ni kuwapa faraja, pia tuna ushirikiano na jamii ikiwemo utoaji wa elimu, kuwaona wagonjwa na kufanya usafi maeneo mbalimbali kwani tukiwa karibu nao itakuwa rahisi kutupa ushirikiano ili kutokomeza uhalifu,” amesema Sodoka.